Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mafinga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Nami kwa kuanza, naunga kabisa mkono hoja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Wakala wa Misitu Tanzania kwa niaba ya watu wa Mafinga kwa ushirikiano wao chini ya usimamizi wa Chama cha Mapinduzi tumeweza kujengewa mabweni mawili. Hivi ninavyozungumza tutapewa fedha kiasi cha shilingi milioni 130 kwa ajili ya kutengeneza lami nyepesi pale kwenye eneo letu la soko kubwa katika Wilaya ya Mufindi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kutoa shukrani zangu za dhati, lakini yale mabweni tuliyojenga ni ya girls. Sasa boys wanatuuliza, pale Luganga Secondary na Changarawe Secondary wanasema mbona sisi mmetusahau? Kwa hiyo, natumia fursa hii pia kuwasilisha kama ombi kwa Serikali kwamba kama tumeanza na girls, which is good, kwa sababu, wako kwenye higher risk, basi tuwaangalie pia na boys. Nitumie nafasi hii pia kutoa wito kwa wawekezaji wengine waige Wakala wa Misitu Tanzania kwa sababu, tunashirikiana nao vizuri sana katika suala zima la CSR.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumekuwa tukishirikiana nao, wakati mwingine tunaazima ma-grader kutoka Sao Hill sisi Halmashauri tunajaza mafuta tunatengeneza barabara zetu. Japokuwa mwaka huu walikuwa wametingwa sana, sasa naomba wakipunguza kutingwa kidogo, watusaidie ma- grader sisi tutajaza mafuta, tutapunguza kidogo kero ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, napenda nifahamishe Bunge lako na Watanzania kwa ujumla kwamba, msitu wa Sao Hill, kutokana na mapato yake, Serikali katika misitu inapata asilimia 35 kutoka katika Msitu wa Sao Hill tu ambapo Makao Makuu yake yako pale Mafinga. Nitumie nafasi hii kuwashukuru sana kamati, walifanya pale ziara na hata katika taarifa yao wameandika na wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na campus ya Chuo cha Misitu pale Mafinga, kwa sababu, itasaidia hata wanafunzi kwenda kupata mafunzo kwa vitendo katika ule msitu ambao ni mkubwa katika Afrika Mashariki na Kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na ukubwa wa msitu huu ambao kwa mujibu wa takwimu kwa mwaka tunapata karibu takribani shilingi bilioni 42. Kati ya mwaka 2015 hadi 2020 tumepata kama shilingi bilioni 216 kwa maana Serikali imepata hizo fedha. Hata hivyo, kasi ya wavunaji kwenda msituni imeendelea kupungua kutokana na wingi wa tozo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninapozungumza hapa, kuna tozo 13 katika sekta ya misitu. Tozo mojawapo ni LMDA. Tozo hii ilianzishwa ili kuisaidia Serikali kupanda miti kwa sababu kwa muda mwingi lile shamba halikupanda miti. Sasa hivi miti imepandwa kwa wingi, naishauri Serikali ingetoa tozo hii ili kusudi kupunguza gharama za watu kwenda msituni.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni tozo katika VAT. Najua tutakwenda kwenye Muswada wa Fedha. VAT ni Kodi ya Ongezeko la Thamani, lakini wananchi wa Mafinga na Mufindi anapoenda kukata tu ule mti nao anatozwa VAT. Ni ongezeko gani la thamani limeongezeka katika ule mti? Sasa matokeo yake wavunaji hawaendi kuvuna msituni, Serikali haipati mapato. Of course wanaenda kuvuna kwa wananchi ambao miti haitoshelezi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu, kuna vitu amesema hapa Mheshimiwa Nape, hata katika wanyamapori, ziko tozo ambazo nadhani tuziangalie kwa macho mawili, kwa sababu, inavyokuwa sasa, yaani msitu unao, fedha hauna. Sasa unakosa shilingi kumi ambayo bora uikose shilingi kumi ambayo ingekuzalishia wewe shilingi 100 katika mtiririko mzima wa Ongezeko la Thamani. Kwa hiyo, naiomba sana Serikali, suala la VAT litazamwe sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo ipo katika masuala ya wanyamapori, vitalu vingi sasa vimekaa idle. Vikikaa idle madhara yake wale watu wanaokuwa wanakodishwa vitalu, mojawapo ya masharti ni pamoja na kufanya uhifadhi katika vile vitalu. Sasa vikikaa idle maana yake kwamba uhifadhi unakuwa haifanyiki, vinashuka thamani. Kwa hiyo, Serikali ifike wakati tuangalie, kuna wakati bora ukose shilingi kumi ukapata shilingi 100. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni migogoro ya wakulima na wafugaji. Nasema hapa, bila kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, tutaendelea kila mwaka kuongeza maeneo. Nina takwimu hapa kidogo tu; katika Tanzania sisi, nchi yetu, population wise, yaani population density, sisi ni watu 67 per kilometer square. Nchi kama Rwanda ni watu 525 per kilometer square. Burundi 463 per kilometer square. Malawi 205 per kilometer square. Kwa hiyo, ukiangalia population density sisi siyo kwamba tuko over populated, ila tunachotakiwa kufanya ni kitu kimoja; tunaanza kwenye kilimo. Lazima tulime kilimo chenye tija. Hiki kilimo cha kudhani kwamba ukilima ekari nyingi ndiyo utapata mahindi mengi, hakitatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ufugaji lazima tufuge ufugaji wenye tija. Siyo kwamba ukiwa na ng’ombe 10,000 ndiyo utapata maziwa mengi. Sasa kutokana na kwamba hatujawekeza tija katika kilimo kwamba, ekari moja inakupa gunia tatu, sasa kumbe eka moja ingekupa gunia 20 usingelima eka kumi. Sasa matokeo yake ili upate magunia 30 unalima ekari kumi; ili upate nyama nyingi, unafuga ng’ombe wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, natoa wito kwa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wawasaidie wakulima na wafugaji wa nchi hii wafuge na kulima kwa tija. Vinginevyo ardhi ya nchi hii haitakaa itoshe. Watakuja watu wa Maliasili na Utalii hapa mtawasulubu. Hao ng’ombe hawataacha kwenda kwenye hifadhi na migogoro ya wakulima na wafugaji haitakaa iishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suluhisho, ni lazima tulime kwa tija, eneo dogo lizalishe sana; tufuge kwa tija, eneo dogo upate mifugo inayokupa tija. Kinyume chake, nchi hii tutakuwa kila siku tuna-declare kuongeza maeneo ya wakulima na wafugaji wakati we are not overpopulated kama nchi nyingine ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge. Bila kufanya hivyo, migogoro haitakwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. Nashukuru. (Makofi)