Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naomba nishukuru sana kwa kupata fursa hii ya kuchangia Wizara ya Maliasili na Utalii na hasa ukizingatia kwamba, utalii upo Kaskazini. Karibu asilimia 80 ya mapato yote ya utalii yanatoka Kanda ya Kaskazini; na huwezi kuzungumza Kaskazini bila kuizungumza Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda nitajielekeza kwenye masuala machache. La kwanza, tunafahamu sote kwamba Corona imetuathiri sana kama Tanzania. Nilikuwa nasikia taarifa ya Waziri kwenye ukurasa wake wa saba na wa nane bado anazungumzia kwamba utalii unachangia pato la Taifa kwa asilimia 17 na unachangia fedha za kigeni kwa asilimia 25. Nadhani hizi taarifa ni za zamani sana kwa sababu kwa namna Corona ilivyotuathiri, mapato yetu yameyumba sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia taarifa zilizopo, kwa mujibu wa taarifa ya Wizara, TANAPA mpaka kufikia mwezi Februari, walikusanya asilimia 13, Ngorongoro asilimia 21 na TAWA asilimia 38. Ukiangalia pia taarifa ya Mheshimiwa Waziri ya leo kwenye ukurasa wake wa 10 na wa 11 anatuambia hadi kufikia mwezi wa Nne target yetu ilikuwa ni shilingi bilioni 584 na sisi tumekusanya shilingi bilioni 89 ambayo ni sawa sawa na asilimia 15, lakini ukienda kuangalia pia kwenye World Tourism Organization, tunaambiwa kwamba mchango wa utalii kwenye GDP umeshuka kutoka asilimia 17.5 mpaka asilimia 11.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kushangaza, bado Wizara ya Utalii wanakwenda kuongeza tozo kwenye maeneo mbalimbali. Tukiangalia nchi zote za Afrika Mashariki; Uganda wamepunguza park fees kwa asilimia 50, Kenya wamepunguza park fees kwa asilimia 47, lakini Tanzania tunaongeza. Vilevile cha kushangaza, ukiangalia dunia nzima sasa hivi inahangaika kwenye kutoa ahueni kwenye sekta ya utalii, lakini Tanzania tunaongeza tozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninalo tangazo hapa la TANAPA ambalo limetokana na GN ya Serikali ya tarehe 29 Juni, 2020 ambalo wanaongeza kipindi cha High Season tozo kutoka dola 60 mpaka dola 70 ambazo bado hazijaanza, wanategemea zianze tarehe mosi mwezi wa Saba, yaani mwaka wa fedha unaokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukiangalia TANAPA hao hao kuna tozo nyingine ambayo pia wanakuja kuiongeza; ni tozo mpya hii, wanaita Land Base, Land Fee; yaani mtu amewekeza kwenye hifadhi zetu mfano Serengeti au maeneo mengine, analipa Concession Fee, kila mgeni aliyelala pale analipa dola 50. Leo TANAPA wanakuja wanaongeza pia, inabidi mtu anayeweka kule kama ni Seasonal Camp inabidi alipe dola 2,000, kama anaweka Permanent Tented Camp alipe dola 20,000, kama ana lodge yake, alipe dola 50,000. Kwa hiyo, unashindwa kuelewa tatizo letu ni nini? Kila tukikaa tunafikiria kuongeza tozo.

Mheshimiwa Naibu Spika, najua tatizo hili lipo TANAPA kwa sababu tunazo hifadhi 22 ambazo ziko chini ya TANAPA. Hifadhi ambazo zina uwezo wa kujiendesha hazizidi tano, hifadhi nyingine zote zinategemea hifadhi tano ziweze kujiendesha. Matokeo yake sasa kila wakilala wakiamka wanaongeza tozo Serengeti, wanaongeza tozo na maeneo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa nadhani kwamba ni vizuri Serikali ikaiona changamoto hii ya Corona kwa uzito wake na kuangalia uwezekano wa kukaa vizuri na wenzetu wa TANAPA ili wasiweze kuongeza sana tozo kama ambavyo wanafanya. Mambo unayoyaona haya hayapo maeneo kama NCAA, wao mambo haya ya Land Base hayapo, lakini ukienda TANAPA kule unaweza ukayakuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naona bado tuna kazi ya kufanya, Wizara ya Utalii ipitie hifadhi zote ambazo tunazo. Hifadhi ambazo hazizalishi, mfano mzuri ni Burigi Chato, hebu mtuletee taarifa hapa, ile hifadhi toka imeanzishwa imepokea wageni wangapi? Imeingiza kiasi gani? Mwisho wa siku pia inatumia gharama kiasi gani? Siyo tunaanzisha hifadhi nyingi, tunaajiri watu wengi, tunapeleka gharama nyingi, halafu mwisho wa siku tunakwenda kuumiza utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, lazima mfahamu kwamba hizi gharama mnazoongeza, anayepewa hizi gharama ni mtalii. Ukimpa tour operator, anachokifanya yeye, anaingiza kwenye gharama zake, mtalii anayekuja anaongezewa gharama na kufanya destination inakuwa very expensive, kwa hiyo, nilikuwa nadhani ni vizuri tukaliangalia vizuri suala hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine pia ambalo nataka nilizungumzie ni kuhusiana na gharama za kupima Corona. Ukienda Kenya kupima Corona ni dola 30 hospitali za Serikali, private dola 50 ukija Tanzania dola 100. Sasa nashindwa kuelewa, hivi hata Corona pia ni fursa kwenye nchi yetu au ni changamoto!

Kwa hiyo, nilikuwa nadhani na lenyewe pia tuliangalie vizuri, kwa sababu Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kafanya kazi kubwa na nzuri sana kuhakikisha kwamba tunakubaliana na dunia kwamba Corona ipo, tutachukua chanjo. Sasa hivi dunia imeanza kuelewa na tunaamini muda siyo mrefu tutaanza kupata wageni wengi zaidi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najiuliza pia, kwa nini Tanzania tuna kituo kimoja tu cha kupimia Corona, pale Dar es Salaam? Ukienda kwenye airport, sawa, wanachukua zile rapid test; ukienda Kenya wana vituo 47. Nadhani ni vizuri mambo haya tukayaangalia vizuri zaidi. Naona muda ni mdogo sana na hizi mada ni very serious…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Imeshagonga kengele ya pili.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)