Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi jioni hii ili nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Dkt. Ndumbaro pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Mary, pamoja na watendaji wa Wizara hii wakiongozwa na Dkt. Allan Kijazi, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo amekuwa akiifanya. Kwa kweli wameacha alama katika kipindi kifupi hiki ambacho wameikamata hii Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Wizara ya Maliasili na Utalii katika kipindi cha miaka mitano iliyopita wamefanya kazi kubwa sana. Nami ni shahidi, tumeweza kutembea katika baadhi ya hifadhi na tumeona mabadiliko makubwa ikiwa ni pamoja na kuona hivi sasa wanyama wameongezeka sana na wale tembo ambao ilikuwa hata ukienda kwenye hifadhi zetu kuwaona ni nadra, basi hivi sasa wamekuwa ni wengi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeelezwa hapa kwamba kabla ya kupata Uhuru tulikuwa na tembo waliokuwa wakifikia 200,000 lakini hivi sasa tembo wamepungua mpaka kufika 40,000. Hivi sasa wameongezeka mpaka wamefika karibu 60,000. Haya kwa kweli ni matokeo mazuri ya uhifadhi ambao unafanywa na wenzetu hawa wa Maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika, tumekwenda kwenye Hifadhi ya Ruaha, wenyeji wametueleza pale kwamba kwa miaka kumi iliyopita Mto Ruaha kilikuwa kinafika kipindi maji yanakata karibu miezi miwili au mitatu, lakini hivi sasa Mto Ruaha kwa mwaka uliopita haukukata maji hata mara moja, umeweza kutiririsha maji kwa mwaka mzima. Haya ni matokeo ya juhudi za uhifadhi ambazo wenzetu wamekuwa wakizifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wenzetu hawa wamefanya kazi nzuri hata katika masuala mazima ya uhifadhi wa maliasili, yaani miti. Kwa sababu wenzetu wa TFS hivi sasa ukiangalia mapato ambayo wameweza kuyapata katika kipindi kilichopita pamoja na maradhi ya Covid, lakini wamevunja rekodi katika vipindi vyote vilivyopita. Yaani wakati sekta nyingine zinahangaika kwa ukusanyaji hafifu wa mapato, wao wameweza kufanya kazi nzuri na kuweza kukusanya mapato kwa kiasi kikubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kidogo katika suala muhimu la usimamizi shirikishi wa maliasili zetu nchini. Kama tunavyojua, juzi na jana, nimesikiliza kwa makini wakati michango ikitolewa katika Wizara za Maji na Nishati, tumekuwa tukizungumzia sana kuhusu uhifadhi na uvunaji wa rasilimali zaidi, yaani vipi tutapata nishati, vipi tutaunganisha tupate umeme? Ila hatuangalii na tija: Je, haya maji sustainability yake itaendelea kuwa vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tukizungumza masuala yote ya uhifadhi, ningependa tu kuwaomba wenzangu kwamba tuka-adopt ile approach ile integrated natural resources management, yaani usimamizi shirikishi. Tusiwaachie watu wa maliasili tu kwamba ndiyo wahifadhi rasilimali za misitu au rasilimali za wanyamapori. Kwa sababu tukizungumza maji wanategemea vilevile sustainability ya hifadhi ya misitu. Tukizungumza nishati wanazitegemea vilevile sustainability wa hifadhi wa misitu; tukija utalii, wanategemea vilevile sustainability ya rasilimali za misitu, hata tukija kwenye masuala mazima ya food security, pia kama hatukuweza kupata kuni na makaa katika njia endelevu, basi hata usalama wa chakula nao hautakuwa mzuri. Kwa hiyo, lazima tuje na usimamizi shirikishi ambao utajumuisha sekta zote hizi muhimu ili tuweze kuhakikisha kwamba maliasili zetu zinahifadhika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunakuja hapa tunazungumza kwamba tunataka kuifanya Tanzania kuwa ni nchi ya tembo. Hii siyo kauli nzuri sana kwa sababu, kama tunavyojua hivi sasa tuna tembo 60,000, huko nyuma tulikuwa tuna tembo zaidi ya 200,000 na tuliweza kuishi katika hali endelevu zaidi na wanyama hawa. Kwa hiyo, nafikiri ni pahala pa kujipanga kisekta tukashirikiana katika uhifadhi wa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunazungumza kuhusu Bwawa la Mwalimu Nyerere. Tunategemea pale tukapate Megawatt za umeme karibu 2100, lakini tunategemea kuanzia mwezi Aprili tuwe tumeshalijaza maji lile bwawa; na kuanzia mwezi Juni tunategemea tuanze kuchaji na kupata umeme. Wakati nazungumzia kuhusu kupata maji, hatuzungumzi kuhusu haya maji, potential threat yake ikoje kama maji hayatatiririka vizuri? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, lazima tuwa- support wenzetu wa maliasili ili wahifadhi vyanzo vya maji ili kuhakikisha kwamba bwawa letu la Mwalimu Nyerere linaweza kupata maji katika hali endelevu na kuweza kupata matunda ambayo tunakusudia. Kinyume na hivyo, tunaweza tukazungumza hapa bila kuangalia zile threats ambazo zinakabili suala hili zima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la taaluma kuanzia kwa Wabunge na wanajamii. Kwa kweli kinachoonekana ni kwamba elimu ni hafifu. Kwa hiyo, naomba wenzetu wa maliasili tujipange vizuri kuweza kuelimisha kuanzia wanajamii hapa pamoja na Wabunge kuweza kupata taaluma muhimu kwa sababu michango tunayokuwa tunaitoa hapa wakati mwingine ni kutokuwa na taarifa za kutosha katika masuala mazima ya uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mfano mdogo tu; kule Zanzibar miaka ya 1970 tulikuwa na Chui zaidi ya 1,000 na kidogo hivi, lakini hivi ninavyokwambia Chui wale wamemaliza na hakuna tena hivi sasa. Chui wameisha. Pia tulikuwa na Paanunga zaidi ya 6,000 kipindi cha miaka ya 1970. Hivi sasa Paanunga wamebakia 300 tu Zanzibar nzima. Kwa hiyo, unaweza kuona athari ya viumbe kuweza kutoweka. Tukifanya masihara tutapoteza viumbe kwa kutokuzingatia uhifadhi sahihi na kutokuwapa nguvu wenzetu wa maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimalizie suala la mifuko ya fedha. Kwa kweli mifuko ya fedha tumeamua kwamba fedha zikusanywe na watu wa TRA na ziende kwenye mfuko mkuu na baadaye ndizo zirejee tena kwa wenzetu hawa waweze kutumia. Vilevile naomba tu kutoa indhari, wenzetu katika kipindi hiki cha fedha wamepokea asilimia 32 tu ya fedha. Kwa hiyo, kama tutaendelea na utaratibu huu, zile kazi ambazo tumezipanga hazitaweza kufanyika.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante, Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)