Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kahama Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nakupongeza wewe, Mheshimiwa Waziri na timu yake nzima ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichonipelekea kuchangia kwenye Wizara hii ni kitu kimoja tu. Kuna sheria mpya hapa ame-introduce Mheshimiwa Waziri, ambayo inamtaka mtu atakayekuwa na gunia moja la mkaa, ni lazima akapate kibali kutoka Halmashauri ya Wilaya na awe na EFD machine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda wenzetu wangejaribu kuangalia jiografia ya nchi, maisha ya wananchi wetu yalivyo unapotaka kutengeneza kitu kama hiki. Ina maana tutarajie ndani ya mwezi mmoja kutatokea chaos kubwa mno ya mkaa. Je, itawezekana? Yaani kwa kawaida itawezekana watu wasipike kweli na wasile?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu wa Wizarani labda wawe wanajaribu kuangalia yanayotutesa kule majimboni. Kuna majimbo mengine kutoka kwenye Makao Makuu ya Halmashauri kwenda kule kijijini ni zaidi ya kilomita 200. Mwananchi anataka gunia moja la mkaa kwenye mti wake mwenyewe, kweli aende mpaka wilayani apate na EFD machine! Anaipata wapi EFD machine mtu wa gunia moja? Ni kitu ambacho wala hakiwezekani wala hakiingii akilini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii vita ya mkaa na kuni toka tunapata uhuru, toka wametuachia Wakoloni: Je, watu milioni 60 wanaotumia mkaa na kuni itatokea wataacha kula? Nani ataibuka mshindi kwenye hii vita? Kwa nini Wizara isirasimishe hii biashara kama tulivyofanya kwenye madini? Dhahabu tulihangaika miaka 50, lakini ilivyorasimishwa, leo hatuna matatizo na biashara ya madini. Kwa nini mkaa na kuni usirasimishwe ukaenda halali, wao wakachukua ushuru wao kwenye gulio, wakapanga kabisa pale kwamba hii miti ya Serikali ikae hapa/mbao za Serikali zikae hapa, mkaa wa Serikali ukae hapa; mkaa wa mkulima mwenyewe mti ukae hapa ili biashara hii iwe halali? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu, yeye TFS au yeye Wizara ya Maliasili na Utalii, anao kweli askari wa kutosha kuwazuia watu milioni 60 wa Tanzania wasipike? Yeye mwenyewe hapa amekula chakula cha mkaa, sisi tumekula chakula cha mkaa, anayekamata amekula chakula cha mkaa. Itawezekana? Ni kitu ambacho hakiwezekani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna sababu ya kupigana vita usioshinda? Leo mkaa, kwa wenzetu Namibia na South Africa inaitwa dhahabu nyeusi, ni fedha. Sasa kama leo unasema kwamba huyu mwananchi tukamzuie kuchoma mkaa, nawe unatuambia tukamwambie apande mti, anapanda mti kwa ajili ya nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake, sisi kwetu huko Kanda ya Ziwa ukimwambia mtu apande mti kwa ajili ya mvua, anakuona wewe ni mpuuzi. Maana tuna mafuriko miaka miwili. Atakuuliza: Je, unataka tupande miti ya kuzuia mvua? Maana yake ukiwaambia unataka miti ya mvua, wanakuuliza kuzidi hii iliyopo leo? Hii mvua iliyopo leo unataka izidi hapa? Ilitakiwa sisi tukawaambie panda miti ya kutengeneza fedha, ndiyo wananchi watapanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine mnasema labda tunawasakama wasomi, lakini jaribuni kufikiria maisha halali ya wananchi. Jiji la Dar es Salaam au Mji wangu wa Kahama, ukiuzuia mkaa kwa siku nne, unategemea nini? Maana yake yule mchoma mkaa hana ulazima wowote, ni mtu yuko porini, ataacha kuja kuchukua kibali. Sasa vipi hawa watu wa mjini, unataka gunia la mkaa lifike shilingi 300,000/=? Unao mkaa wewe wa ku-supply? Ni kitu ambacho lazima wenzetu wafikirie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Tanzania ni nchi ya nne kwa ku-export mkaa wa magendo na TFS hajawahi kutoa export permit ya mkaa, lakini kwenye data za World Bank inaonyesha ni ya nne. Sasa unakataaje kurasimisha ili upate hizo fedha na wale wanaonunua wa magendo waje wanunue pale kwenye soko? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri wenzetu wataalam lazima wafikirie sana. Haiwezekani baada ya miaka 60, kweli watoto wasome waende wakawe mgambo wa kukamata wazazi wao, ni sawa kweli! Haiwezekani! Kazi ya elimu duniani ni kutatua matatizo. Leo, Wazungu wametengeneza mpaka mapapai ya miezi sita. Wazungu wametengeneza kuku wa kizungu baada ya kuona kuna tatizo la kuku wa kienyeji na mayai yapo ya kizungu. Kwa nini hawa wataalam wasipande miti, wasilete miti ya miezi sita ili watu wakawa wanapanda miti wanauza kuni na mkaa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kurudi kwenye eneo la ugomvi, ugomvi, ugomvi, haiwezekani. Lazima twende kwenye pesa. Ina maana sasa hivi wao wanaenda kuanza fine, utawafunga watu milioni 60! Halafu mnataka hao watu tukawaombe kura. Unaweza? Unaweza ukaomba kura kwa watu uliowakatalia kula? (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Karibu.
T A A R I F A
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba kesi zote zinazohusisha misitu ni kesi za uhujumu uchumi. Sasa na mkaa utaingia huko: Je, nchi hii itakuwa na nusura? (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Kishimba, unapokea taarifa?
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono mitatu. (Makofi/Kicheko)
MWENYEKITI: Haya, endelea.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua na wewe ni graduate. Tunataka wasomi mtuletee mabadiliko. hatutaki wasomi kuwa Polisi, tunakuwa na majeshi mangapi? Tuna Jeshi la Polisi, tuna Jeshi la Wananchi, tutakuwa na majeshi kutwa nzima, haiwezekani. Tunataka mkaa ugeuzwe kama alivyofanya Mheshimiwa Dotto kwenye dhahabu. Sisi tumekaa gerezani miaka 20 kwa ajili ya dhahabu, lakini leo dhahabu si imekuwa halali? Ambayo ni sahihi. Kweli twende kuwaambia wazazi wetu kwamba tunakuja kukamatwa shauri ya miti. Sasa wanafanya nini? Haiwezekani tupeleke uhujumu wazazi wetu kwa ajili ya miti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana wenzetu wa maliasili, wajaribu kuangalia kabisa maisha ya watu. Tunapoongea, leo Jiji la Dar es Salaam ukiangalia matumizi ya mkaa ni makubwa mno. Kwa nini kusiwe na soko tu kesi hii ikaisha, wakachukua na ushuru wao pale pale; ili iwe ni kitu huru na kila mtu apende kupanda mti? Kupanda mti ni rahisi zaidi kuliko kulima mazao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri ajaribu kutoka kwenye Sheria za TFF. Maana yake TFF najua ndiyo yenye sheria ngumu sana, naye najua alikuwa kiongozi wa TFF. Ni kweli! Alikuwa TFF kwenye mpira, nafahamu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba sana wenzetu, kuna suala hili la mifugo. Kwa kuwa wewe mwenyewe ni Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Viwanda,
Mazingira na Biashara…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Ni kengele ya pili?
MBUNGE FULANI: Ya kwanza.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wewe ndio Mwenyekiti wa Kamati yetu, najua hiki tunachoambiwa kwamba ng’ombe kwenye mapori yale ambayo hayana Wanyama, kwamba ng’ombe wanaharibu mazingira; unaonaje tukiteuliwa Wabunge watano na wataalamu watano, tuchukue ng’ombe 100 tukakae mle porini siku nne tuchunge wale ng’ombe, tuone physically uharibifu unaosemwa? (Makofi/Kicheko)
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Karibu Mheshimiwa, Doctor.
T A A R I F A
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nimpe mzungumzaji taarifa kwamba kuna model za ufugaji wa mseto kati ya wanyamapori na mifugo ambayo imeshafanywa hapa Tanzania na hata Kenya. Tanzania kuna Ranchi inaitwa Manyara Ranch Mkoa wa Arusha, kuna mifugo maelfu pale na wanyamapori; ni njia ya wanyamapori na hatujaona madhara. Kule Kenya kuna Ranchi inaitwa Ol Pejeta ina hekta 95,000, kuna mifugo zaidi ya 5,000 na wanyama wa kila aina, hata faru weupe wapo. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Unapokea hiyo taarifa Mheshimiwa Kishimba?
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sina nia ya kupingana na elimu, lakini hao walimu wenu wanaowafundisha, waliwahi kuchukua ng’ombe 100 wakakaa porini ndiyo wakaandika huo uharibifu? Maana yake tunashinda tunazozana tu na wananchi mpaka wananchi wanaona kama hata na nyie Wabunge ni wapuuuzi tu. Hivi kweli, ng’ombe anafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna wanyama mle porini. Sawa, wananchi wako tayari kulipa, lakini watu wa maliasili wanachukua hela, wanaweka ng’ombe. Kwa nini tusiende nao tukaka humo siku tano tuone physically kwamba hasa huwa kinaharibika nini? Maana tukikalia tu makaratasi na kusomewa risala, uharibifu wa mazingira; itakuja kuwa mpaka lini? Wenzetu wanatengeneza pesa, hatuwezi kukaa na mawazo ya makaratasi kwa sababu tu mtu mmoja amesema, yeye amesoma; uharibifu wa mazingira alisomea London. Sasa wewe, tunataka kama ulisome London, utuletee mawazo ya kupata pesa, hatutaki mawazo ya London kuja kutukwamisha sisi, hapana. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine huwa sipendi lugha ya Musukuma, lakini kuna wakati kwenye hili, inabidi niungane na Mheshimiwa Musukuma. Kweli inauma sana. Anakuja kijana kasoma, anasema hamruhusiwi kupikia mkaa, hamruhusiwi kuni, ni uharibifu wa mazingira. Kuni sisi tunachukua matawi. Leo ukitembea na gari usiku au mchana, wazee wamebeba matawi, hakuna mtu anakata gogo la mti. Sasa unawakatazaje? Hao unaowakataza, ndio walikusomesha wewe na ndiyo wanaolipa kodi. Hiyo degree yako unaongea kiingereza, si ndio hao wanaotoa hela? Sasa unawakatazaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulitegemea wewe umesoma, uje ulete mawazo kama Wazungu wanavyofanya. Mimi nimetoka Ulaya, nimekuja na miti ya kisasa, inaota miezi mitatu, unakata mkaa, unauza kwa pesa. Tunataka hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nashukuru sana, lakini namwomba sana Mheshimiwa Waziri…
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)