Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Busega
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nami nikupongeze kwa kuwa Mwenyekiti. Nakutakia mema sana katika kazi hiyo. Pia nichukue fursa hii adimu sana kumpongeza Waziri, mtani wangu kwa kazi kubwa sana anayoifanya kwa jamii yetu hii ya Tanzania. Kipekee nampongeza Naibu Waziri kwa kazi
kubwa pia anayofanya na kweli ameonesha hekima kubwa sana hata leo asubuhi, ameonesha upendo wa dhati sana kwenye Wizara yake na hiyo ndiyo tumeona faida kubwa sana ya kuzaliwa usukumani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichangie mambo machache sana kwenye Wizara hii leo. Naishauri sasa Wizara, leo asubuhi hapa Mheshimiwa Mrisho Gambo amesema asilimia 80 ya mapato ya Wizara ya Utalii yanapatikana kule Kanda ya Kaskazini. Hata hivyo, tunaamini kabisa kwamba Kanda ya Ziwa pia tunaweza kuwa na mapato makubwa ya utalii mkitufanyia mambo ya msingi sana ikiwemo na kufungua geti la Ndabaka lililoko pale Lamadi na pia mtufungulie geti la pale Kijereshi. Mageti haya mawili yatakuwa mageti ya msingi sana kwenye pato la Taifa; vile vile yatakuza uchumi wa Kanda yetu ya Ziwa, yatakuza uchumi wa pale Jimbo langu la Busega, hasa pale Lamadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna hoteli nzuri sana Speke Bay, tuna hoteli nzuri pale Serenity na pia tuna hoteli nzuri pale Ndabaka, zina uwezo kabisa wa kutunza watalii. Naomba mtufungulie yale mageti ili yaweze kupokea watalii mbalimbali. Watalii siyo lazima waende KIA, wanaweza kushukia pale Mwanza Airport na baadaye wakaenda Lamadi kwa ajili ya kufanya tour pale Serengeti.
Kwa hiyo, nawaomba sana, mkitufungulia haya mageti mawili yatafanya kazi kubwa sana ya kukaribisha wale watalii na hasa mkiyatangaza. Myatangaze ili watalii wetu sasa waweze kupitia pale kwenye geti la Ndabaga lililopo pale Lamadi na geti la Kijereshi lililoko kule Kata ya Mkura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nataka nichangie ni uvamizi wa tembo kwenye makazi ya watu. Pale kwangu kuna Kijiji kinaitwa Kijereshi, kuna Kijiji kinaitwa Lukungu, kuna Kijiji kinaitwa Mwakiroba vijiji hivi vitatu vinaathirika sehemu kubwa sana na uvamizi wa tembo. Naomba sasa mchukulie hatua za dharula ili wananchi wetu sasa waweze kutokutishwa na hawa tembo. Mwaka 2020 tulikuwa na vifo zaidi ya vinne vilivyotokana na uvamizi wa Tembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, leo nakuomba sana Mheshimiwa Waziri, wewe ni msikivu, naomba sana kwa mara nyingine tuweze kuangalia namna ya kuleta askari wa kutosha tuweze kutengeneza Stesheni pale Kijereshi ili maaskari waweze kukaa pale. Ikibidi linapotokea tatizo, basi wapatikane kwa urahisi kwa sababu sasa hivi wanakaa Lamadi na Kijereshi ni mbali kidogo, tembo wanapoingia kule Kijereshi, wao mpaka waje wafike ni zaidi ya nusu saa muda mwingine, mpaka saa nzima au saa 1.30 ndiyo wanafika. Tembo tayari watakuwa wameharibu mazao, tayari watakuwa wamewadhuru wananchi.
Kwa hiyo, naomba sana, mtengeneze Stesheni pale Kijereshi kwa sababu ndiyo sehemu kubwa ya hifadhi. Pia muwape gari pale. Kuna shida ya gari kwa ajili ya usafiri wa kukabili hawa tembo. Kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atusaidie hili ili tuweze kupata gari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nililotaka kuzungumzia ni tatizo la TFS. Mheshimiwa Waziri, TFS ni pasua kichwa kwa baadhi ya watumishi; kuna baadhi ya watumishi sio waadilifu. Ukienda pale Magu, kuna TFS ambao wanalinda Hifadhi ya pori la Sayaka. Pale ni pasua kichwa. Wanakamata wafugaji, ni sawa inawezekana wanasimamia sheria, lakini faini ni kubwa sana. Ni shilingi milioni sita, shilingi milioni nne au shilingi milioni nane. Ni tatizo kubwa. Naomba sana tuliangalie hili, mfugaji akiambiwa kulipa shilingi milioni sita leo, haiwezekani. Mfugaji akiambiwa kulipa shilingi milioni nne leo haiwezekani; yaani how much is milioni nne? Yaani ni fedha nyingi kweli kwa mfugaji mdogo. (Makofi)
Mheshimwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hawa watumishi kidogo wanapokuwa wanalingalia hili, wawahurumie na wafugaji wetu, wawahurumie na wakulima wetu kwa sababu wanaumizwa sana na faini ambazo wanapigwa. Mheshimiwa Waziri, nimeshazungumza, nawe umeshakubali kuja pale, uje ujionee namna wananchi walivyo na malalamiko juu ya hifadhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakuomba sana, wananchi wale walikuwa na shida ya eneo la mita 840. Naomba sana utakapofika pale uzungumze na wananchi, usikie kilio chao na kama utaona inafaa Mheshimiwa Waziri, basi muweze kuwarejeshea eneo hili ili watu wa Nyaruande pale Kata ya Nyaruande katika Jimbo langu la Busega na sehemu ya Jimbo la Magu waweze kunufaika pale Sayaka kwa sababu sasa hivi wanapata shida katika namna ya kupata sehemu za kuchungia ng’ombe, lakini pia sehemu kubwa ya kulima. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri; wewe kule ni kwenu, wewe pale ndiyo umezaliwa, hili tatizo unalifahamu, njooni mlitatue ili wananchi wetu sasa waweze kunufaika na hii sehemu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nskushukuru sana, niseme nawapongeza, nawakaribisha Busega mje mtatue huu mgogoro. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)