Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Muhambwe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii. Nami niungane na wenzangu kuwapongeza viongozi wote wa Maliasili kwa kazi nzuri wanayofanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye hoja ya msingi. Jimboni kwangu tunao wafugaji wa nyuki. Tunao wafugaji wa nyuki takriban 2,400 ambao wameundwa na Kata mbalimbali ikiwemo Bitale, Murungu, Kitahana, Lusohoko, Kimodo Mjini pamoja na Misezero. Wafugaji hawa wanaweka mizinga yao katika msitu wa Myowosi. Tunaishukuru Serikali ilitenga shilingi milioni 507 kwa ajili ya kujenga kiwanda cha kuchakata mazao ya nyuki. Tumekwisha kupokea shilingi milioni 300 ambazo zimejenga jengo. Tunasubiri shilingi milioni 207 ambazo zinakwenda kununua vifaa kwa ajili ya kuchakata mazao ya nyuki. Tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri hayo, bado tuna changamoto. Changamoto ya kwanza ni tozo. Wafugaji hawa wa nyuki walikuwa wakitozwa shilingi 5,000/= kwa mwezi kwa kwenda kurina asali au kuweka mizinga. Ni wiki tu iliyopita wametangaziwa kwa kupewa tahadhari kwamba ifikapo mwezi wa Saba mwaka mpya wa fedha watakwenda kutoa shilingi 15,000/= kwa mwezi kwa ajili ya kuingia msituni. Ni kubwa sana kwa mwananchi wa kawaida tena mfugaji wa nyuki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile wameongezewa kodi ya baiskeli, shilingi 200/= kwa siku; hiyo inaleta shilingi 6,000/= kwa mwezi. Kwa hiyo, kwa mwezi mmoja huyu mrina asali atatoa shilingi 21,000/= ili aweze kufanya kazi zake kule msituni. Tunaiomba Wizara iangalie upya kabla haijaanza kutumika. Hii ni gharama kubwa sana kwa mfugaji wa nyuki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, cha pili, mfugaji yule wa nyuki haruhusiwi kuingia na pikipiki. Angalia mfugaji wa nyuki mwenye ndoo 200 za asali, asombe kwa pikipiki na ana kibali cha mwezi mmoja, haitekelezeki. Tunaomba Wizara iangalie vizuri upya kuona jinsi gani huyu mfugaji ataweza kuyachukua haya mazao yake ya nyuki; asali kuweza kutoa kule msituni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya tatu ni eneo la kuweka ile mizinga. Wafugaji wale wameweka mizinga kilometa tano mpaka kumi. Mwanzo walikuwa wakienda mpaka kilometa 25, imekuja sheria warudi nyuma zaidi. Ombi lao, wafugaji wa nyuki wamenituma, wanaomba waendelee kuachwa pale pale kilometa 20 mpaka 25 kwa sababu hawataki wale nyuki wale haya mazao ambayo yanawekwa kemikali. Maana Jimbo langu la Muhambwe linaongoza kwa asali nzuri organic, hivyo nyuki wale wakila hizi kemikali asali ile itakuwa haifai. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwa wakulima ambao wanalima karibu na hiyo hifadhi ya Myowosi. Wameshalima, wameshapalilia, umefika muda wa kuvuna, hawaruhusiwi kwenda kuvuna. Naomba hekima itumike, wakulima waweze kwenda kuvuna mazao yao, baadaye sheria itafuata mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo Kata ya Mrungu katika Kijiji cha Kumbanga. Hiki Kijiji kimeanza mwaka 1974 kikiwa na wakazi 800. Tukiwa tunafahamu kabisa growth rate ya 2.7 tunaweza tuka-imagine hiki Kijiji sasa hivi kina watu wangapi? Kijiji hiki kipo mpakani kabisa mwa Pori la Myowosi na mpaka uko chini ya kilometa moja. Wananchi hawa wamenituma, wanaomba wasogezewe mpaka kwa sababu ni dhahiri wameshaongezeka. Kama idadi ya watu imeongezeka, basi na shughuli za kijamii zimeongezeka ikiwemo kilimo, ufugaji na ziada. Naomba Mheshimiwa Waziri ikikupendeza twende wote Murungu, pale Kumbaga…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja.
(Makofi)