Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Muharami Shabani Mkenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bagamoyo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kutoa mchango wangu katika Wizara hii. Kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu, kwa kazi nzuri wanayoifanya, japo Wizara ina changamoto nyingi sana. Nami naomba tu niwaambie, wanayozungumza Wabunge hapa, hebu yachukueni kwa makini mkayafanyie kazi, msiyaache yakapita ikawa business as usual.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda zaidi kuzungumzia suala la utalii wa ndani. Utalii wa ndani naona umesuasua sana katika Taifa letu. Kila siku Wizara inapiga kelele, inahamasisha, inapiga debe kuhusu utalii wa ndani, lakini bado utalii wa ndani haujawa sawasawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe ushauri. Sasa hivi duniani biashara huwa inamfuata mteja na siyo mteja anayeifuata biashara. Naomba niishauri Wizara, sasa hivi wabadilishe mfumo wa utalii wao wa ndani. Sasa hivi hakuna Watanzania walio wengi wenye uwezo wa kutembelea Ngorongoro, Manyara na Mikumi; na wana hamu ya kuona wanyama katika hizo mbuga na kutembelea mbuga hizo, lakini uwezo wao ni mdogo. Nawashauri kitu kimoja. Kama mnavyofanya Saba Saba katika maonesho, Banda la Maliasili linatembelewa na watu wengi sana kuliko mabanda yote katika maonesho ya Saba Saba. Hii ni kwa sababu gani? Watu wengi wanapenda kuona wanyama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jaribuni sasa hivi kuweka utalii wa mobile. Mtafute viwanja katika miji kama Dar es Salaam na Dodoma, muweke mabanda ambayo wananchi watakwenda kutembelea wanyama na kulipia pesa. Mtaingiza pesa nyingi za kutosha. Mikoa mingi sana haina mbuga za wanyama na hawawajui wanyama hawa wakoje, kwa hiyo, watu wengi sana wanapenda kuona simba, chui na wanyama mbalimbali, lakini wanakosa fursa za kwenda kuwaona. Sasa ifikie wakati mtengeneze hicho kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, pale Dar es Salaam, Coco Beach au pale kwangu Bagamoyo, kuna beach nzuri na maeneo mazuri. Mkiweka zoo pale ya Wanyama, watu waje kutembelea, watu wengi kutoka Zanzibar; Zanzibar inapokea watalii wengi sana, lakini wanaishia kule, hawana pa kwenda. Wakitoka Zanzibar wanaondoka zao kwenda Kenya. Hebu tuwape fursa watalii wengi wanaokwenda Zanzibar waje Bagamoyo. Nawashauri kitu kimoja, mjenge gati pale, mjenge gati ya kupaki speed boat ambapo mtalii anaweza akatoka Zanzibar akaja mpaka Bagamoyo, akatembelea Mbuga ya Wanyama ya Saadani, akatembelea vivutio vilivyo Bagamoyo na halafu akapanda boti akarudi Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana kuamsha uchumi wa utalii, lakini tukitegemea utalii wetu tuone watu wakitembelea mbuga za wanyama, hiyo itachukua muda mrefu sana na hamtatengeneza pesa. Kwa sababu, watu wengi sasa hivi wanapenda kuona Wanyama; vijana wa shule za msingi, vijana wa sekondari, vijana wa vyuo, wote wanapenda kitu hiki. Kwa hiyo, nawaomba sana, mbadilishe mfumo wa utalii wa ndani, mtengeneze zoo katika miji yetu…

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. MUHARAMI S. MKENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuunga mkono hoja.