Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Donge
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, nami nimshukuru Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala kwa kutujaalia afya njema, hali kadhalika nikushukuru na wewe kwa jinsi unavyoliendesha Bunge hili na hata sisi wa form one tumekuwa tunajisikia vizuri wakati tukitoa michango yetu hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwapongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri pamoja na Naibu Waziri Mheshimiwa Masauni hali kadhalika ningependa vilevile kuwapongeza Watendaji wa Wizara hii ya Fedha wakiongozwa na Mtendaji Mkuu Katibu Mkuu Ndugu Emmanuel Tutuba Rafiki yangu ambaye kwa kipindi fulani tulikuwa tuko pamoja kule Ufaransa tukishughulikia masuala mazima ya mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba wakati nikiwapongeza kwa jitihada kubwa alizokuwa akizifanya lakini pia ningeomba nitoe mchango wangu katika maeneo mawili makubwa, kwanza ni kuhusu masuala mazima ya fedha za maendeleo au miradi ya maendeleo hususan katika fedha za maendeleo kwa kupitia wadau wa maendeleo au wahisani.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli kuna tatizo changamoto kubwa ambayo imekuwa ikiikabili hii miradi ya maendeleo na zaidi ni ucheleweshaji wa fedha kupitia Wizara ya Fedha. Kama tunavyojua kwamba tumefanya mabadiliko kidogo hivi sasa tunazitaka taasisi au sekta mbalimbali kwenye utararibu mzima wa fedha za wahisani zipitie Wizara ya Fedha kwa ajili ya kuratibiwa na ndipo ziende katika sekta husika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Lakini kwa kweli kumekuwa na tatizo kubwa la ucheleweshaji na ambalo limekuwa liki-disappoint au likikatisha tamaa wahisani na pia watekelezaji wa miradi. Kwa mfano, kuna mradi wa equal PRC ambao ulikuwa ukitekelezwa na wenzetu wa Chuo cha Misitu Olmotony, mradi ule kwa bahati nzuri mimi nilikuwa ni miongoni mwa Board Member badala ya kutekelezwa mradi ule kwa miaka mitatu mradi ule ulitekelezwa kwa miaka minne na nusu na sababu kubwa ilikuwa ni ucheleweshaji wa fedha kupitia Wizara ya Fedha, kwa hiyo ningeliomba sana Mheshimiwa Waziri eneo hili akalifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivi sasa kuna mradi ambao wenzetu wa NEMC na niwapongeze kwa hili, wenzetu wa NEMC wameomba miradi miwili, mradi mmoja wa Tanzania Bara ambao utatekelezwa kule Bunda na mradi mwingine ambao utatekelezwa Zanzibar unaitwa mradi wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jina la Climate Change Resilience for Coastal Community for Zanzibar. Sasa mradi huu una jumla ya dola milioni moja na mkataba wake umesainiwa tarehe 2/7/2020 na hapana mkataba wake umepitishwa rasmi na Bodi ya Adaptation Fund tarehe 2/7/ 2020 halafu mkataba rasmi umesainiwa taehe 7/11/2020 na fedha zimeingizwa katika akaunti ya NEMC ambayo iko BOT mwezi 11 mwaka 2020. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, huu ni mwezi wa Tisa fedha ambazo zimeingizwa kwa ajili ya utekelezaji wa mwaka wa kwanza wa mradi bado fedha hazijakuwa released kwenda kwenye sekta husika na kwa ajili ya matumizi au ya utekelezaji. Delay hii itatugharimu baadaye tuje tuombe no cost extension kwa ajili ya utekelezaji wa mradi kwa uzembe wetu sisi wenyewe.
Mheshimiwa Spika, Katibu Mkuu unakumbuka wakati tuko Ufaransa mwaka 2015 nchi masikini zilivyokuwa zikihangaika kutetea mfuko wa Adaptation Fund na unakumbuka vilvile nchi masikini zimekuwa zikihangaika kuweza kuomba fungu la Adaptation Fund liongezwe ili ziweze kusaidia kukabiliana na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi. Sasa kama leo fedha zinaingia mwezi wa Tisa hivi sasa bado hazijakuwa released kwa ajili ya kwenda kutekeleza miradi nafikiri hapa itakuwa hatujifanyii sisi haki na vilevile hatufanyi haki hawa wenzetu wa NEMC ambao wamehangaika kuweza kuzitafuta hizi fedha na zimeshafika nchini fedha, tuna delay kuzitoa kwa ajili ya utekelezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapa ningeliomba vilevile kupeleka mchango wangu kwenye suala zima la Kamati ya Madeni. Kuna Kamati ya madeni ambayo iko Wizara ya Fedha ndiyo inayoratibu na inajumuisha wadau mbalimbali, lakini kuna shida kubwa napo hapa kwa sababu imekuwa miradi mingi au bajeti nyingi ambazo zinapelekwa Wizara ya Fedha za kupitia wahisani wa maendeleo hawa, unaambiwa kwamba mradi hauanzi kwa sababu Kamati ya madeni haijakaa sijui utaratibu wa hii kamati ya madeni ukoje kwasababu hata ile miradi ambayo ni grant siyo madeni lakini pia unaambiwa tusubiri Kamati ya Madeni ikae.
Mheshimiwa Spika, nakumbuka mwaka 2014 binafsi nilikuja Wizara ya Fedha mara saba kufuatilia mradi wa ADB (African Development Bank) mabadiliko ya tabianchi na kila nikija kuuliza naambiwa Kamati ya Madeni haijakaa, huu mradi ulikuwa una dola laki 360 tu ni fedha ndogo mno, kiasi kwamba mpaka unaambiwa kwamba mpaka Kamati ya Madeni ikae na inaweza ikawa miezi mitatu miezi sita haijakaa. Kwa hiyo, ningeomba tu hii kamati ya madeni nayo vilevile tupate utaratibu ukoje, hizi fedha za ruzuku kwa nini tusiziondoe kwenye Kamati ya Madeni tukazitafutia utaratibu mwingine wa kuweza kuzipitisha badala ya kutumia Kamati ya Madeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia naiomba Wizara ya Fedha kwa sababu fedha kama hizi laki 350 hivi mpaka zije zipate signature ya Waziri wa Fedha Tanzania Bara? Hatuwezi tukaweza tuka-apportion haya madaraka kwa Waziri wa Fedha Zanzibar fedha kama hizi ndogo akasaini yeye yakaisha? Kwa sababu signature ya Waziri wa Fedha ilituchukua karibu miezi sita! signature tu ya Waziri wa Fedha unakuja Tanzania Bara na kurudi bado signature hujaipata sasa kwa nini tusiangalie uwezekano wa hizi fedha za ruzuku na hasa kama asilimia ndogo kama hii laki 350 tusiangalie uwezekano Waziri wa Fedha Znzibar akasaini badala ya kutumia Waziri wa Fedha wa Tanzania Bara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningeliomba vilevile kuendelea na suala moja la accreditation. Niliwahi kuchangia hapa katika Bunge lako Tukufu kuhusu suala zima kwamba Wizara ya Fedha walikuja na suala la registration karibu miaka 10 iliyopita, mpaka leo hii Tanzania ukiondoa CRDB ambao wamejitahidi kwa upande wao lakini hakuna taasisi ya Serikali ambayo imeweza kupata accreditation kwa ajili ya mfuko wa mabadiliko ya tabianchi wa dunia (Green Climate Change Fund). Kwa hiyo, ningeliomba Waziri wa Fedha atakapokuja hapa aje atuambie wapi Wizara ya Fedha wamekwamba, kwa sababu wenzetu Ethiopia Wizara ya Fedha sasa hivi imekuwa accredited na inaweza kuomba fedha moja kwa moja kwenye huu mfuko wa GCF.
Mheshimiwa Spika, hali kadhalika Rwanda Wizara ya Kilimo wao wameomba wamekuwa accredited na wanaweza kuomba fedha moja kwa moja Mfuko wa GCF. Tanzania tumekwama wapi? Suala hili zaidi ni suala la uzalendo, kwa sababu bila kujituma, bila watu kuwa dedicated, kuwa committed, nchi ikawauma, wakaweza kuomba kusimamia vitu kama hivi siyo rahisi, wenzetu wa Wizara ya Fedha mnakwama wapi uzalendo uko wapi mpaka leo mmeshindwa wakati wenzetu nchi nyingine wamefanya hili? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye suala zima la ucheleweshaji wa miradi hasa mradi huu wa Zanzibar na Bunda ningeliomba kama sikupata majibu ya kuridhisha nitazuia kifungu hapa, kwa hiyo ningeliomba kabisa nitazuia mshahara wako Mheshimiwa Waziri kama sikupata majibu ya kuridhisha katika suala zima la ucheleweshaji wa fedha za mradi hasa wa mabadiliko ya tabianchi kwa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)