Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kidogo katika bajeti hii ya Wizara ya Fedha. Leo ninayo machache, kwanza ningependa kuongea kuhusu bajeti ya CAG, CAG ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Fedha za Serikali, lakini sio hilo tu Mkaguzi Mkuu huyu CAG anaangalia mwenendo mzima wa nchi kiuchumi, lakini pia ni jicho la Bunge, kwamba sisi Bunge tunafanya kazi na CAG. Kwa hiyo kama wananchi ambao tupo katika chombo hiki, CAG anatusaidia kujua mwenendo mzima wa mapato, matumizi, manunuzi ya nchi, miradi inaendaje na utendaji wa mambo yote yanayohusu fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda niseme kuhusu bajeti yake, CAG anapaswa kupata bajeti ya kutosha kwa sababu anakagua Halmashauri zote za nchi hii, anakagua Idara zote za Serikali, anakagua Mashirika yote ya Umma. Ili aweze kufanya ukaguzi huu vizuri ni lazima awe na wataalam na ni lazima awe na fedha ya kutosha. Ukiangalia CAG anajitahidi kukagua Halmashauri, lakini kuna baadhi ya Mashirika ya Umma ameshindwa kukagua kwa sababu hakuna fedha ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha uliopita CAG alipewa bilioni 80.5, kipindi hiki amepewa bilioni 81 ni kama ameongezewa Milioni 840 tu, kwa hiyo ni kama kitu ambacho kwa kweli hakimsaidii zaidi. Kwa upande wangu, naishauri Serikali kwamba CAG ili aweze kufanya kazi yake vizuri angekuwa anapata fedha kuanzia bilioni 150 mpaka Bilioni 200, hiyo ingeweza kumsaidia kukagua na kutupa picha ilivyo katika nchi yetu. Licha ya CAG kukagua taarifa za fedha, lakini pia ana kaguzi mbalimbali ambazo anazifanya, wakati mwingine kwa kuelekezwa na Serikali, kwa kuelekezwa na Bunge, zile ambazo zinaitwa special audit, ambazo zinahitaji fedha na ukaguzi wa kina. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, CAG ameanzisha ukaguzi ule wa ufanisi yaani performance report na ukaguzi wa kifanisi unahitaji wataalam mbalimbali, sio sawa na ukaguzi ule wa taarifa za fedha ambao unahitaji Wahasibu tu. Kwa mfano, anakagua mifumo, akikagua mifumo ya TEHAMA inavyokwenda nchini, anahitaji wataalam wa IT, anahitaji wataalam mbalimbali wa kumsaidia ambao wakati mwingine hawakuajiriwa katika ofisi yake. Kwa mfano akikagua mienendo ya mifumo ya utoaji mbolea hapa, mifumo ya kilimo na mambo mbalimbali, anahitaji wataalam ambao wengine ni Ma-engineer, wengine ni wataalam wa maji, ili aweze kusaidia Serikali kuona kwamba hii mifumo ambayo inatengenezwa na Serikali au imewekwa na Serikali inafanya kazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo naishauri Serikali kwamba CAG aongezewe fedha. Najua kwamba inawezekana kwamba Serikali haitaki kukaguliwa, najua kukaguliwa sio kitu kizuri, lakini ni lazima wakubali na wao Serikali kwamba hawawezi kujua kila kitu katika nchi. Ni lazima CAG asaidie, anasaidia wananchi kujua mwenendo mzima wa nchi yao, lakini pia anawasaidia Serikali, hii nchi ni kubwa, inahitaji mtu ambaye atakagua na kuonesha kwamba hapa mambo yanakwenda vizuri, hapa mambo hayaendi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo langu la pili ni kuhusu hii Wizara ya Fedha ambayo ndio inayoangalia uchumi wa nchi, ndio inayoangalia mapato ya nchi na Serikali iweze kwenda, ndio inaangalia matumizi na mambo mengine ambayo yapo katika Instrument ya Wizara yao. Sasa nataka niongelee chanzo kimoja ambacho Wizara hii imeonesha udhaifu mkubwa kutotuambia sisi Watanzania kwamba chanzo hiki kinaleta mapato gani na kikoje, ni chanzo cha Vitambulisho vya Wajasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilitegemea kwamba Wizara ya Fedha ingeweza kutuambia kwamba chanzo hiki kupitia Sheria ya Fedha kiko wapi, kipo kasma ipi. Kwa hiyo nategemea labda kipindi hiki watatueleza kwamba chanzo hiki kikoje, kipo kasma gani na kimezalisha fedha kiasi gani. Chanzo hiki kilianza katika misingi isiyoeleweka na kimeleta conflict, kimeleta kutoelewana kati ya Serikali Kuu pamoja na TAMISEMI, kwa sababu Halmashauri zilikuwa zinakusanya fedha kupitia vyanzo mbalimbali vya fedha hizi za wafanyabiashara wadogo wadogo, lakini Halmashauri zimejikuta mahali zimekwama. Kwa hiyo, tunataka kujua ni kipi sasa. Je, hiki chanzo kinaendelea, kipo au hakipo? Maana yake sasa hivi hatusikii chochote. Kwa hiyo inawezekana kikafa lakini bila halmashauri kujua kama wanaendelea kukusanya au Serikali inaendelea kukusanya…

T A A R I F A

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Ngoja Mheshimiwa. Taarifa nakukubalia Mheshimiwa Kakunda.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, ningependa kumpa taarifa msemaji anayeendelea, amenishtua kidogo alivyosema kwamba hakuna maelewano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Nataka nimhakikishie kwamba maelewano ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa hapa Tanzania yapo kila siku na yataendelea kuwepo, mawasiliano yapo kila siku na yataendea kuwepo. Ahsante sana, aendelee kuchangia.

SPIKA: Mheshimiwa Rwamlaza unapokea taarifa hiyo?

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana inawezekana nimeteleza labda nimetumia neno, lakini ninachotaka kulieleza Bunge hili ni kwamba, halmashauri zimekosa mapato kwa sababu ya chanzo hiki kuondolewa, ndio ilikuwa nia yangu. Kwa hiyo sikusema kama nisema hivyo I am sorry, lakini ninachosema ni kwamba kitendo cha halmashauri kunyang’anywa chanzo hiki kimewafanya halmashauri zishindwe kuwa na mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunachoomba ni kwamba sasa kutokana na Wizara ya Fedha kutosema na kutotuambia chanzo hiki kupitia sheria hii ya fedha kipindi hiki mtueleze kwamba chanzo hiki kinazalisha nini, kimetoa fedha kiasi gani na Halmashauri wanapata hasara kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine naomba niongelee Wakaguzi wa Ndani. Kamati ya Bajeti imependekeza kwamba Wakaguzi wa Ndani na wenyewe warudi kwa CAG, nakubaliana nalo japokuwa mzigo ni mkubwa kwa sababu gani, kwa sababu hawa Internal Auditors hawana uhuru wa kukagua na hasa katika halmashauri, kwa sababu mimi nafanya kazi na Halmashauri kama Mjumbe wa LAAC…

T A A R I F A

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, endelea mtoa taarifa.

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Spika, naomba nimpe taarifa msemaji kwamba katika taarifa yetu ya Kamati ya Bajeti hatukusema Wakaguzi Wakuu wa Ndani katika halmashauri zetu na Wizara warudi kwa CAG, ila waripoti kwa Mkaguzi Mkuu wa Serikali ambaye yupo Hazina.

SPIKA: Pokea taarifa hiyo Mheshimiwa.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee. Ninachopenda kusema ni kwamba hawa Wakaguzi wa Ndani kule wanakokagua hawana uhuru, ndani ya Halmashauri Wakaguzi wa Ndani wapo chini ya Mkurugenzi, anawanyima bajeti, anawanyima fedha, kwa hiyo unakuta na wakati mwingine wanashindwa hata kutoa taarifa sahihi kwa sababu hawa watu wanakaa na Mkurugenzi, hawawezi wakati mwingine ambaye ndiye bosi wao kuhakikisha kwamba wanasema ukweli kinachotendeka ndani ya halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho, nije kwenye hii monitoring and evaluation. Niseme kwa maneno machache kwa sababu hii ni mara yangu ya pili natoa mawazo yangu na haya nayachukua kama mawazo yangu. Baada ya kufanya kazi na Kamati hizi ambazo zinafanya kazi ya oversight, nimegundua kwamba wewe na kiti chako hiki nakumbuka umefanya kazi kubwa kuandaa na kutengeneza ile Kamati ya Bajeti, ilikuwa sio kazi nyepesi. Natoa ushauri kwamba ndani ya Bunge lako Tukufu uangalie namna ya kuwa kama sio Kamati ya Bajeti basi kuwe na Kamati inayofanya Monitoring and Evaluation. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu hata kama ni kwa Waziri Mkuu, hata kama ni kwa Waziri wa Fedha, huwezi wewe mwenyewe kujisimamia, yaani unaji-monitor, halafu unajitathmini, naona ni kitu ambacho hakiwezekani kwa kweli. Ndio maana wakati mwingine tunashindwa kupata taarifa ya namna bajeti tunayopitisha kama kweli inatekelezwa ipasavyo. Tungekuwa tunapata ripoti kila baada ya miezi mitatu ndani ya Bunge hapa, kwamba tumepitisha bajeti lakini kwa miezi mitatu tumepata fedha hizi, tumeenda hivi, mradi wetu umekwama, hiki kimekwama.

Mheshimiwa Spika, naomba hiki kitu kifanywe na watu wengine ambao ni tofauti na Wizara yenyewe. Kwa hiyo napenda kutoa ushauri wangu kwamba Bunge hili hata kama sio leo, hata kama sio kesho, lakini lifikirie namna ya kuanzisha Kamati ya Monitoring and Evaluation ambayo itafanya kazi nzuri kama hii ya bajeti inavyofanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo machache, nakushukuru sana. (Makofi)