Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie kidogo kwenye hoja hii, lakini naomba nianze kwenye kitabu chetu kitukufu, kinaitwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba nianze kwenye Kifungu cha 62(1) Sura ya 3 ya Katiba hii. Kuna chombo kimoja kinaitwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba ninukuu: (Makofi)

Kifungu cha 62(1) kinasema: “Kutakuwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano, ambalo litakuwa na sehemu mbili; yaani Rais na Wabunge.” Naomba niendelee kwenye Kifungu 63 (1): “Rais kama sehemu moja ya Bunge atatekeleza madaraka yote aliyokabidhiwa na Katiba hii kwa ajili hiyo,” lakini 63 (2) inasema: “sehemu ya pili ya Bunge itakuwa ndicho chombo kikuu cha Jamhuri ya Muungano ambacho kitakuwa na madaraka kwa niaba ya wananchi kuisimamia na kuishauri Serikali ya Jamhuri ya Muungano na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa Katiba hii.” Hili ndiyo Bunge la Jamhuri ya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niendelee 63 (3) (d) kinasema hivi: “Kwa madhununi ya utekelezaji wa madaraka ya Bunge, laweza (b) kujadili utekelezaji wa kila Wizara wakati wa Mkutano wa Bunge wa kila mwaka wa Bajeti.”

Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie. Nimekuwa nikifuatilia bajeti zetu za miaka mingi, Bunge linakaa kama chombo chenye mamlaka iliyopewa na wananchi, lengo ni kuziandalia Wizara hizi na kuzipitishia bajeti zake kwa mujibu wa zilivyoomba. Marekebisho yanafanyika, lakini hatimaye Bunge linapeleka fedha kwenye Wizara husika. Matokeo yake ni nini? Matokeo yake ni kwamba mara nyingi tunarudi kwenye kuangalia Bunge au Serikali imetekelezaje bajeti kwa mwaka uliopita? Pia kuangalia kwa mwaka ujao.

Mheshimiwa Spika, mara nyingi kwa masikitiko makubwa tunashindwa au Wabunge tunalalamika kwamba Serikali kupitia Wizara ya Fedha haipeleki fedha zinazotakiwa kama tulivyopitisha. Sasa maana yake ni nini? Maana yake ni kwamba Bunge kama Bunge linafanya kazi yake ya kupitisha lakini Bunge linashindwa kusimamia bajeti iliyoipitisha ili kuhakikisha kwamba kila Wizara inafanya kazi kwa mujibu wa maelekezo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ombi langu, ukiangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Wizara ya Fedha ina majukumu 10 imejipangia pale. Moja katika hayo ni kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza bajeti kama ilivyoahidiwa au ilivyopitishwa na Bunge. Bahati mbaya sana kwamba kwa asilimia kubwa Wizara nyingi tunakuja kuzilaumu hapa kwamba hazikutekeleza; wenye maji wanalalamika, wenye barabara wanalalamika, wenye kilimo wanalalamika, uvuvi wanalalamika, kila Wizara kwa asilimia kubwa tunakuja kulalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ushauri wangu kwa Bunge lako, Bunge lichukue nafasi yake ya kupitisha lakini kusimamia ili miaka ijayo au mwaka mwingine wa fedha tusije kumlaumu mtu, kwa sababu kazi yetu kubwa hapa tumeambiwa sisi kama Bunge ni kuisimamia Serikali na kuishauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama hoja ni hiyo, ombi langu na ushauri wangu kwa mujibu wa kifungu hiki cha 63 (2) naomba basi kushauri kwamba Bunge hili sasa likubali kutunga au kuandaa Kamati ambayo itafanya kazi ili Wizara ya Fedha pamoja na mambo mengine, kazi zake kubwa ziwe mbili: kwanza, kutengeneza sera na ya pili iwe ni kukusanya, period. Hii ni ili Bunge hili lije lifanye kazi ya kusimamia fedha zilizokusanywa na kuzipeleka kunakohusika ili tuje tujiulize wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nilishauri Bunge lako lifanye kazi ya kuunda Kamati ambayo ndiyo itafanya kazi ya uhakika kuhakikisha kwamba kile ambacho tumekipitisha kama Bunge, basi kinapelekwa kwenye Wizara zote na taasisi zote ili baadaye tuje tujitathmini wenyewe na wala siyo Serikali kuja kutuambia hiki sikupeleka. Maana yake kwa taratibu hizi tumewaachia Wizara ya Fedha mamlaka ya kujiamulia nani wampe? wampe nini? Kwa wakati gani? Kwa kiasi gani? Hii siyo kazi ya Wizara ya Fedha, ni kazi ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa maneno haya mafupi, naomba kuchangia hoja. Ahsante sana. (Makofi)