Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nishukuru kwa kupata nafasi ya kuweza kutoa maoni yangu katika bajeti hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nataka nianze kwa kumpongeza sana Waziri wa Fedha kwa bajeti yake hii ambayo ameiwakilisha, bajeti ambayo kimsingi ni ya kimkakati na imejikita kweli kweli kwenye kutatua changamoto za Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana mama yetu mpendwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa bajeti hii nzuri, ambayo moja kwa moja inaonyesha nini ambacho amekusudia kuwatendea Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, itoshe kusema kwamba, hii ni bajeti ya wananchi; na ziko sababu nyingi sana ambazo zinaonesha na kuthibitisha kwamba bajeti hii ni bajeti ya wananchi wa Tanzania. Ikizingatiwa kwamba, ndiyo bajeti yake ya kwanza tangu alipoingia madarakani, lakini ndani ya muda mfupi huo amefanikiwa kwa asilimia 100 kuonesha nini ambacho amepanga kwa ajili ya kuwasaidia Watanzania. Vilevile ameonesha vipaumbele vyake vizito alivyonavyo katika kufikia maono hayo. Ni wazi kwamba Rais wetu Samia Suluhu Hassan, amebeba maono makubwa sana kwa Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kana kwamba haitoshi, ukifuatilia hii bajeti imegusa makundi mbalimbali katika jamii yetu. Sisi sote ni mashahidi, tumekuwa tukizungumza humu Bungeni changamoto kubwa ya watumishi. Kilio kikubwa cha watumishi ilikuwa ni kupandishwa madaraja. Kupitia kwenye bajeti hii, mama yetu ameweza kutenga zaidi ya bilioni 449, kwa ajili ya kupandisha madaraja watumishi. Jambo hilo lina tija kubwa sana. Kwa sababu, kwanza litasaidia sana kuweza kuongeza motisha kwa watumishi wetu wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi, tunafahamu, ilikuwepo tozo ya asilimia sita ya ongezeko la thamani. Tozo ile ilikuwa inasababisha deni lilikuwa haliishi; unalipa lakini bado deni linaendelea kuongezeka. Watumishi wamefurahi sana kwa kuondokewa kwa tozo hiyo, kwa sababu sasa ni wazi moja kwa moja, itasaidia kuweza kukuza uchumi wa watumishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu changamoto ambazo zipo kwenye barabara zetu, na barabara nyingi ambazo zinachangamoto kubwa ni zile barabara za vijijini. Lakini kupitia bajeti hii fedha zimetengwa za Kimarekani milioni 300 kwa ajili ya kwenda kusaidia barabara za vijijini, na hizo fedha zinatoka kwenye mkopo wa Benki ya Dunia. Vilevile, dola za kimarekani milioni 50, kwa ajili ya kwenda kuhudumia barabara zetu za vijijini (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kilichonifurahisha zaidi ni kwa sababu huu mkopo moja kwa moja utapelekwa kwenye yale maeneo ambayo yana tija kubwa ya uzalishaji, na hicho ndicho kilichokuwa kilio cha Bunge hili, kwamba sehemu nyingi ambazo zinatumika kwa ajili ya uzalishaji barabara zake zilikuwa zina changamoto kubwa sana. Mimi kama Mbunge wa wanawake wa Mkoa wa Songwe nimefurahi sana kwa sababu sote tunafahamu wazalishaji wakubwa ni wanawake. Kwa hiyo moja kwa moja fedha hizi zitasaidia sana kuweza kukuza uchumi wa wananchi, hususani uchumi wa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ipo tozo ambayo imewekwa kutoka kwenye mafuta. Mimi nasema Bunge lililopita Waheshimiwa Wabunge wote humu Bungeni tulikuwa tukisimama tunaiomba Serikali. Kwamba Serikali tunaomba iongeze tozo kwenye mafuta ili kwenda kushughulikia changamoto zetu. Na leo tumeshuhudia Serikali imesikia kilio hicho na tozo hiyo imeongezeka, kwa lengo ambalo ni jema la kwenda kukarabati barabara zetu za kule vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi wanawake tunajua namna ambavyo tulikuwa tunapata shida sana inapokuja suala la hizi barabara. Wanawake wengi walikuwa wanajifungulia barabarani, wanajifungulia njiani kutokana na ubovu wa hizi barabara. Sisi wanawake tunamshukuru sana Rais wetu kwa sababu sasa suala la wanawake kujifungulia barabarani linafikia kikomo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi ambayo nikianza kuyaeleza ni mambo mazuri ambayo yapo kwenye bajeti yetu. Lakini ni wazi kwamba, ili mambo hayo yote yaweze kutekelezwa itakuwa si sawa kwamba mzigo huu wote ukaachiwa Serikali. Ni lazima wananchi tuweze kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba haya mambo mazur, ambayo Rais wetu ameyakusudia kwa Watanzania yanapatiwa ufumbuzi. Na namna pekee ya kuwashirikisha wananchi ni kupitia kodi. Mwalimu Nyerere alisema wakati wa Azimio la Arusha; naomba ninukuu kwamba:-
“kila mtu anataka mendeleo, lakini si kila mtu anaelewa na kukubali mahitaji ya msingi, kwa ajili ya maendeleo”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya msingi kwa ajili ya maendeleo ni pamoja na kuwa na Serikali nzuri, kufanya kazi kwa bidii, wananchi kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo yao pamoja na Serikali kusimama kidete katika ukusanyaji wa kodi. Ni wazi kwamba Serikali isiyokusanya kodi ni Serikali ambayo ni mfu. Ni Serikali ambayo ni mfu kwa sababu daima haiwezi kuwapelekea maendeleo wananchi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia kwenye bajeti hii, kwamba Serikali imeleta kodi aina mbalimbali. Sasa mimi nataka nizungumzie kodi ya Property Tax kwa sababu, ni kodi ambayo ilikuwepo miaka mingi, si kitu ambacho ni kipya. Hata hivyo changamoto yake ilikuwa ni kwamba, kodi hiyo wananchi tulikuwa hatulipi nikiwemo mimi mwenyewe Juliana Shonza, sijawahi kulipa kodi ya majengo. Hii ni kutokana na usumbufu ambao mtu ukifikiria, utoke, uende ukapange foleni TRA, ilikuwa ni usumbufu mkubwa sana. Sasa Serikali imekuja na ubunifu wa kukusanya kodi, na imetumia akili kwamba sasa kodi hii itakusanywa kwa akili kuliko kutumia nguvu na mabavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie changamoto chache ambazo zipo kwenye hii kodi. Niishauri Serikali, kwamba tunatambua wazo ni jema na ubunifu ambao umefanyika ni mzuri. Ni lazima sasa Serikali iweze kusimamia, ili basi, katika utekelezaji wa agizo hili la Serikali kusije kukaibuka sintofahamu na changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria ya majengo ya awali inasema kabisa kwamba suala la kulipa kodi ya majengo ni suala la mwenye nyumba si suala la mpangaji. Kwa hiyo kwenye agizo hili nataka nimuombe sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, atakaposimama hapa kuja ku-windup bajeti yake atuambie Serikali imejipangaje, ina mkakati gani wa kuondoa sintofahamu kati ya mwenye nyumba pamoja na mpangaji? Kwa sababu ni kweli mmiliki wa nyumba ni mwenye nyumba, lakini kwa kuwa kodi inakatwa kwenye LUKU maana yake atakayekuwa anakatwa ni mpangaji na si mwenye nyumba. Kwa hiyo nilikuwa naomba Serikali ilete utaratibu mzuri ambao imejipanga kuhusiana na kodi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunafahamu katika sheria ya kodi wazee wa miaka 60 walikuwa exempted kwenye kulipa kodi hii. Sasa sijajua, kwenye sheria hii haijazungumza kwa sababu sheria hii imesema kwamba agizo hili kwenye bajeti, kwamba ni nyumba yoyote ambayo ina umeme. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-windup atuambie kuhusu kwa wale wazee ambao wana miaka 60 na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, kuna zile nyumba ambazo inakuwa ni nyumba moja lakini kila mtu anakuwa na LUKU yake, utaratibu utakuwa vipi? Kama haitoshi kuna yale maeneo ambayo yalikuwa nje ya wigo wa kodi; kuna maeneo ambayo kodi hii ilikuwa haiwagusi, je, Serikali imejipangaje kuweza kuhakikisha kwamba kodi hiyo wakati wa kuanza kuikusanya haitaleta mgongano? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalize kwa kusema kwamba, bajeti hii ni nzuri sana. Ni kwa sababu ni takwa tu la kisheria kwamba ijailiwe, lakini ilipaswa ilipomalizwa kusomwa pale Wabunge wote tuipitishe iweze kupita kwa kishindo kwa sababu imebeba mambo mazuri sana. Rais wetu ni sawa na mama ambaye ameandaa chakula kazi yetu imebaki ni kuweza kula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niwaombe Waheshimiwa Wabunge, tuiunge mkono bajeti hii kwa sababu, imekusudia kuweza kutatua changamoto mbalimbali kwa wananchi. Ahsante. (Makofi)