Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti hii. Kimsingi kwa sababu Rais sasa ni mgeni na hii ndio bajeti yake ya kwanza, niseme tu tunatoa ushauri kwa Serikali, yale ambaye yalikuwa yakikosewa awamu zilizopita, tunaomba bajeti hii wasiendelee kuyakosea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama wengi walivyosema, tunazungumzia TRA ambayo sisi kama Watanzania tumeipa jukumu la kuweza kukusanya kodi kwa niaba ya wananchi wote. Leo hii TRA, imeshindwa kukusanya kodi sawasawa na malengo ambayo sisi tuliwapangia wakusanye kodi. Tunafahamu kabisa bajeti yetu ni ya kukusanya kodi na kutumia. Kwa hiyo wanapokosea na wanapofanya chini ya kiwango cha ukusanyaji kimsingi inachelewesha maendeleo ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TRA wana uhaba wa wafanyakazi na mtu anayesimamia TRA, kwa TRA iliyopita kuna wakati tuliona walichukua hata vyombo vya usalama kusaidia kukusanya kodi. Watu wa TRA wanatakiwa wasomee na ndio maana kuna Chuo cha Ukusanyaji wa Kodi. Tunaomba sana, TRA iwajengee uweze wafanyakazi wake wa ukusanyaji wa kodi na hasa hasa kupata mafunzo ya mara kwa mara ili wawe makini na wawe na weledi katika ukusanyaji wa kodi. Mlipakodi ni mtu namba moja anayefanya nchi hii iendelee, ukimwendea kibabe, ukamwendea kwa hali za vitisho, walipakodi wengi wanajificha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado TRA haijaweza kufanikiwa walipa kodi ni akina nani, wachache wanaowafahamu hao ndio wanao wabana zaidi. Namwomba Mheshimiwa Waziri tuhakikishe TRA inafanya identification ya walipakodi wa Nchi nzima ili kodi iweze kulipwa kwa usahihi na ufasaha zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Ukaguzi wa CAG wa mwaka 2019/2020, CAG anasema katika wale watu ambao wamekwepa kodi na Baraza ya Kodi tunadai kodi zaidi ya trilioni 360. Hii ni nini? Ni kwamba bajeti ya nchi hii zaidi ya miaka mitano inaweza ikajengewa uwezo kutokana na fedha hii ambayo inapotea kwa wale watu ambao hawalipi kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Mabaraza ya Kodi ambao wao wanatakiwa wafanye kazi kesi kwa sisi tunaowadai, TRA haijafanya kwa ukamilifu. Pesa hii trilioni 360 na Mheshimiwa Rais anisikilize, tunahitaji kuhakikisha TRA inasimamia fedha hizi ili ziende kuongeza maendeleo ya nchi hii; kwa sababu leo hii tunakusanya fedha kidogo, bajeti yetu ya mwaka mmoja ukijumlisha hizi trilioni 360 ni miaka kumi takriban tunaweza tukakaa tunakula pesa ambayo ipo mikononi kwa watu haijakusanywa sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nini tufanye? Kwanza kabisa nimesema lazima wafanyakazi wajengewe uwezo, hicho ni cha msingi. Pia Ikama ya TRA ina wafanyakazi wachache sana ambao hawajaweza kuajiriwa na kutusaidia kukusanya kodi. Ni aibu sana watu wanaokusanya kodi eti wana uhaba wa wafanyakazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji kabisa kwenye ile Mamlaka ya Rufani ambayo ndiyo nimesema wao wanao wajibu wa kufanya hizo kesi lazima tuwaongezee nguvu waweze kufanya kesi za ukusanyaji wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nizungumzie wafanyabiashara. Leo hii kwenye biashara ili ufungue biashara kuna tozo nyingi sana na ziko scattered. Lazima tuwe na one stop center ambayo mfanyabiashara akitaka kufungua biashara yake ahakikishe anakwenda anakutana na OSHA sehemu moja, akutane na watu wa mamlaka ya halmashauri sehemu moja, sio kwamba anakaa mwezi mzima kwenye dirisha moja akifuatilia namna gani afunguliwe biashara. Akimaliza hapo tena unamtuma aende OSHA, akitoka OSHA anakwenda kwenye halmashauri anakutana napo kuna tozo, hii inaleta usumbufu kwa wafanyabiashara. Tunaomba wawe na eneo moja, mtu akiamua kufungua biashara isiwe ni mateso, kazi yake iwe kutafuta mtaji wala siyo kuhangaika namna ya kufungua biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la kilimo. Asilimia 65 ya Watanzania wanategemea kilimo, lakini leo hii nikizungumzia Nyanda za Juu Kusini ambayo ipo kwenye big five ambayo inalisha Taifa hili, leo hii hatuna mkakati makini kwenye kilimo hususan kwenye utafiti. Leo ukienda Mbeya kuna Chuo cha Uyole, huu ni mwaka wa tatu hawajapata fedha za utafiti. Huwezi kuwa na kilimo bila ya utafiti. Ni lazima uwekeze kwenye utafiti ili ujue udongo huu unafaa mbegu gani, ili ujue mazao haya yanafaa maeneo gani, lazima watafiti watutangulie. Kama kilimo kinachukua asilimia 65 ya Watanzania, tunahaja ya kuwekeza maeneo hayo ili tuweze kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii bajeti ya kilimo inakwenda chini ya asilimia 30. Huwezi kupitisha bajeti kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania utekelezaji wake ambao Wizara ya Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, Mheshimiwa Waziri haipeleki fedha kwa wakati na inapeleka chini ya kiwango. Hatuwezi kufanikiwa, kwani kilimo ndio kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukizungumzia kilimo, tunazungumzia masoko, vitu hivi vinakwenda sambamba. Leo hii katika Nyanda za Juu za Kusini tumekuwa wakulima wazuri wa parachichi. Tunaita ni zao la kijani, zabibu ya kijani, lakini leo hatujajua yakini wanunuzi wa parachichi waliowekeza huko Iringa, Njombe, Rungwe, na maeneo kama haya wanauza kiasi gani nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli wananunua kwa kilo moja 1,500 sisi unafahamu tulikuwa tunauza maparachichi 10 kwa buku, lakini leo wanachukua kwa 1,500 kwa kilo, lakini bado kuna haja ya kuchunguza, kama mwekezaji ananunua parachichi, amesafirisha zaidi ya container 100 yeye kapata kiasi gani? Kwa maana ukienda nje, unakuta parachichi moja unaweza ukapata kwa dola 1.9 ambayo hiyo ni karibu Sh.3,000 kwa nini mkulima asiuze kwa bei kubwa 1,500 bado naona ni ndogo, naomba Mheshimiwa Waziri Mwigulu asimamie hilo ili wakulima wetu wapate fedha sahihi na sawasawa na thamani ya zao lao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia masoko nikija suala la chai. Nimekuwa nikizungumza sana suala la chai katika Bunge hili. Hii leo, chai inanunuliwa dunia nzima na kwenye soko la dunia bado ina soko. Katika nchi hii, ukienda Rungwe chai ni Sh.320 baada ya kupiga kelele. Ukienda Njombe chai Sh.500, ukienda Lushoto chai iko juu, mimi nataka kujua Mheshimiwa, Bodi ya Chai ni moja, nchi ni moja na CCM ndio wanaongoza nchi hii, kwa nini kunakuwa na bei tofauti wala hakuna usawa wa bei katika zao moja? Naomba suala la chai lipatiwe jibu makini wakati Mheshimiwa Waziri anapokuja kujibu masuala yake hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la maji. Maji ni uhai, tunafahamu kabisa kwamba maji ndio kila kitu, lakini leo hii, tuna vyanzo vingi vya maji na nijikite kwetu Nyanda za Juu Kusini. Leo hii ni aibu kubwa sana miaka 59 kwenda 60 ya Uhuru hatuna maji ndani ya nyumba za watu tunachota maji mitoni na vyanzo vya maji. Ziwa Nyasa lipo kama ambavyo Ziwa Victoria lipo. Niiombe Serikali iweze kuwekeza kwenye Ziwa hili na tuweze kupata maji katika Mkoa wa Mbeya wote, tupate maji kwa sababu uwezekano wa kupata maji upo na fedha zipo za kuweka maji. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)