Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Chato
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, mmi pia nitajielekeza kwenye sayansi na teknolojia, na maelezo yangu ni dakika tano hadi kumi tu kwa sababu ni sayansi na takwimu peke yake. Nimesoma kwa kina sana taarifa ya Mheshimiwa Waziri na nimesikiliza kwa makini sana michango ya Waheshimiwa Wabunge, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yao, ninakiri na kuamini kwamba wasiwasi walionao Waheshimiwa Wabunge kuhusiana na ushamilifu wa tasnia ya nishati ya miundombinu mingine pamoja na viwanda, inatakiwa iangaliwe kwa umakini mkubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasahau niunge mkono hoja hii ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na takwimu za kisayansi. Tunapozungumza viwanda na biashara, tunapozungumza karne ya viwanda vya kati na ikiwezekana vya juu tunamaanisha miundombinu mingi sana na lazima nikubali kuna changamoto, siyo suala la siku moja wala mwaka mmoja. Lakini nishati kwenye viwanda ndiyo uchumi wenyewe, huwezi ukazungumza viwanda, huwezi ukazungumza chochote kama hujazungumza nishati ya umeme, kwa hiyo nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge na wananchi wengine wanaochangia kwa hoja hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nianze kutaja takwimu, Serikali namna ambavyo imejipanga na nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wa Bunge lililopita kwa sababu mlipitisha mipango hii na sasa ni utekelezaji wake. Leo Tanzania tumegundua kiasi kikubwa kweli cha gesi ambacho mnajua sasa ni trilioni cubic feet 57 wote tunajua, ni gesi nyingi kwa Afrika sisi ni wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeki, leo tunapozungumza uwezo wa kuzalisha umeme, Tanzania kwa leo anayetuongoza kwa Afrika Mashariki ni Kenya peke yake mwenye megawatts 2,357, Tanzania ni ya pili. Tanzania tuna megawatts jumla wake 1554.12; Wanyarwanda wana megawatts 49, Waburundi wana megawatt 185; Waganda wana megawatts 185.6; kwa hiyo sisi ni wa pili na tunatembea. Tunakwenda mbali na hapa tunazungumzia umeme utakaozalisha viwanda vidogo vidogo na vya kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazungumza tuna uhakika wa umeme nimezungumza kwa ujumla wa megawatts nilizotaja, lakini bado tunaendelea na kugundua umeme wa maji, wenzangu wa Kigoma wamezungumza, Kigoma wanatumia umeme wa mafuta ni kweli na wanatumia zaidi ya shilingi milioni sitakwa siku, sasa umeme wa Malagarasi unakuja, tunaanza kujenga Malagarasi kuanzia mwezi wa tisa mwakani na ni ujenzi wa miaka mitatu, 2019/2020 umeme wa maji Kigoma unatembea na tunawatundikia umeme huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kusema umeme wa viwanda ndiyo huo tunaosema umeme unaotabirika. Sasa hivi wananchi wa Kigoma wanatumia takribani megawatts 15, sasa megawatts 44.8 za Malagarasi zinawatosha na maeneo ya jirani watautumia. Kwa hiyo, viwanda vya tumbaku vya Kigoma, viwanda vya samaki vya Kigoma, viwanda vyote vya nguo na kadhalika vitatembea sasa kwa umeme wa maji. Kwa hiyo, nataka kuwaondoa wasiwasi wanachi wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili niunge hoja mkono vizuri kwenye hoja ya viwanda nilikuwa nazungumza ugunduzi wa umeme, tunatoka sasa kwenye umeme wa mafuta tunaelekea kwenye umeme wa gesi na maji. Mwaka huu tarehe 1 Aprili, tumeachana na umeme wa mafuta megawatts 70 wa Aggreko, kwa sababu tunataka kutumia umeme wa gesi tunaanza sasa kusafirisha umeme naomba wananchi na Waheshimiwa Wabunge ninapokuwa nataja zile megawatts muwe mnashangilia basi kwa sababu ni juhudi zenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa na hizi ni juhudi zenu Waheshimiwa Wabunge leo Kinyerezi I tunazalisha megawatts 150 na tunaongeza megawatts 185 extention yake. Kinyerezi II Mheshimiwa Rais amezindua tena megawatts 240, Kinyerezi III megawatts 300, Kinyerezi IV itakuja baada ya miezi miwili megawatts 320, huo ni umeme wa gesi peke yake na bado tunaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mtwara kuelekea Songea, Symbion na TANESCO wataanza tena megawatts 600. Waheshimiwa Wabunge, suala la umeme, suala la viwanda ni la kufa na kupona, Waheshimiwa Wabunge nizungumzie usafirishaji wa umeme. Tunaanzia Zambia, tunachota umeme Zambia unaoitwa ZTK tunasafirisha kwa kilovolt 400, tunautoa Zambia kuuleta Iringa – Mbeya kilometa 292, tunasafirisha kilowatts 400. Lakini tunautoa huo huo wa megawatts tunaupeleka mpaka Arusha mpaka Namanga, kilometa 412; sasa huu umeme unapita wapi siyo kwa watu na viwanda? Lakini bado tunapeleka umeme North West Grid wenzangu wanajua, umeme huo unatoka Mbeya unapita Sumbawanga, unapita Mpanda, unapita Kigoma mpaka Nyakanazi kilometa 1,284. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizo ni kilovolt 400 za umeme na hapa tunataka tuwaeleze wananchi kwamba sasa umeme utakuwa ni uhakika, lakini bado tuna umeme unaotoka North East Grid kutoka Dar es Salaam Kinyerezi unapita kwa mwenzangu Chalinze Mheshimiwa Kikwete unakwenda mpaka Tanga, una kwenda mpaka Arusha kilometa 664 za umeme, zote ni kilovolt 400 lakini bado tunatembeza umeme huo kutoka Makambako kwenda Songea kilovolt 220 na ni kilometa 100 zote hizo tunatembeza umeme, tunatoa umeme kutoka Geita kwenda Nyakanazi kilovolt 220 kilometa 133, huo ni umeme na yote haya yanajenga viwanda vyetu. Waheshimiwa Wabunge naomba tukumbuke sasa tumedhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bei ya umeme, bei ya kuunganisha umeme sasa hivi ukijaza fomu ni bure, ukishaunganishiwa service charges sasa hivi ni bure, sasa tunataka umeme gani wananchi, Waheshimiwa Wabunge tutajenga viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kutaja ndugu zangu juhudi ambazo tumezifanya, sasa hivi tunapozungumza kuhusu ugunduzi pale Madimba - Mtwara leo tunazalisha trilioni themanini cubic feet za gesi na tunaweza tukafikisha 130 tunachohitaji watu wajitokeze kuusomba umeme wa gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunazalisha umeme mwingi wa gesi kuliko mahitaji pale Mtwara, lakini bado pale Songosongo tuna uwezo wa kuzalisha sasa hivi trilioni cubic feet 130 hadi 200 na hakuna wanaousomba, tunasubiri viwanda. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge, takwimu tunazosema ni za kisayansi na tunataka tujenge viwanda vya kisayansi na siyo maneno. Nilisema nitatumia dakika tano tu kwa sababu nikibaki humu nitawa-bore, lengo langu ni kuwaletea takwimu za kisayansi zilizokusudia kujenga umeme, viwanda pamoja na miundombinu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungemze jambo la mwisho ambalo tulieleza kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kwamba leo Watanzania wanaopata umeme kweli ni wachache asilimia 40 lakini tunakusudia ifikapo mwaka 2025 Watanzania zaidi ya asilimia 75 watakuwa wanatumia umeme wa uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natamani niendelee lakini nataka wananchi na Wabunge wabaki na kumbukumbu hizi, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi kwamba sasa Awamu ya Tano inakuja na umeme unaotabirika wenye gharama nafuu na ambao pia sasa hautakuwa unakatika, tukishaunganisha hizi kilovolt 400 leo ni kweli umeme unakatika kwa sababu tunatumia msongo mdogo zaidi 132 na 220, ifikapo mwaka 2019, tutakuwa tumeshaunganisha miundombinu yote ya kilovolt 400 na umeme sasa utakuwa ni wa uhakika ambao utakuwa haukatikikatiki. Tunajipanga kwa hilo ili kusudi viwanda vya sasa viweze kujengwa kwa uhakika na wananchi wafanye biashara zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo machache maneno mengi sipendi, nataka mtakapokuja hapa kupitisha bajeti yetu tutaendelea kutundika umeme katika viwanda ili vianzwe kujengwa na maendeleo yaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja.