Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kibiti
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili kuweza kuchangia bajeti hii, bajeti ya kihistoria kabisa. Kabla sijaanza kuichangia bajeti hii nilikuwa naomba tu kwanza nimtoe shaka Mheshimiwa Waziri na kumpongeza yeye pamoja na timu yake. Siku ya tarehe 10 Juni, 2021, wakati ana windup bajeti alisema bajeti hii inaweza kumfanya yeye awe very unpopular Finance Minister kwa sababu yupo tayari kupendwa tu na washabiki wa Yanga na wale Wapiga Kura wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimtoe wasiwasi, nimwambie tu bajeti hii imekufanya kuwa very popular Finance Minister, kwa sababu amekwenda kugusa maisha halisi ya wananchi na amekwenda kujibu maswali ambayo wananchi walikuwa wanahitaji. Kwa tafsiri hiyo hiyo, maana yake ni nini? Amekuwa very popular kuliko alivyokuwa popular kuwa mshabiki wa timu ya Yanga. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee kwa kusema kwamba, naomba sasa nichukue nafasi hii, nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa mambo makubwa na mazuri ambayo ameanza kuyafanya tangu alivyoweza kuingia madarakani. Kabla sijaichangia bajeti hii nataka niguse matatu, manne tu ambayo Mheshimiwa Rais ameweza kuyafanya yameweza kutupa matumaini na vile vile kuwapa ladha nzuri sana wananchi kujua kwamba sasa tunakwenda katika kazi yenye kuendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja la msingi ambalo Mheshimiwa Rais ambalo ameweza kufanya ameweza kutupa fedha za takriban shilingi bilioni 172, zimekwenda katika majimbo ya Wabunge wote ambao wapo ndani humu katika Bunge hili. Ikiwemo kule Mtwara Kusini pamoja na Nkasi vile vile zimekwenda katika maeneo ya Tarime na maeneo mengine. Tumepewa fedha hizo ili kwenda kusaidia katika masuala mazima ya TARURA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, Mheshimiwa Rais jambo lingine la msingi ambalo ameweza kulifanya; ameweza kuweka jiwe la msingi katika kuhakikisha kwamba barabara ile Standard Gauge inaanza kujengwa kuanzia Mwanza kwenda kule Isaka na bilioni 300 tayari zimeshatoka. Nani Kama mama? (Makofi)
WABUNGE FULANI: Hakuna.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivyo haitoshi, Mheshimiwa Rais katika jambo lingine la msingi ambalo ameweza kutufanyia sisi Wabunge, ametupa heshima kubwa sana kwani ameweza kuhakikisha kwamba kila Mbunge ambaye yupo ndani humu katika Jimbo lake imechaguliwa kata moja kwenda kujengwa shule ya sekondari. Nani kama mama? (Makofi)
WABUNGE FULANI: Hakuna.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema haya machache, naomba sasa nijikite katika bajeti ambayo bajeti hii imekwenda kutengeneza taswira nzima na kujibu maswali ambayo wananchi wetu wengi sana walikuwa wanajiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, moja la msingi ambalo limeweza kufanyika katika bajeti hii ni suala zima la kuweza ku-reduce ile tax ambayo wanaenda kukatwa wale wafanyakazi wetu. Imetoka kwenye asilimia tisa sasa inakwenda kwenye asilimia nane. Mheshimiwa Waziri wa fedha naomba tu nimwambie, yuko very popular kwa sababu alichokifanya amekwenda kuwafanya wafanyakazi waendelee kuwa na disposable income ambayo inakwenda kuwasaidia kwa namna moja ama nyingine waendeane na kasi ya kimaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivyo haitoshi, jambo lingine la msingi ambalo limefanyika katika bajeti hii na hili ni la msingi kweli kweli. Naomba tu niseme kwamba kuna katozo kameweza kutozwa kale kanachohusiana na mambo mazima ya mafuta Sh.100. Naomba niseme tu fedha hii ambayo inatozwa ni fedha ya msingi kwa sababu inakwenda kutatua kero za wananchi kule vijijini. Kwa kusema hivyo tafsiri yake ni kwamba, naomba niungane na Mheshimiwa Juliana Shonza yale aliyokuwa ameyasema, akinamama walikuwa wanapata adha kubwa sana. Mazao yetu yalikuwa hayawezi yakaenda katika masoko kwa wakati. Mheshimiwa Waziri, katika jambo la msingi ambalo ameweza kulifanya, hili ni mojawapo. Tunamshukuru sana na tunampongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, katika jambo la msingi ambalo ameweza kulifanya, hili ni mojawapo. Tunamshukuru sana na tunampongeza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nami niseme tu, bajeti hii tunapoenda kuiunga mkono mpaka wale rafiki zetu ambao tumewafunga speed governor watakwenda kuunga mkono bajeti hii, kwa sababu ni bajeti ambayo kwa namna moja ama nyingine imekwenda kugusa maisha ya wananchi kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo yote, naomba tu niseme TARURA ni sehemu ambayo ilikuwa ina kero kubwa sana. Wakati tunachangia hapa Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, kwa mara ya kwanza niliweza kupokea shikamoo ya Mheshimiwa Waziri wakati anataka tuipitishe bajeti ile. Mambo yalikuwa magumu sana humu ndani. Mheshimiwa Rais ameliona hilo. Fedha zinaoenda kupatikana takribani shilingi bilioni 332, tunaweza kuziongeza kule. Hizo tunaenda kuongeza na shilingi bilioni 172 ambazo Mheshimiwa Rais tayari ameshatupa. Haya ni mambo ya msingi kabisa. Nani kama mama? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee mbele. Katika mambo mengine mazuri ambayo bajeti hii imeenda kugusa wananchi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba, wewe utaendelea kuwa popular, ondoka kule katika Yanga, njoo Simba. Moja la msingi umeweza kulifanya, umekwenda kuwasaidia wananchi wanyonge, bajeti imekwenda kuongezeka shilingi bilioni 500 sasa, tunakwenda kutoa mikopo kwa wanafunzi. Nani kama mama? (Kicheko/Makofi)
WABUNGE FULANI: Hakuna. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niendelee kusema tu, kule kwangu katika maeneo ya Kibiti na maeneo ya kule Mbeya na maeneo mengine yote, kuna wanafunzi wengi sana ambao wapo katika maisha ya kawaida sana. Bajeti hii imekwenda kuongeza shilingi bilioni 500, sasa wanafunzi wanakwenda kukopa na wanakwenda vyuoni. Nani kama mama? (Makofi)
WABUNGE FULANI: Hakuna. (Makofi)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niendelee mbele. Mama huyu mambo makubwa sana ameyafanya. Naomba tu niweke rekodi sawa sawa kwenye Hansard, ninaposema mama, nakusudia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu, mama yetu Mheshimiwa Nama Samia Suluhu Hassan. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote haya, naomba niishauri Serikali katika jambo moja la msingi, hasa katika suala zima la kukusanya mapato. Tozo tulizokuwa tumetoza, shilingi moja, bado haitoshi kwa sababu TARURA mtandao wa barabara waliokuwa nao ni sawasawa na kilometa 108,449.19. Fedha ambazo tulikuwa tumewapa mwaka jana, 2020 zilikuwa ni shilingi bilioni 245. Ili TARURA waweze kufanya kazi kwa usahihi wanahitaji shilingi trilioni moja ili sasa kwa namna moja ama nyingine waende kutatua kero zote. Naomba nitoe ushauri kwa Serikali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ikiwezekana tuangalie suala zima la TV License. Hili jambo liko wazi. Mimi nilipata bahati ya kwenda kutembea kwa Wandengereko kule. Wao walichokuwa wanakifanya, kuna kitu kinaitwa TV License pale Uingereza. Nasi siyo vibaya tukifanya hivyo. Ukienda katika database ya Azam utakuta watu waliopo. Tuna Azam, Zuku, DSTV, Star TV; in totality, Mheshimiwa Waziri chukua tu kwamba viwers wako 1,000,000, ambao wana-own TV. Wanapokwenda ku-subscribe pale, sisi tuchaji shilingi 1,000 tu kwa kila mwezi. Tafsiri yake ni nini? Tunakwenda kukusanya shilingi bilioni 120. Tukifanya hivyo, tunakwenda kuupanua wigo huu ili sasa tuweze kumsaidia mama, twende tusonge mbele ili sasa hii bajeti ambayo inakwenda kujibu maswali ya wananchi, iweze kukamilika na wananchi hawa wafurahie kuwa na Mama Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kama Amiri Jeshi Mkuu wa nchi yetu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivyo haitoshi, eneo lingine ambalo naomba nilikazie vizuri ni katika suala zima la kufanya projects hizi kubwa kubwa. Mnajua tumefanya utaratibu. Mheshimiwa Waziri amekuja hapa, ana taswira nzuri sana ya kusema kwamba tunakwenda kuitengeneza miradi mikubwa mikubwa kwa kupitia mambo mengine kama vile infrastructure bond. Nina ombi vile vile Serikali tuweze kuangalia suala zima la PPP. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, PPP tunapaswa tuitumie kwa namna moja ama nyingine. Siyo vyema kweli kuitumia katika infrastructure kwa sababu najua hilo ni eneo liko very sensitive, lakini tunayo miradi mingine. Kwa mfano, tuna mradi ambao tunakusudia katika Wizara yetu hii ya Uvuvi kwenda kule katika deep sea kuvua samaki. Tunakusudia vile vile kwenda kujenga bandari. Haya hatuwezi kuyafanya kama hatuwezi kwenda katika suala zima la PPP. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, muda huu hautoshi, lakini kule kwetu sisi Wandengereko huwa tunasema, mtu akifanya vizuri sana, huwa tuna ngoma ya kuicheza. Tuna ngoma inaitwa Kinyantindili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiniruhusu nicheze tu kidogo nidemke. Kama utaniruhusu ili tuweze kumpongeza mama. Unaniruhusu? (Makofi/Kicheko)
NAIBU SPIKA: Hapana Mheshimiwa Twaha. Hapana, ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Naibu Spika, kama huniruhusu basi mimi nitakachokifanya niseme tu nitakwenda kuandika paper na hii tutaiita concept note. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mama yangu, nakushukuru. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Kicheko/Makofi)