Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nitoe mchango wangu kidogo kwenye Hotuba ya Bajeti iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Kwanza nimpongeze yeye Waziri wa Fedha na pia Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Bajeti kwa uwasilishaji mzuri, hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nami nianze kuchangia maeneo ya uchumi machache, lakini mwishoni nitatoa pongezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze pale ambapo mwenzangu ameishia. Nimekuwa nikishangaa sana ninapoona Wachumi wa Benki Kuu, Wachumi wa Wizara ya Fedha na Wachumi wa Serikali wanatamba kwenye taarifa mbalimbali unajua Tanzania tuko imara, mfumuko wa bei uko asilimia 3 hadi 5 kwa miaka miwili mfululizo iliyopita na maoteo hivyohivyo mwaka ujao, halafu wanatamba kwamba, ni kitu kizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hilo sio zuri kwa sababu tuna uchumi imara. Tuna stable economy, ilitakiwa wacheze na buttons za kuweza kuruhusu inflations angalau isogee kwenye viwango vya SADC kati ya asilimia 5, asilimia 6, asilimia 7, asilimia 8, ili kuweza kuufumua uchumi usisimke watu wawekeze wapate faida za muda mfupi na muda wa kati, ili uchumi uweze kuwa stable zaidi na kutozalisha ajira kwa wingi na tuzalishe fedha kwa wingi ndani ya nchi, lakini iliyopo sasa hivi ni kwamba, uchumi ni kama vile uko- dormant. Kwa hiyo, suala hili la inflations asilimia 3 nikizungumzia kwa upande wa wakulima, wameathirika vibaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uhamasishaji wa Serikali wakulima wamezalisha mazao ya chakula, wameongeza kwa zaidi ya tani milioni mbili katika kipindi cha miaka mitano iliyopita; mwaka 2015 walizalisha tani milioni 15 mpaka ilipofika 2019 tulikuwa na tani milioni 17 za chakula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa sababu ya inflation iko asilimia 3 matokeo yake ni nini, debe ambalo lilikuwa linauzwa shilingi 6,000, 8,000 mwaka 2015 leo linauzwa shilingi 3,000 hadi 5,000, ni kilio kikubwa sana kwa wakulima. Lakini suluhisho ambalo lingeweza kuchukuliwa na Serikali ambalo sijaliona kwenye hotuba ni kuwa na price stabilization fund ambayo ungeweka buffer stock wakulima wakizalisha zaidi ya mahitaji ya soko la ndani Serikali inanunua kilichoongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mwaka jana ingenunua tani milioni tatu ina maana kwamba, leo debe la mahindi lingeuzwa shilingi 6,000 na kuendelea, bado wakulima wasingekuwa kwenye kilio. Kwenye bajeti hii sijaona ile stabilization fund ya Serikali kwa sababu, Serikali lazima iongeze matumizi katika kuokoa uchumi wa nchi, hasa uchumi wa wakulima, lakini vilevile suala hilo lingeweza kuwapa nafuu wafanyabiashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitatoa mfano, mfano sera za fedha zinatwambia kwamba, mwenendo wa mikopo kwa sekta binafsi umekuwa ukishuka. Mwaka 2019/2020 ulikuwa asilimia 13.5, mwaka 2020/2021 ulikuwa asilimia 11.6, maoteo ya mwakani 2021/2022 itakuwa asilimia 10.6 maana yake nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake ni kwamba, wafanyabiashara wanapunguza kukopa kwenye benki. Maana yake nini? Maana yake benki zinaatamia fedha. Fedha zinakuwepo, lakini hakuna mkopaji. Kwa sababu, gani hawakopi? Kwa sababu kuna masgarti ambayo sio rafiki ya riba ambayo yanaathiri faida. Mtu huwezi kukopa kwa sababu huwezi kupata faida na huo mkopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania pekee ndio utakuta tofauti ya riba ya mkopo na tofauti ya riba ya amana iko kati ya asilimia 7 mpaka asilimia 10. Hii ni mbaya sana na upunguaji wake umekuwa unapungua chini ya asilimia 1, sasa data hizo zipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili inatakiwa Serikali ifanye utaratibu mzuri wa kwanza kutokutafiti sababu ni nini? Sababu ni hiyo tu riba au kuna sababu nyingine ambazo zinasababisha?

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo ningependa kulichangia; leo nimemtoa mtoto nenda dukani kanunue lita moja ya mafuta ya kula ya alizeti, kaambiwa dukani kwenye duka la jirani shilingi 9,000. Chupa hiyo hiyo ya lita moja ya alizeti mwaka jana nilikuwa nainunua shilingi 4,500 maana yake nini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana yake kuna shida kubwa ya mafuta hapa nchini. Na viwanda vyetu ambavyo vilikuwa vinazalisha mafuta vimepunguza kuzalisha mafuta, ukiwauliza wanakwambia hatuna malighafi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali nimeona juzi Waziri Mkuu alikuwa Singida, hiyo mikakati ambayo wanaifanya kupitia mikutano ya wadau haitoshi. Inatakiwa ionekane kwenye Government expenditure wamechukua hatua gani za wazi za kuhakikisha kwamba, viwanda vyetu vinapata malighafi ya kuzalisha vitu ambavyo vinaumiza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa ningependa nitoe pongezi. Natoa pongezi bajeti kwa kweli, bajeti kwa ujumla katika maeneo fulani, fulani bajeti imekuwa nzuri sana, hongera sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hongera sana kwa mikakati ya kuongeza fedha kwa TARURA, kimekuwa kilio kikubwa kwa wananchi. Barabara za vijijini ni ukombozi mkubwa sana wa wananchi kuweza kusafiri wao wenyewe na kusafirisha mazao yao kwenda katika masoko, hilo ni jambo moja zuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nime-calculate hapo mtaongeza karibu bilioni 400 kwa ajili ya TARURA, hicho ni kitu kimoja kizuri sana, lakini vilevile mtaongeza fedha kwa ajili ya maji, mtaongeza fedha kwa ajili ya umeme. Hiyo ni pongezi kubwa sana nawapa, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu utapata umaarufu mkubwa endapo masuala hayo matatu yatatekelezwa vizuri na kusimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pongezi kwangu kule mmeweka fedha shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuanza kujenga Barabara ya Ipole – Rungwa. Nawaombea mwakani muweke angalau bilioni 100 kwenye barabara hii kwa sababu, huwezi kuweka bilioni 5 kwenye barabara ya kilometa 172.

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu pongezi nyingine maji Ziwa Viktoria yatafika Sikonge, karibu zaidi ya bilioni 25 hongera sana, lakini Barabara ya Sikonge – Mbono – Kipili itakamilika. Barabara ya Tutui – Zimbili itaendelea kuwekwa changarawe, lakini vilevile tutaendelea kujenga Barabara ya Tabora – Sikonge – Mpanda ambayo nadhani ndani ya miaka miwili ijayo itakamilika. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna mpango mzuri wa kumalizia vijiji kuvipa umeme, lakini kuna kufikisha umeme kwenye Bwawa la Igumula. Kuna kufanya sensa mwaka 2022; hiyo sensa naipa kipaumbele cha juu sana na nitashiriki kwenye Jimbo langu la Sikonge siku zote za hiyo sensa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hongera sana kwa Serikali kupeleka mawasiliano ya simu kwenye kata zote za Jimbo la Sikonge ifikapo mwishoni mwa 2021/2022, lakini pongezi nyingine ni kwa Serikali kuanzisha nature reserve katika eneo la Sikonge ambayo itasaidia kupunguza eneo lililohifadhiwa na kuongeza eneo la wananchi kuishi na kufanya shughuli zao za kiuchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunategemea utekelezaji wa mambo hayo uwe wa makini kwa sababu Serikali hii naiamini sana. Naamini hizi ahadi zote ambazo zimewekwa kwenye hotuba ya bajeti na hotuba za bajeti za kisekta naamini zitatekelezwa. Naomba sana niwashukuru sana Serikali, ahsanteni sana Serikali. Karibuni Sikonge tufanye kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)