Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Gairo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kwanza ya kuchangia. Kwanza nimpongeze dada yetu, Waziri wa Afya pamoja na msaidizi wake, Ndugu yetu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa kuwakilisha hotuba yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitajikita katika sehemu chache tu na za muhimu sana kwa watu wetu wa vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na huu Mfuko wa Afya ya Vijijini (CHF). CHF ukiiangalia sana muundo wake na jinsi ilivyoanzishwa iko ki-theory sana. Ukiiangalia utajua labda huu mfuko ni ukombozi wa wananchi wanaoishi vijijini. Lengo lake kwa wanachama wake ni kuchangia ili kupata huduma za dawa pamoja na vifaa vinavyohusiana na tiba.
Ukiangalia kiundani katika practical hakuna kitu kama hicho. Utakuta vituo vya afya au zahanati zinachangia Mfuko huu wa CHF, zile pesa zinakwenda CHF makao makuu, badala ya watu kuletewa dawa hawaletewi dawa, utakuta wanaletewa condom au vitu vingine tu havina hata msingi, hata chanjo za watoto vijijini zinashindikana. Mimi sioni huu mfuko wa CHF maana yake nini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia katika muundo wake kwa kweli una maana kubwa sana. Mwanachama wa CHF akienda kwenye kituo cha afya au kwenye zahanati kitu atakachoambulia kupata pale ni kipimo tu kama akiambiwa ana malaria hicho kipimo kidogo basi ameshamaliza, zaidi ya hapo dawa nenda kanunue, hakuna dawa. Sielewi mpango huu wa CHF una faida gani!
Mimi nitoe ushauri kama huu mpango wa CHF umeshindikana kwa nini msiunganishe hii mifuko ili mfuko wa bima uwe mmoja? Nina maana kwamba CHF na NHIF uwe mfuko mmoja, kuna faida gani ya kuwa na mifuko mingi ambayo haina faida yoyote? Hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusu madaktari, kwa mwaka wanahitimu zaidi ya madaktari 1,000 lakini wanaoajiriwa hawazidi 300. Halafu tunakwenda vijijini na kwenye vituo vya afya tunawaambia watu wachangie kujenga vituo vya afya na zahanati. Kwa mfano, pale Gairo kuna zahanati zaidi ya sita zimeshajengwa, vituo vya afya viwili mpaka leo havina Muuguzi wala Daktari sasa maana yake nini? Tukija hapa tuna kazi ya kuambiwa tu tuwashawishi wananchi. Mimi kama Mbunge kwa kweli sasa hivi nimechoka simshawishi mtu hata mmoja ajiunge CHF, namwambia kwanza achana nayo nenda na hela yako cash, haina maana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba dada yangu aliangalie sana hili kwa sababu ni Waziri mgeni uwe makini sana na suala hili. Tunapozungumzia habari za afya za watu basi Madaktari muwape ajira na mhakikishe kwamba wanafika Wilayani. Kwa mfano, Wilaya ya Gairo mpaka sasa hivi haina Madaktari kabisa na Wauguzi. Mwaka huu mmetupangia Wauguzi wanne Wilaya nzima na hao Matabibu watano Wilaya nzima kwa kweli haina maana ya aina yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu nataka kufahamu, hii Wizara ya Afya iko tu kazi yake kutengeneza sera au iko kwenye majukumu? Maana mimi naona iko kwenye kutengeneza sera kwa sababu yenyewe inapohudumia inahudumia mwisho Hospitali za Rufaa tu, lakini ukija huku kwenye Hospitali za Wilaya utakuta ziko chini ya Halmashauri. Ukiuliza ambulance, utaambiwa ambulance kwani ninyi hamna mapato? Sasa hizi Halmashauri zinatakusanya wapi mapato ya kutosha wakati ambulance moja ni zaidi ya shilingi milioni 150 au 200! Hizi Halmashauri zitawezaje kupata vitu vyote hivi, zihudumie elimu, maji, majengo yao na ambulance? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu maana inaonekana hii Wizara ingekuwa Bodi tu ingekuwa hamna tena Wizara ya Afya iwekwe Bodi fulani tu basi kwa sababu ukiangalia huduma zake zote ziko chini ya TAMISEMI. TAMISEMI ndiyo imebebeshwa kila aina ya mzigo. Ukiangalia TAMISEMI siyo imebebeshwa mizigo tu imebebeshwa hata majitu mabomu mabomu yale yote yasiyojua kazi yote yako TAMISEMI, sasa kuna huduma gani hapo itakayofanyika ya ukweli? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nazungumza kile kitu cha ukweli, ndiyo ukweli huo. Huduma za afya ni mbovu na utakuta Halmashauri za Wilaya kama kituo cha afya kiko mjini manesi pamoja na upungufu kama wako watano au sita, utakuta wanne wako kwenye kituo cha mjini, kule kijijini utakuta wakati mwingine kama kuna Daktari mmoja ndiyo huyo mpaka anazalisha akina mama, tunawadhalilisha akina mama. Sasa mimi sielewi, kama iko kisera, mimi nataka kujua kisera tu kwa sababu ukija kwenye TAMISEMI ndiyo ina mambo yote ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia pale Gairo, namshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii alizungumza kwamba unaweza ukatoka hapa unaenda Morogoro ukapata accident, sasa ukiangalia katikati ya Tumbi ya Morogoro hapa ni Gairo, kilomita 131 kutoka Dodoma na kilomita 131 kwenda Morogoro, kila siku tunapiga kelele pawepo na madaktari na ambulance lakini mpaka leo hakuna. Mimi nashangaa hapa mkitoa mifano mnatolea Kanda ya Ziwa tu sijui wapi hakuna madaktari mbona hamtolei mfano Gairo, Gairo Madaktari hawapo na ndiyo barabara kuu hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee MSD. Naomba pesa zao wanazodai walipwe zaidi ya shilingi bilioni 130, wapewe hela zao ili watoe huduma safi. Ule mpango wa MSD kuweka maduka ya dawa kwenye Hospitali ya Rufaa isiwe hivyo, waweke maduka yao mpaka Hospitali za Wilaya. Kinachotakiwa kufanyika pale wao wapewe nafasi tu lakini waweke maduka yao. Wanaopenda huduma za afya siyo kwamba wako mijini tu, wako vijijini na Wilayani basi angalau wapewe nafasi kwenye Hospitali ya Wilaya ili nao waweke maduka ili wananchi nao wa sehemu za vijijini na kwenye Halmashauri wapate huduma za MSD. Naona kila atakayezungumza au kwenye vyombo vya habari utasikia MSD imeweka duka Muhimbili sasa hivi ina mpango wa kuweka Morogoro, ina mpango wa kuweka wapi, huku Wilayani vipi au MSD haiko Kitaifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki kugongewa kengele ya pili nafikiri kwa haya machache nimeeleweka, ahsante.