Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Segerea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa hii nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa bajeti yake ambayo imekuja inaleta matumaini kwa wananchi, pia nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu wake kwa sababu hii kazi wanaiweza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii pia kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kutoa milioni 500 kwa kila Jimbo kwa ajili ya barabara zetu na mimi nimekuwa nikichangia hapa siku zote sisi ambao tunatoka Mkoa wa Dar es Salaam au na Mikoa mingine ambayo inafanya biashara au inatumia sana miundombinu, tunamshukuru sana kwa sababu ndiyo kitu kikubwa ambacho tunakipigania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nilitaka niongelee mradi wa DMDP na Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Mwigulu pamoja na Mheshimiwa Ummy tumesha wafuata sana kuhusiana na mradi wa DMDP. Mradi wa DMDP kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni muhimu sana na hata Mheshimiwa Waziri alivyoongea kwenye bajeti yake kwamba wapo kwenye mazungumzo tulitaka tujue haya mazungumzo yataisha lini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama unavyojua baada ya Bunge hapa Wabunge wote tunaenda kufanya mikutano na wananchi wetu na maswali ambayo tutakayoulizwa ni maswali ya barabara na tuna ahadi ya kama Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam, mradi wa DMDP pamoja na Bonde la Mto Msimbazi. Wakati tukiwa kwenye kampeni tuliahidi kwamba tutakapomaliza kampeni Bonde la Mto wa Msimbazi litaanza kutengenezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukaahidi kwamba mradi wa DMDP Phase II utaanza na tayari wananchi wameshaanza kuuliza na tumekaa hapa Mheshimiwa Waziri miezi mitatu tukijadili maendeleo ya wananchi, tukirudi kule inabidi twende tukawaambie, hatuwezi kwenda kuwaambia kwamba Mheshimiwa Waziri katika kusoma bajeti yake amesoma mradi wa DMDP utakuwepo Phase II, utakuwepo lini? mwaka gani wa fedha unaanza? na utaanza lini? ili tuweze kujua tuweze kuwaambia wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu huu mradi siyo kwamba tu upo Dar es Salaam, Dar es Salaam tunaita DMDP, lakini sehemu nyingine wanaita TACTIC kwa hiyo huu mradi upo Miji 45 nani miradi ya muhimu sana, sana Mheshimiwa Waziri tunaomba hayo maongezi ambayo yanaendelea sasa hivi yaweze kumalizika haraka ili hii miradi iweze kuanza, itatusaidia sana wananchi wa Dar es Salaam na ukizingatia Mkoa wa Dar es Salaam kama nilivyosema hapa nilisimama wakati wa bajeti ya TAMISEMI nikasema hatuhitaji mbolea, hatuhitaji sijui stakabadhi ghalani, sijui vitu gani, sisi tunachohitaji ni barabara na maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaolipatia mapato makubwa Taifa letu, kwa hiyo ni Mkoa ambao unatakiwa kulelewa, kuangaliwa, kutengenezewa miundombinu mizuri ambayo wananchi au wawekezaji waweze kuwekeza vizuri wakiona mazingira ni mazuri pamoja na miundombinu yetu ni mizuri tutaweza kupata wawekezaji waje kuwekeza katika Mkoa wa Dar es Salaam, lakini kwa sasa hivi Mkoa ule haufai kabisa, barabara ni mbovu kwa sababu hata master plan ya Dar es Salaam ni mbovu, sasa hivi mvua ikinyesha saa moja mvua ikinyesha Dar es Salaam, kwa sababu hata stendi ya mwendokasi wamejenga kwenye mto, kwa hiyo mvua inavyonyesha tu inabidi kwanza yale mabasi ya mwendokasi wayaondoe yaani mji wote unasimama kwa mvua ya saa moja Mji unasimama kwa siku nzima hakuna biashara inayofanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimekuwa nikisimama hapa siku zote nikisema Mkoa wa Dar es Salaam tunahitaji sana miundombinu kwa sababu hiyo na sasa hivi Mheshimiwa Waziri Mkoa wa Dar es Salaam mvua yaani inanyesha kila siku na watalaam wetu mvua ikianza kunyesha…
MHE. RIDHIWANI J. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa, Mheshimiwa Ridhiwani.
T A A R I F A
MHE. RIDHIWANI J. M. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba hilo jambo lilishajadiliwa humu ndani arudi kwenye Hansard za mwaka 2014 kama sikosei mchango mzuri wa Waziri kipindi kile Mheshimiwa Professor Anna Tibajiuka unaweza kumuelezea nini ambacho kilipangwa katika mradi huo.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Bonnah Kamoli.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa naipokea, lakini mpango wenyewe ulikamilika? Haujakamilika kwa hiyo mimi ninachoongea hapa huu mpango ukamilike, kama ni suala la kujadili hata mimi hapa katika miaka yangu mitano nimeongea sana kuhusu master plan ya Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam sasa hivi ndiyo inatuingizia mapato, ndiyo inatuingizia uchumi, yaani kila kitu kinafanyika Dar es Salaam, hakuna mtu anayeingia kutoka nchi tofauti bila kupita Dar es Salaam, lakini Dar es Salaam yenyewe ukifika tu pale airport ambayo ipo Kipawa, barabara yake ni mbovu, ukija kama ninavyokwambia hayo mabasi ya mwendokasi kama mgeni anakuja siku mvua inanyesha magari yenyewe yamepaki kwa sababu hata huyo mtu ambaye alienda kujenga hiyo stendi akaijenga kwenye Bonde la Mto Msimbazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndiyo maana tunasema kwamba watu wa Dar es Salaam tunaomba sana ili uchumi wetu uweze kukua ni lazima muilee Dar es Salaam nani lazima muitengenezee mazingira mazuri ili barabara zake ziweze kuwa nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara zingine, kwa mfano kama kwenye Jimbo la Segerea, unakuta barabara ya kilometa tano inajengwa kwa miaka mitano. Sasa hapo utaona kweli kuna uchumi gani hapo. Mtu anachukua mzigo wake bandarini mpaka kuufikisha Chalinze masaa 10. Kwa hiyo hayo yote yanaifanya Serikali iweze kupoteza uchumi. Kwa hiyo kama wataweza kutengeneza hiyo miundombinu basi inaweza kuwapatia uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine ambacho nilikuwa nataka niongee ni kuhusiana na kauli ya Mheshimiwa Rais Mama Samia. Mama Samia katika mikutano yake au events zake ambazo alizifanya aliongea kwamba, Manispaa ambazo zinakusanya mapato mengi au mapato kwa wingi inabidi ziangalie barabara zake, yaani pesa zibaki kwa ajili ya kutengeneza barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kauli hii tangu Mheshimiwa Rais ameisema, tunaomba basi Mheshimiwa Waziri utakapokuja kuongea uende waraka wa Mkurugenzi. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Rais amesema, lakini tunataka tujue, ni asilimia ngapi ndiyo itabaki kwa ajili ya barabara, ili Madiwani waweze kujua ni jinsi ya kuweza kufanya mipango yao, wakakaa kwa ajili ya ku-budget fedha hizo za barabara, kwa sababu tangu tumelisema hapa halijafanyiwa kazi. Kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri pamoja na DMDP na hili ni mambo muhimu kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nilikuwa nataka kuliongelea ni kuhusiana na diaspora. Ili kukuza diplomasia ya uchumi, ni lazima hawa diaspora tuwaingize kwenye bajeti zetu. Tuwatengenezee mazingira mazuri ili waweze kuja kuwekeza. Kwa sababu hawa watu wako nje na wana uwezo wa kukutana na watu wengi kule kwa ajili ya kuja kuwekeza huku, lakini tatizo huku mazingira sio mazuri. Nilikuwa nashauri dawati la uwekezaji wawe na special package ya hawa watu wa diaspora ili waweze kuja kuwekeza kwenye nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliongea hapa kwenye Wizara ya Mambo ya Nje, tukasema, kwamba hawa watu pamoja na kwamba wako kule bado ni Watanzania; na kule wanafanya shughuli nyingi ambazo sisi wanaweza wakaja huku Tanzania na wakatuingizia mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa sababu Serikali mnatafuta fedha na mnatafuta uchumi lazima hawa watu waingie, yaani muwatengenezee mazingira waje kuwekeza. Kwasababu, kwa sasa hawa watu wanataka kuja lakini hawawezi kuja kutokana na mazingira kutokuwa mazuri. Kwa hiyo nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Wizara ya Uwekezaji kwamba litengenezwe dawati special kwa ajili ya watu wa diaspora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nililokuwa nataka…(Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Muda umeisha, Mheshimiwa, ahsante sana.
MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)