Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi nichangie kwenye Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kabla sijachangia nipende kuishukuru Serikali kwa kweli kwa kufungua mnada wa Magena uliopo Halmashauri ya Mji wa Tarime ambao ulifungwa tangu mwaka 1997, na tukawa tunakosa mapato mengi sana maana ule mnada una multiply effect. Nashukuru sana, na namshukuru sana Waziri wa Mifugo na Naibu wake; na hii inaenda kuongeza mapato kwenye Serikali Kuu pamoja na kwenye Halmashauri ya Mji wa Tarime. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia bajeti hii kwa kweli ambayo kwa mbali imeonesha matumaini makubwa kwa Watanzania, hasa kada ya wafanyakazi. Japo wameweka tija kwa mbali sana lakini ni mwanga mzuri, ukizingatia miaka mitano yote tulikuwa hatujawakumbuka hawa wafanyakazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutoa tozo ya asilimia sita, ambayo ilikuwa kwenye mikopo ya elimu ya juu. Kwa kweli imeenda kutoa unafuu mkubwa sana kwa wafanyakazi ambao walikuwa ni wanufaika wa mikopo hii ya elimu ya juu. Pia, kwenye kuondoa kodi kwenye cold rooms, Ibara ya 57 imeonesha, hii itachochea zaidi kilimo cha mboga mboga na matunda. Kwa hiyo nashukuru sana kwa hili na kwa kweli kwa hili wanastahili pongezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukiangalia Ibara ya 73 wameonesha kwamba wameondoa faini kutoka shilingi 30,000/= mpaka kuja shilingi 10,000/=, ni jambo jema. Ningependa nishauri pia kuwa wafanye tathmini, kwamba faini isiwe kwenye uniformity, shilingi 30,000/= kwa gari za abiria, kwa gari binafsi na malori. Kama itawapendeza pia fanyeni tathmini ya kina ili muweze ku-charge kulingana na aina ya gari hizo ambazo nimezitaja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa, wamepunguza faini kuwa shilingi 10,000/=, ni jambo zuri sana kwa sababu tunaajiri vijana wengi, lakini hapo hapo wameweka kodi ya kuingiza matairi mapya ya pikipiki, ambao ni ya hawa hawa vijana. Wameondoa kutoka asilimia 10 kwenda asilimia 25; ina maana hapo mnakuwa tena hamusaidii hawa vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningeshauri muiangalie hii, kama mnaweza mkaiacha ikabaki pale pale asilimia 10; kwa sababu hatimaye watashindwa kununua haya matairi, watakuwa wanapewa adhabu ya matairi kuwa kipara barabarani na unakuta hizi shilingi 10,000 zinajirudia mara mbili mbili, na sasa unakuta haujasaidia chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine, ningependa kuzungumzia kwa haraka tu Ibara za 45 na 46 ambazo zimezungumzia kuhusu madiwani, ambapo kwa kweli kwa muda mrefu ilikuwa ni kilio kwa. Vilevile mmeondoa, na kwamba mtakuwa mnawalipa posho ya mwisho wa mwezi kutoka Serikali Kuu kwa halmashauri ambazo zina kipato kidogo; na pale pale mmeeleza kwamba, mnafanya hivyo ili hawa madiwani wasipige magoti kwa wakurugenzi, lakini pia kuongeza ufanisi kwenye shughuli hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikawa najiuliza, kwamba kwa nini mnaweka double standard? Kuwa zile halmashauri 16 zenye vipato vya juu wenyewe waendelee kujilipa? Sasa kama wanaendelea kujilipa hamuoni kwamba inaweza ikatokea sehemu wakurugenzi wakaacha kuwalipa kwa makusudi ili waendelee tu kupiga magoti kwa wakurugenzi? kwa ajili kwamba wana mapato makubwa ili wawalipe. Kwa hiyo ningeomba hili mliangalie, muweke tu kwamba Serikali Kuu mtalipa kwa madiwani wote bila kujalisha kipato cha halmashauri husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mmeweka kwamba ni mapato ya mwisho wa mwezi tu. Kuna halmashauri zingine kwa mfano Halmashauri ya Mji wa Tarime kuna kipindi tulikuwa tunakopa mpaka vile vikao vya madiwani vya kati kati hapo. Yaani vile vikao vile vinavyoendeshwa vinakopwa, sasa sijui hilo mnaliangalia kivipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kuhusu nyasi bandia, ni jambo jema ambalo linaenda kuchochea sekta ya michezo Tanzania, lakini napingana na ninyi kuweka kwenye majiji tu. Naomba sana muondoe, muweke kwa yeyote atakayetaka kujenga viwanja kwa standard ya kuweka nyasi bandia, basi aweze kupata huo msamaha wa kuingiza nyasi bandia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mkoa wa Mara, tuna kiwanja cha Karume pale Musoma Mjini. Pale si jiji lakini kile kiwanja kinatumika kwenye Ligi Kuu. Tukitaka kukiendeleza kuweka nyasi bandia tutashindwa maana mtataka tulipie kodi, ilhali Dar es Salaam na hizo halmashauri za majiji ambazo mmesema zina vipato vizuri wenyewe mnawapa msamaha. Hii naomba kwanza muitumie vizuri, Shinyanga pia inatumika, na kwingineko ambako si majiji. Kwa wekeni wazi iwe manispaa, iwe mji, iwe jiji, watakaokuwa tayari kujiendeleza kuweka nyasi bandia, basi wapate msamaha wa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho kwa kweli naipongeza Serikali ni hili la kuona kwamba wapunguze muda wa mkataba kwa hawa askari polisi kutoka miaka 12 kuja miaka sita, na ikiwezekana mwende mpaka miaka mitatu kama ilivyo kwa JWTZ. Lakini hapa mmewasahau watu walio kwenye idara moja, askari magereza na askari zimamoto nao mikataba yao ni miaka 12.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa nao washushwe kama askari polisi, iwe miaka sita na baadaye huko muwashushe pia kuja miaka mitatu. Lakini pia, ukizingatia, kwa mfano maslahi yao, wako idara moja hawa. Askari polisi mwenye degree analipwa gross salary ya shilingi 860,000 anapewa asilimia 15 ya taaluma, anapewa na fedha ya makazi; lakini askari mwenzake aliye magereza mwenye degree analipwa shilingi 770,000 tu, hapewi asilimia 15 ya taaluma wala hapewi fedha za accommodation. Kwa hiyo naomba muweze kuwapa wawe na usawa kwa sababu wako kwenye Idara moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ni kuhusiana kwa kweli na tozo ambazo tumezi-introduce, Ibara ya 88 ya Sheria ya Posta na Mawasiliano, ambayo inaelekeza kukata kati ya shilingi 10/= mpaka shilingi 10,000/= kwenye hizi za mobile transaction. Fedha hizi zinaweza kufikia takribani trilioni moja na bilioni mia mbili hamsini na nne; na wakati unasoma hapa Mheshimiwa Waziri ulielekeza kwamba zinaenda kwenye sekta ya afya. Na ikizingatiwa sekta ya afya hatujawahi kufikia Azimio la Abuja, ambalo linatutaka tutenge asilimia 15 ya bajeti kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hizi trilioni 1.25 zitaenda huko, na najua hizi fedha kwa hivi mlivyoziweka, lazima zitakuwa zinapatikana automatically. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ziweze kuwa ring-fenced na ihakikishwe kwamba kweli zinakwenda kwenye sekta ya afya kama ambavyo mmetueleza hapa, isiwe kwamba mnawakata Watanzania halafu baadaye hizi fedha haziendi. Tunahitaji, mathalani tukiamua kuwekeza kwenye miundombinu katika hii trilioni 1.234 tukichukua bilioni 800 tu tunaweza kujenga vituo vya afya 2,000 ambavyo hamjavijenga mpaka leo tangu tumepata uhuru wetu. Pia tukachukua bilioni 200 kupeleka kwenye vitendea kazi, dawa na vifaa tiba vingine. Vilevile, tukachukua labda bilioni 252 tukasema tunaweka kwenye zahanati ili kumalizia yale maboma tunaenda kutatua matatizo ya vifo vya mama na mtoto, matatizo ya Watanzania wakiugua kutembea umbali mrefu na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, kwenye Ibara ya 88 hiyo hiyo kumeelekezwa fedha bilioni 322 kwenda TARURA ambazo zimeelekezwa zinaenda kuwa ring-fenced. Pia kuna bilioni 396 ambazo mmesema mmezielekeza kwenye maji. Mwaka huu wa fedha umepita zilienda tu bilioni 292. Sasa hivi bilioni 396 kama kweli zikienda kwenye maji, na kwa bajeti ya maendeleo waliyoomba ina maana kuna fedha zitabaki. Kwa hiyo tunatarajia miradi ya maji tukija hapa mwakani iwe imetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 100; na zote hizi ziwe ring- fenced.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia ukisoma Dhima nzima ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa; unasema ni kujenga uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Na ukisoma pia, Ilani ya CCM Ibara ya 8, mmesema mtazalisha ajira takribani milioni nane. Ukisoma Ibara ya 13 mnajenga Tanzania ya Viwanda, ukisoma Ibara ya 14 mmesema mtatambua na kuthamini sekta binafsi kama ndiyo inayochochea uchumi wa taifa letu. Pia Ibara ya 15 mmesema kwamba mtaendelea kutambua sekta binafsi kuwa ni engine ya kuchochea uchumi wa taifa letu na hivyo mtalinda na kuiendeleza hii sekta binafsi. Sasa, tunaratajia muweze kuyaishi haya mambo; lakini ni kinyume. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia sasa hivi viwanda vingi vimekufa wala hata havihuishwi. Vilevile kuna mazingira yasiyo rafiki kuweza kuvutia wawekezaji waje kuwekeza Tanzania. Sasa ili uweze kwenda na hii ambayo imeonyeshwa kwenye Ilani yenu ya CCM, ni wajibu sasa hivi, sera ya viwanda iweze kuwa attractive kwa investors ili waje kuendeleza viwanda vyetu hivi na vilevile muweze kuona vikwazo vilivyopo. Mathalani, kule kwetu Kanda ya Ziwa kuna viwanda vya pipi vilianzishwa. La Kairo ambaye alienda kuzindua Mheshimiwa Hayati na Jambo Sweet, Kenya ndio wana-supply pipi kutoka Kenya wanaleta huku kwa sababu wao hawana kodi kwa pipi ambazo wana-export. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Tanzania kuna asilimia 25 kama wana-import glucose na sukari kuja kutengeneza pipi hapa; lakini pia wana VAT, kwa hiyo wanashindwa ku- compete. Hivi viwanda vinakufa, na Mheshimiwa Magufuli alienda kuvifungua; Jambo Sweet na hiyo ya La Kairo, lakini sasa hivi vinakufa na ajira nyingi zinapotea na hatima yake hata hayo mapato na na vingine mnakosa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nizungumzie kuhusu viwanda vya matrela. Tunajua tulikuwa na viwanda takribani 10 hapa Tanzania, sasa hivi vimebaki vitatu tu na hivyo vitatu vinasuasua. Kwa nini? Ni kwa sababu matrela yameagizwa kutoka nje, China, German na kwingineko hivyo hawa hapa ndani wanashindwa ku-compete kwa sababu kuingiza matrela mmeweka asilimia 10 tu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tulinde viwanda vyetu ili tupate na mapato nashauri tuweke asilimia 25, ili sasa kama watahitaji kuingiza hayo matrela yaweze ku-compete na viwanda vyetu hapa. Lakini hata hivi viwanda na vyenyewe tuvitunde, tuvisaidie, tuvipunguzie kodi. Tukitengeneza matrela hapa Tanzania tutazalisha ajira nyingi, tutapata SGL, tutapata pay as you earn na kodi zingine ambazo ni indirect zinapatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo la kushangaza sana. Ukiangalia Tanzania hatutengenezi magari, lakini import wameweka asilimia 25, matrela ambayo kuna Watanzania wanatengeneza asilimia 10. Nakuomba sana Mheshimiwa Mwigulu muirudishe, muweke asilimia 25, itaenda kuongeza mapato ya taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine mmeondoa msamaha kwenye taa za solar ilhali mnajua kabisa; mbali na hizi takwimu ambazo tunaziweka kwenye madaftari na kwenye vitabu Watanzania wengi kaya nyingi za vijijini hawana umeme, hawajafikiwa na umeme. Tunategemea taa za umeme wa jua, ambao bidhaa zao pamoja na kwamba huwa kuna msamaha wa kodi bado zilikuwa ziko juu sana. Sasa leo mnaondoa ilhali mnajua kabisa umeme haujamfikia kila Mtanzania kule vijijini kila kaya haina umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nashauri warudishe msamaha kwenye vifaa vya umeme wa jua ambavyo ni ghali sana ili kuweza kuwasaidia Watanzania ambao wamejiwekeza kule. Leo kuna saluni kuna mashine sijui za kusaga, watu wanasindika na nini. Mnavyoweka mnaua kabisa uchumi kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba waondoe kwanza mpaka pale ambapo watakapojihakikishia kwamba kila kaya kijijini ina umeme, ndio waweke sasa hii asilimia 25 ambayo wameileta ili kusema kwamba wapate uwiano sawa. Hivi ilivyo na msamaha uwiano wa bidhaa za umeme wa jua zilikuwa zipo juu sana, ukinunua bulb, wiring yake, ukinunua control unit panel zake, zote zipo juu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba sana, pump zinazotumia umeme wa solar nazo pia wazipe msamaha. Zinakwenda kuchochea umwagiliaji kwa watu wa greenhouses huko vijijini. Ukiwa na umeme wa solar unasaidia, lakini pia wanaofuga samaki and the like. Kwa hiyo naomba sana, Mheshimiwa Waziri aangalie hili ili tuweze kuchochea sekta ya kilimo na mifugo huko vijijini katika kuhakikisha kwamba tunachochea kwenye uchumi wa Taifa hili. (makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, tuhakikishe kwamba hii miradi ya kimkakati kwa kweli inamalizika on time kama SGR. SGR ikimalizika itasaidia sana kuchochea uchumi wa Taifa letu. Itasaidia sana na siyo tu kuchochea uchumi, itapunguza hata na ajira ambazo zinapatikana ambazo zinatokana kwa sababu ya malori makubwa kuchangamana na magari, mabasi na vitu vingine kama hivyo. Tukimaliza SGR kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza ina maana tunakwenda kukuza uchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma transport economy itakwambia, moja ya vitu ambavyo vinasaidia na kuchochea kwenye uchumi, ni kuwa na miundombinu imara ya reli ambayo itasaidia kusafirisha. Kwa hiyo naomba sana, kama fedha tumezitenga hapa ziende tuweze kumaliza huu mradi kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema, maendeleo ya watu it includes elimu, maji, umeme na miundombinu ya barabara kutoka vijijini ambavyo ndio wanalima kuja huku mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa hizi dakika zangu za kuchangia. Ahsante sana. (Makofi)