Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuweza kunipa nafasi hii nami kuweza kuchangia bajeti hii ya Serikali.
Awali ya yote naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Mama Samia Suluhu kwa maono mazuri aliyonayo juu ya nchi yetu, pili nimshukuru sana Waziri Dkt. Mwigulu Nchemba, Naibu wake na wafanyakazi wote wa Wizara ambao kwa namna moja au nyingine wameshiriki kikamilifu katika uandaaji wa bajeti hii. Tatu, naomba niwashukuru sana Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Bajeti, Ndugu yangu Mheshimiwa Daniel Silo, Makamu wake CPA Omar Kigua kwa mchango mzuri walioutoa kwenye Kamati na kuishauri Serikali hatimaye leo hii tunaijadili bajeti hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie katika maeneo yafuatayo, kwanza naipongeza sana Serikali kwa maono yake iliyonayo juu ya kuhakikisha Madiwani wetu wanapata posho moja kwa moja kutoka Serikali Kuu. Tatizo hili lilikuwa tatizo kubwa sana, Rais wa Awamu ya Nne Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alifanya kama leo Mama yetu anavyofanya, aliamua kuhakikisha Madiwani wote wanalipwa kiinua mgongo kutoka Serikali Kuu, hii ilikuwasuluhisho la matatizo kwenye Halmashauri zetu. Leo hii tunapoamua kuwalipa madiwani posho zao kupitia mfuko mkuu tunahakikisha Halmashauri zote tunazitendea haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana posho inayopatikana sasa hivi ni ndogo. Mheshimiwa Waziri kwa kuanzia ajaribu kuona alternative way ambayo tunaweza tukainua kidogo posho za Waheshimiwa hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwangu Mheshimiwa Diwani anahudumia vijiji 12, anatembea ana vijiji 12. Nina Kata mimi inaitwa Kata ya Sengenya Mheshimiwa Diwani ana vijiji 12, posho hii yote anayopata inatumika katika kuhudumia vijiji hivi. Kwa hiyo, badala ya kutumia kidogo kujikimu anajikuta anaitumia kwa ajili ya shughuli za wananchi. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri hili aliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kwa kuamua kuwalipa Maafisa Watendaji wa Kata posho zao, posho za mafuta. Pamoja na kwamba, Maafisa Watendaji hawa hawana vitendea kazi, lakini ninaamini wataitumia posho hii kwa ajili ya kukodi bodaboda, ili kuweza kufanya shughuli za halmashauri. Sisi ni mashahidi, sisi ni Madiwani, tunafahamu Maafisa Watendaji Kata wetu ndiyo wakusanya ushuru wa Halmashauri, ndiyo walinzi wa amani katika Halmashauri zetu kwa hiyo, kwa kweli, hizi 100,000/= watakazopewa zitawasaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu hii isiwe hisani, Wakurugenzi wa Halmashauri wasije wakawakopa hawa Watendaji, walipwe kila mwezi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mwigulu, Mheshimiwa Waziri, lazima utoe paper itakayowa- instruct hawa Wakurugenzi, hakuna kuwaruka, vinginevyo hawa watakopwa. Sheria ya posho huwezi uka-carry forward, kama hautamlipa ndani ya mwaka wa fedha hautasema hili ni deni. Kwa hiyo, Wakurugenzi wengi wanaweza wakatumia kigezo hiki kutokuwalipa posho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu uamuzi wa kuwalipa Makatibu Tarafa ni wazo la busara sana. Hawa ndiyo viungo muhimu, wanafanya kazi kubwa katika Tarafa zetu kwa kweli, mmewapa vitendeakazi kwa maana ya pikipiki, posho hizi zitawasaidia kwenye mafuta, hongereni sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili naomba nikushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kuangalia suala la TARURA. TARURA tulizungumza hapa ndani ya Bunge kwamba, wanapata fedha ndogo, tumewaongezea fedha, jambo hili ni heri kabisa. Rai yangu Mheshimiwa Waziri, kuna Sheria ya TARURA ya mwaka 2007, Sheria ya Barabara, inakataza malori yenye zaidi ya tani 10 kwenda vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kijijini kwetu ndiko ambako kuna mazao, wafanyabiashara, hasa kipindi hiki cha mazao mfano kwangu mimi, huu ni msimu wa ufuta halafu utakuja msimu wa korosho, hakuna lori la tani 10 ambalo litatakiwa lipite. Kwa hiyo, nawaomba sana Mheshimiwa kwa kuwa tunaongezewa fedha naomba Mheshimiwa Waziri ije sheria tuibadilishe, hakuna lori la tani 10 kijijini kwetu malori yote ni kuanzia tani 15, tani 30.
Sasa leo unaposema tani 10 yasionekane vijijini maana yake yakae barabara kuu halafu gharama ya kuanza kutoa mazao kutoka vijijini kuleta barabara kuu, tunaongeza gharama ya uendeshaji. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana hili mliangalie. Hii kero kubwa sana huko vijijini wananchi wetu wanalia, wafanyabiashara wanalia kwa sababu ya sheria hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni Property Tax. Imezungumzwa vizuri, Mheshimiwa Mwigulu nakuunga mkono kwa uamuzi wa kubadilisha njia ya ukusanyaji. Ni kweli 2017/ 2018 Property Tax ilikuwa inakusanywa na Halmashauri kabla ya 2017/2018 ikawa matatizo makubwa. Badaye Serikali Kuu kupitia TRA na sasahivi mmebadilisha utaratibu huu wa ukusanyaji, mimi nauunga mkono. Rai yangu kwao, kupitia LUKU katika wilaya zetu nataka kujua mgawanyo wa mapato utakuwaje? Najua watu watalipa Property Tax kutoka sehemu mbalimbali za nchi hii.
Je, ile Property Tax itakayokusanywa ndani ya wilaya yangu, itabaki ndani ya wilaya yangu au ndio ile asilimia 15 uliyoizungumza kwa utaratibu upi? Lazima tujue mgawanyo halisi wa Property Tax kwenye halmashauri zetu ili halmashauri zetu ziweze kufanya kazi inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine Mheshimiwa Chumi amezungumza, kuna ahadi za viongozi. Viongozi wetu wanatoa ahadi nzuri sana, Mheshimiwa Mwigulu tunakuomba sana hizi ahadi za viongozi muwe mnaratibu na mnaziingiza kwenye bajeti. Isiwe jukumu la sisi Wabunge kuanza kufanya lobbing, kuanza kuwabembeleza kuna ahadi, kuna ahadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi Mheshimiwa Rais alipokuja kwangu wakati wa kampeni aliahidi kujenga barabara ya lami kutoka jimboni kwangu kwenda Mkoa wa Morogoro kupitia Selous, ipo ndani ya ilani, lakini kwenye bajeti haipo. Lini itaingizwa ndani ya bajeti? Nilitarajia leo kingekuja kitabu hapa kikaeleza hizi ni ilani za viongozi wetu. Ilani hii itatekelezwa mwaka huu, ilani hii itatekelezwa mwaka huu, badala ya sisi kuanza kuja kuanza kubembeleza kuna ahadi! Waziri Mkuu 2018 aliahidi barabara kilometa tano ndani ya Jimbo langu, haipo popote tangu 2018 mpaka leo. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Mwigulu, tunaomba hizi ahadi za viongozi wetu mziratibu na mziingize ndani ya utaratibu wa bajeti ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Bajeti ya Serikali Mheshimiwa Mwigulu aliongelea mambo ya msingi mengi, mambo ya kupunguza tozo kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wetu. Mimi naunga mkono mia kwa mia.
Rai yangu Mheshimiwa Waziri yale yote ambayo mmeyaeleza yatekelezwe ndani ya mwaka ujao wa fedha ili tutakapokutana tuweze kuisifia bajeti na utekelezaji wake, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana. Naomba sana itekelezwe kama tutakavyokubaliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)