Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika bajeti hii ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimpongeze Mheshimiwa Rais, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa mambo mengi tu, lakini nimkumbuke aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli. Kama huko aliko duniani na huku nje mambo yakaharibika sisi tutamlaumu yeye aliyetuachia watu wazuri kwenye safu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Magufuli alikuwa utatu mtiifu, Wakristu msinielewe vibaya nikasema Utatu Mtakatifu, utatu mtiifu. Wa kwanza ni huyu Rais wetu wa sasa ambaye alikuwa Makamu wa Rais, Mama Samia, ndiye aliye wa kwanza kwake. Wa pili alikuwa naye Waziri Mkuu ambaye bado anaye Rais wa sasa. Makamu wa Rais wa sasa alikuwa Waziri wake wa Fedha ambaye naye yupo. Hivi nchi inayumbaje, nchi ambayo Magufuli ameiacha kwenye watu waliokuwa utatu wake mtiif inaachaje? haiwezi kuacha. Kwa hiyo mimi naamini katika hili tunaloendanalo nchi itaenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme maneno, na kwa maneno haya msini-quotet mkasema sasa wewe mgombea ukamishna, a’ a’, ni maneno yangu. Nchi yetu inatakiwa iwe na watu watakatifu, watu wakumuogopa Mungu, watu wasio na mapenzi ya kujipendekeza kumbe roho zao zipo tofauti. Wakitokea watu wa namna hiyo na Mama Samia ambaye sasa ni mtiifu wakati wote nchi itakwenda salama; lakini kama kuna watu wala rushwa, watu wabadhilifu watakao mzunguka mama akiwa kwenye jukwaa wanampamba huku ndani wanafanya mambo mengine nchi itakwenda chini.. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi niseme tumuombe Mungu, watakatifu mawaziri wake wote wafuate watu wale watatu ambao Hayati Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli alituachia. Alituachia Makamu wa Rais ndiye amekuwa Rais wa sasa, alituachia Waziri Mkuu bado yupo na anafanya kazi, yaani huyu si wa kusema tena. Hivi nchi inawezaje kwenda nje ya Majaliwa? haiwezekani, nchi inawezaje kwenda tofauti na Mpango? Haiwezekani. Kwa hiyo tuwaombe viongozi wetu, mawaziri wetu na viongozi wote wawe watiifu, roho zao ziendane na wanavyosema kwenye majukwaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi inanishangaza sana kumuona mtu yupo jukwaani anazungumza mambo mazito, lakini huku chini ana mambo ya ajabu sana, mla rushwa mkubwa, kwa nini sasa inakuwa hivyo? Tuombe watu wetu Mungu awasaidie waende upande ule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili nalizungumza polepole maana hili lilikuwa la nchi. Nilikuwa naangalia PAYE ile kodi ambayo inalipwa na watumishi wa Serikali. Waheshimiwa Wabunge nataka hili mlielewe vizuri. Tuna madaraja manne ya PAYE. Daraja la kwanza ni wale watu wa 270 mpaka 540 ambao wanalipa asilimia tisa, maana yake ikipunguzwa sasa itakuwa asilimia nane. Daraja linalofuata ni 540 mpaka 740, hawa wanalipa asilimia 20, ikipunguzwa itakuwa asilimia 19. Daraja linalofuata ni 740 mpaka 1,000,000, hawa wanalipa asilimia 25. Daraja la mwisho ni kuanzia 1,000,000 na kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na Waheshimiwa Wabunge nimesikia watu wengine wanazungumza huko mitaani kwamba Wabunge wanazungumza haya mambo hawalipi kodi; jamani, hii Pay As You Earn maana yake makundi yote sisi ndio tunalipa. Mbunge analipia milioni moja na kitu kwenye makundi yote. Kwa formular hii kundi la kwanza litalipiwa na kundi la pili, kundi la pili litalipiwa na kundi la tatu, kundi la tatu litalipiwa na kundi la nne, kwa hiyo sisi Wabunge makundi yote tunayalipa hela. Sisi ndio tuna kodi kubwa katika watumishi wa Serikali ambao wanalipa Serikalini hapa, kwa hiyo tuseme kwamba tunalipa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nilikuwa na ombi langu hapa, Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba unisikilize hapa kidogo. Mimi naona badala ya kupunguza asilimia moja ya hii kodi hili kundi la kwanza la 270 mpaka 540 tuliondoe, tuliondoe hilo kundi lisilipe kodi kwa sababu ukipiga hesabu yake ni kama bilioni saba au bilioni nane. Tuliondoe tubaki na kundi la pili na kundi la tatu na kundi la mwisho ili hawa ambao wana hela kidogo waendelee kupata kidogo waendelee kuishi. Kwa hiyo ushauri wangu kwa hapo nilikuwa naona hapo inakuwa nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie TRA; na Mheshimiwa Mwigulu kama ni jambo la kutufanyia sisi Watanzania ili tukukumbuke masaa yako yote ni kuangalia mfumo wa TRA kwa sababu mfumo wa TRA si rafiki kwa kukusanya hela, mfumo wa TRA unakupa nafasi ya kwenda kukadiria. Mimi naleta makontena ya bilioni tatu halafu tunakubaliana sasa nilipe ngapi. Mimi ninaduka unakuja kunipigia mahesabu ya bilioni mbili, milioni 500 au milioni 100 au bilioni 50 tunakubaliana nilipe ngapi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tutafute mifumo mizuri ya TRA ili hela zetu ziweze kupatikana, vinginevyo hakuna hela tutakayokusanya hapo. Kwa hiyo tuangalie mifumo ya TRA kwenye maduka, kwenye bandari na kwenye maeneo yote tuweze kuona kwamba tunaifanye mifumo hiyo ili tuweze kuishi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kodi ya majengo. Mimi hii kodi kwangu naona kama ni jambo gumu sana, na hasa kwa watu wa vijijini. Naiomba Serikali, Mheshimiwa Mwigulu wewe ni mtaalam wa hesabu hizi. Hii kodi wala msiipeleke kwenye umeme huko, hii kodi pelekeni kwenye Wizara ya Ardhi. Mtu mwenye kiwanja mumuongezee kakodi hako alipe, si ni mali yake, kuna ubaya gani? Hii kodi msiipeleke popote ipelekeni kwenye Wizara ya Ardhi walipe kupitia Wizara ya Ardhi, mimi nadhani hapo itakuwa nzuri zaidi kwenye upande huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie Deni la Taifa. Deni la Taifa ni himilivu, na tunasema ukiangalia nchi ambazo ni ten bora zenye madeni makubwa ni pamoja na Tanzania, ni ya kumi. Ni kweli tuna deni kubwa, lakini kukopa si dhambi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi tajiri duniani ni Marekani, lakini nchi yenye madeni makubwa duniani ni Marekani. Sasa sijui kama watu mnaliona hilo, nchi tajiri duniani ni Marekani na nchi yenye madeni makubwa duniani ni Marekani; kwa hiyo kukopa si dhambi, mimi nafikiri tunakopa kufanyia nini ndiyo hoja. Kwamba tunakopa kulipa mishahara, tunakopa kufanya vitu ambavyo havina tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi nishauri kwenye Serikali hii ya Awamu ya Sita, Mama asiogope kukopa, akope kwenye malengo maalum. La muhimu hapa sana ninachoomba ni kwamba sisi Wabunge sasa ufike wakati tupewe taarifa, kwamba tumekopa wapi na tunadaiwa wapi, na hili deni tunalipa lini na likoje. Ije taarifa rasmi hapa Bungeni tujue tunadaiwa kiasi gani na tunadai kiasi gani na nani anatudai, tujue ili sisi Wabunge tuwaeleze watu huko, kwamba deni letu ni himilivu, lakini tunadaiwa na watu fulani, lakini kukopa si dhambi; kwa sababu hakuna kitu kinaitwa good debt, madeni yote ni mabaya hakuna deni zuri, hata sisi madeni yetu ni mabaya tu hakuna deni zuri hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie mifumo ya usimamizi wa fedha za bajeti zetu, na hapa ndipo patamu. Kuna watu wanaitwa Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Ma-DAS, Makatibu Tarafa, Wakurugenzi, Watendaji wa Kata na Watendaji wa Vijiji; ni nani anasimamia vizuri miradi inayopelekwa kwenye Vijiji huko na kwenye Kata? Ni nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha sana. Akienda Naibu Waziri kwenye Wilaya anakutana na Mkuu wa Mkoa, anakutana na Mkuu wa Wilaya. Kama kuna hela zimeliwa kwenye Wilaya hiyo Mbunge analalamika, Wananchi wanalalamika, Waziri aliyeenda pale kama ni Naibu au Waziri wa Wizara analalamika, Mkuu wa Mkoa anamwambia Mkuu tuachie hilo tutatekeleza, mwaka wa kwanza. Anakwenda pale Waziri Mkuu mradi ule ule kwenye sehemu nyingine umeliwa, Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wanamwambia tuachie Mkuu hilo tutatekeleza. Sasa najiuliza, hivi nchi yetu imekuwa ya kurugenzi ya matukio?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi inatokeaje mkoa au wilaya fedha zinaliwa milioni moja, milioni mbili, milioni mia tatu, milioni mia nne, kila siku tunapoenda kwenye mikoa na wilaya kuna madeni na kuna hela zimeliwa, Wakuu wa Wilaya ukikutana nao wanakwambia mkuu tuachie, tunatekeleza mkuu tuachie tunatekeleza, watamaliza lini? (Makofi)

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita kuna taarifa.

T A A R I F A

MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpe taarifa mchangiaji, hapo anapoongea ni penyewe sasa, maana tunapitisha bajeti nyingi kubwa lakini ukiangalia kiuhalisia hela zinaliwa na hakuna mtu anayefungwa. Nilikuwa napenda kumpa taarifa mchangiaji yupo vizuri sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita Getere unaipokea taarifa hiyo.

MHE. BONIPHACE W. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Unajua humu ndani tupo tofauti, wapo Wabunge wanaoishi kwenye lami huko na kuna Wabunge tunaishi vijijini, sisi wa vijijini ndio tuna shida. Hivi Mbunge kama mfano Mheshimiwa Zungu, Mwenyekiti wetu ana shida gani kule, kule atazungumza watu wake tu wakawaida wale, lakini ukiangalia magorofa yamejaa, lami imejaa, kila kitu kimejaa; umeme upo vizuri, atazungumza mambo mengine yapo ya kibinadamu lakini si kama ya kwetu vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mfumo wa utendaji wetu ukubalike ili Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wawe na mikataba. Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ambaye eneo lake lina wizi, lina ubadhilifu watuambie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani tukawe na Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa, Watendaji wa Kata, Makatibu Tarafa, Ma-DAS, Ma-RAS miradi inaliwa wapo, ukienda mkuu tuachie, ukienda mkuu tuachie, wanamaliza lini?

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nimpe taarifa kaka yangu ninaye mheshimu sana, Mheshimiwa Getere. Siyo nchini kote Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wanafanya ubadhilifu. Mimi kwa Wilaya ninayotoka, ya Ikungi Mkuu wetu wa Wilaya Mpogoro pamoja na Mkurugenzi wake Kijazi wanafanyakazi iliyotukuka ambayo hata Waziri Mkuu alipokuja kwenye ziara ndio moja ya wilaya alizisifia ambazo hazikuwa na makando makando katika utendaji. (Makofi)

Kwa hiyo, tunapowazungumza kwa u-general tuwatendee haki baadhi ya Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi ni waadilifu sana na wanaitumikia nchi kwa moyo wa uzalendo sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mwita malizia dakika yako.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mtaalam amezungumza, mimi nimezungumza toka awali hakunisikia, nimesema baadhi, labda Kiswahili cha kikurya hukusikia vizuri. Kwa hiyo, mimi nataka niombe kusema hivi, unajua tunavyozungumza uhalifu wa jambo tunazungumza in terms of average. Kama tuna watu Wakuu wa Mikoa 100 wanaofanya vizuri au kwa mfano sisi Wabunge tuulizwe kwenye Majimbo yetu ni Wabunge wangapi wana miradi iliyoliwa? Wataweza kunyoosha juu Wabunge hapa, miradi ambayo ipo ambayo haitekelezeki ni mingapi? Hivi tujiulize swali, Mtendaji wa Kata akiamka asubuhi anaenda wapi? Ana ratiba gani, Katibu Tarafa anaenda wapi? Tutengeneze utaratibu ambao mtu akiamka asubuhi kama ni mtumishi wa Serikali ana kazi ya kufanya, anaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hilo nataka nikuambie tukitengeneza mfumo mzuri, maana yake Serikali yetu itaenda vizuri. Kila mtu atakuwa anaamka na kitabu tuwe tuna-search umeenda kufanya kazi gani leo? Leo tuna wale maafisa ugani anaweza kuishi Dodoma, anakaa Singida. Tunataka kuwajua asubuhi wanaamka wanaenda wapi? Kazi gani wanafanya? Watoe taarifa ya kila siku wanafanya kazi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti: kwa hiyo, mimi nilikuwa nafikiri kwamba niunge mkono.