Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kasulu Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kupata nafasi hii ya kuchangia bajeti kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza kabisa kwa uzito wake, nipende kuchukua fursa hii, Mwenyekiti jana Mkoani Mwanza kulitokea tukio zuri la kihistoria na la kuenziwa. Mheshimiwa Rais wetu mpendwa alipata muda wa kukaa na vijana wa nchi hii kutoka maeneo mbalimbali Mkoani Mwanza, akaongea nao kwa kirefu sana, lakini alitumia muda wake mwingi kuwaeleza imani kubwa aliyonayo kwa vijana wa nchi hii, lakini fursa ambazo zipo Serikalini, akatutia moyo vijana wa nchi hii lakini akatuhakikishia ulinzi katika harakati zetu zautafuta maisha na kujenga nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kadi nyekundu ilitoka jana pale pale kwa watu ambao walionekana kwamba wanabeza juhudi za vijana za utafutaji. Sasa kwanza nampongeza Mheshimiwa Rais lakini nashawishika kuwaomba vijana wenzangu Tanzania kote, kwamba ni wakati muafaka sasa kama ambavyo tulikuwa tunafanya kuhakikisha kwamba tunamlinda Mheshimiwa Rais wetu na kumtetea katika maeneo yote. Kwenye mitandao, kwenye matukio mbalimbali, tuhakikishe kwamba tunamlinda na kumtetea Rais wetu kwa kuwa anayo maono makubwa sana kuhusu vijana wa nchi hii.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa
MWENYEKITI: Taarifa.
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe Mheshimiwa taarifa sio ombi ni amri kwa vijana. (Makofi)
MHE. VUMA A. HOLLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa naipokea. Vile vile nipende kumshukuru sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita nilipata taarifa kwamba ametupatia Jimbo la Kasulu Vijijini shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za vijijini. Fedha ambazo nimeshajadiliana na meneja wangu wa TARURA kwamba tutachonga barabara ya kutoka Kata ya Kigembe kwenda mpaka Kata ya Rungwe mpya kwenda kufungua maana yake Tarafa ya Buyonga na Tarafa ya Heruchini. Kwa kweli tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hili ninamshukuru sana pia kwa shilingi milioni 600 za Ujenzi wa shule ya sekondari ambazo anatupatia Kasulu Vijijini fedha ambazo tumekubaliana tunakwenda kujenga kwenye Kata ya Karela, kata ambayo ina shule tatu za msingi sasa tunataka kuwapa shule ya sekondari ambayo ni zawadi kutoka kwa Mama Samia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo nipende kumpongeza sana Mheshimiwa Mwigulu na timu yake kwa kazi kubwa ambayo wameifanya ya kuandaa bajeti. Ni bajeti ambayo imeonesha vyanzo mbadala vya mapato ukiachilia mbali ambavyo tumekuwa tukiendelea kubana walipa kodi kwa maana ya watumishi na wafanyabiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumshauri au kumwongezea yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala la watengenezaji wa matrela ya malori haya, mwanzo au miaka ya nyuma kidogo tulikuwa na watengenezaji zaidi ya 10 nchi hii, lakini leo hii wamepungua wamebaki watatu, kama sikosei tunao Super doll, AM sijui na mwingine yupi, lakini ziko kama tatu. Kwa nini wanapungua na hawa wanaweza wakafunga viwanda vyao ni kwa sababu zipo nchi ambazo watu wanaenda kununua huko matrela na kwa nini wanaenda huko?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanakwenda huko kwa sababu manufactures wa huko wa China nadhani kama kama sijakosea na Uturuki, wanapewa export levy na nchi zao asilimia 20 ya FOB. Sasa wanakuwa na uwezo wa kuuza matrela kwa bei ndogo sana, sasa mtu akinunua kule akija kwa bei ndogo, akija hapa Tanzania analipa import duty yaani asilimia 10. Sasa ukiangalia mtu akinunua gari za kutembelea IST kwa mfano, akija hapa Tanzania analipa import duty nadhani asilimia 20 sijui 25. Wakati huyo mtu hana mpinzani, hakuna mtu ambaye anatengeneza magari hapa Tanzania kwa maana IST na gari nyingine, lakini matrela haya ambayo wapo watengenezaji wa Tanzania wapo hapa Tanzania, unashangaa wanatozwa kidogo na hatimaye viwanda vyetu vinaendelea kupata wakati mgumu kwa sababu ushindani wa bei unakuwa ni mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, hapa kuna chanzo kingine cha fedha moja tuongeze import duty kwenye matrela haya iende kuwa sawasawa na gari zingine tu za kawaida za kutembelea angalau asilimia 20. Hii italinda viwanda vyetu na hawa watengenezaji wa ndani na lazima wataongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sio ya kwetu tu yapo mengine mengi matrela ambayo yanapita hapa kwetu kwenda kwenye land locked countries na wenyewe wanalipa asilimia 10 hapo import duty. Kwa hiyo tunayo nafasi ya kungeza fedha, tunayo nafasi ya kulinda viwanda vyetu, tunayo nafasi ya kufanya jambo hili ili kuongeza fedha katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo mwanya mwingine nataka nimshauri Mheshimiwa Mwigulu na timu yake, Kasulu sisi tunao walipa kodi wachache kwa maana ya watumishi ni wachache lakini na wafanyabiashara ni wachache. Hata hivyo, ipo fursa, tulianzisha miaka mitano iliyopita. Sisi kule kwetu baada ya Tanzania kuingia kwenye uchumi wa kati, Watanzania wa Kasulu wale wananchi wa Kasulu hawaendi tena kufanya kazi za mashambani, wanaofanya kazi za vibarua vya mashambani idadi yao imepungua. Sasa pale mara nyingi wanatumia watu kutoka nchi ya jirani ya Burundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu hakuna utaratibu ambao ni rafiki wale watu wanaotoka Burundi wanakuja na ni maarufu wako Kasulu. Ukitafuta data kutoka kwa watu wa Immigration Kasulu watakwambia. Yako maelfu ya watu wanatoka Burundi kuja kufanya kazi za mashambani. Sisi baada ya kuingia uchumi wa kati, lakini pia shule za kata zikajengwa, watu wa Kasulu awanaenda kusoma shule na wakimaliza shule wanaajiriwa, wengine wanajiajiri, wengine wanaenda mikoani kutafuta Maisha. Kwa hiyo ule utaratibu wa watu wa Kasulu kwenda kufanya kazi ya vibarua mashambani umepungua. Kwa hiyo manpower ambayo tunaitegemea sasa hivi ni nchi ya jirani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulianzisha utaratibu, ilikuwa miaka mitatu iliyopita, tukamshauri Waziri wa Mambo ya Ndani tuanzishe kituo kinachoitwa season immigrant pass ambayo akija hapa mtu wa Burundi ataweza kulipia Sh.30,000, aliyemleta atalipa Sh.60,000. Hawa watu ni wengi kuliko wafanyabiashara na watumishi wa Kasulu, hapa kuna fedha nyingi kuliko kodi ambayo tunaikusanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana sana Serikali ilitazame hili kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani. Mchakato ulishaanza nadhani Mheshimiwa Kangi Lugora aliusaini wakati ule, naomba tuuendeleze, kuna fedha nyingi sana hapa kuliko ambazo wanawabana wafanyabiashara. Juzi nimesikia, mpaka wafanyabiashara wamegoma kwa sababu wanakamuliwa Kasulu pale mpaka inakuwa ni too much, wamegoma. Akaenda Kamishna wa TRA kurekebisha mambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, hapa kuna chanzo kingine cha fedha, nyingi sana mamilioni ya shilingi kutoka Wilaya ya Kasulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikumbushe jambo moja tu iko miradi inaendelea kwetu Mradi wa Barabara kutoka Buhigwe-Kasulu, Kasulu kwenda mpaka Nyakanazi. Ule mradi speed yake tunashukuru ipo vizuri, lakini iko miradi ya bonus ambayo tuliambiwa inakuja na hiyo barabara. Kwangu pale tuliahidiwa kujenga hospitali lakini na gari la wagonjwa ambayo ni zaidi ya bilioni mbili na milioni 400.
Ukienda Buhigwe, ukienda Kasulu Mjini wana ya kwao, ukienda Kakonko kwa ndugu yangu Mheshimiwa Kamamba yapo, ukienda Kibondo kwa dada yangu yapo, tunataka hii miradi sasa ianze kuletewa fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iletwe hela kwa sababu tuliambiwa kwamba utekelezaji wa ujenzi wa barabara utaendana na miradi hii ni mabilioni ya shilingi ambayo kama fedha zikitolewa kwa wakati Mkoa wetu wa Kigoma unakwenda kunufaika sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti, ahsante sana.