Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia hotuba hii kwa siku hii ya leo. Awali ya yote kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu aliyenipa nguvu kuweza kusimama hapa kwa heshima ya kipekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe shukrani na pongezi zangu za dhati kwa Rais wetu, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kazi endelee Jemedari mkuu Mheshimiwa Mama Samia kwa jinsi anavyosimamia kuiendesha Serikali yetu hii na leo hii bajeti yake katika Awamu hii ya Sita. Bajeti ambayo imegusa wananchi wote na bajeti ambayo imeakisi na kulenga mambo muhimu yote ya maendeleo ya kila mtu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukubali kwamba lazima tuwe na mbinu yoyote ya kupata kodi ili kuendesha Serikali na kuendesha nchi. Kwa hivyo kuna sehemu itaumauma lakini hakuna nchi inayoendeshwa bila kukusanya kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu leo nataka niunganishe pale Mheshimiwa Rais Jemedari Mkuu Mama Samia alipokwenda kufungua tawi la Benki kuu Tanzania na kuonyesha jinsi nchi yetu inavyotarajiwa kufanya kwa kutumia sekta hii ya kifedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo jambo ambalo limekua likisemwa humu bungeni kwa muda mrefu nalo ni la benki ya Federal Bank of Middle East. Tokea tarehe 8 Mei, 2017, FBME benki ili wekwa chini ya ufilisi kwa DIB deposit insurance board na Benki Kuu ya Tanzania. Leo ni miaka minne na mwezi moja hakuna majibu ya utatuzi kwa suala hili.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wateja wa benki hii hawajapata amana zao Zaidi ya kulipwa shilingi milioni moja na laki tano licha ya ramana yao kuwa kubwa. Uwe na milioni mia mbili, uwe na milioni mia tatu kwa mujibu regulation uwe unalipwa 1500, wafanyakazi licha ya kuwachishwa kazi hawajapata stahiki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi hiki wenye amana mauti imewakuta bila kupata haki zao na familia zao zinaendelea kuteseka. Kwa ruhusa yako naomba niwataje baadhi ya hao waathirika ili Serikali na watu wengine wote wapate kuona jambo na uzito wake; mfano Marehemu Ally Juma Shamuhuna, aliyekuwa Waziri na Naibu waziri kiongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme hili jambo nina interest nalo mimi nausika nalo sana pia. Marehemu Dkt. Maliki Abdallah Juma, alikuwa mkurugenzi mkuu wa wizara ya afya, marehemu Mohamed Toll Suleiman, Marehemu Shaibu na wengine kadhaa na baadhi wengine walio hai sasa hivi wameshafika kustaafu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa ruhusa yako niwataje; Mzee Buruani Sadati ambaye alikuwa Waziri na mshauri katika Ofisi ya Rais ya Dkt. Shein, Dkt. Mohamed Sale Jidawi, Dkt Nafisa Dkt. Mwatima na wengine kadhaa ambao hao wa sasa na wenzao wengi wamestaafu wanategemea amana yao hiyo waliyoweka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Bunge lililopita 2018 walisemea jambo hili mara kadhaa halikupata majibu, Mawaziri, Naibu Mawaziri mpaka Mwanasheria Mkuu lakini bado jambo hili limekwama. Ushauri wangu kwa vile Benki Kuu ndiyo custodian na ndiyo guarantor basi waone namna ya kulimaliza jambo hili. Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Mwanasheria wakutane na makundi ya wadau husika bila kubagua na mbili kutafuta njia bora kuhakiki haki za wadau hawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu chini ya jemedari wetu Samia Suluhu Hassan iweje kulitatua jambo hili, hichi ni kilio akisikie Mheshimiwa Rais kupitia Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ninalotaka kulizungumzia hapa ni hili la suala ya VAT kwenye bidhaa, natoa shukrani sana kwa Serikali kulifanyia kazi jambo hili, kuamua mfumo wa marejesho kama ilivyokuwa zamani. Ombi marejesho yafanywe moja kwa moja baina ya TRA na ZRB kwa sababu wanayo mifumo ya risiti kila mmoja anamuona mwezake, zoezi likifanywa na Hazina patakuwa na urasimu na Hazina zetu Hazina mifumo wanayoonana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nimelifurahia na kweli limetia moyo vijana wetu ni hili la biashara za bodaboda. Ni ukweli usiopingika biashara hii inafanywa na vijana wetu wengi na inawasaidia sana lakini wamekuwa wakipata mkwamo mkubwa katika kufuatia tozo za faini kubwa ya elfu 30, lakini Serikali yetu sikivu imeona na imeweka kiwango kizuri cha Shilingi elfu kumi huu ni uamuzi wa kupongezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ninataka kulisema hapa ni mkopo nafuu kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, Bunge la Kumi na Moja lilitunga sheria kuzitaka Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato kwa ajili ya mikopo nafuu kwa vijana wanawake na watu wenye ulemavu. Ni ukweli usiopingika utaratibu umepunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za ukosefu wa ajira hivyo kuyawezesha makundi haya kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba Halmashauri zote ziongeze usimamizi na udhibiti wa makusanyo na migawanyo yake ili kuhakikisha fedha za mikopo zinawafikia makundi stahiki na mikopo itolewe bila upendeleo. Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI wakae pamoja kuona namna bora ya uratibu wa mikopo hiyo ya makundi maalum lengo la kuhakikisha makundi yanajiendeleza kiuchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine ni nafasi ya taasisi ya OSHA kuchochea uchumi wa viwanda nchini. Kupitia Kamati yetu ya Katiba na Sheria nimeona usimamizi wa afya mahali pa kazi (OSHA) chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na chini ya jemedari anayeendelea kusogea mbele Mheshimiwa Jenista anapambana kweli kweli kazi hapa inafanyika vizuri, mazingira yamekuwa mazuri sana kutokana na ufanisi wa shughuli zao kusimamia mazingira rafiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na michango mizuri ya taasisi ya OSHA bado narudia hoja yangu kwamba kumekuwepo na tatizo la kuwakaimisha watumishi kwa muda mrefu, kwa hivyo niombe ofisi hii ilifanyie kazi watu wasikaimu kwa muda mrefu ili wapate kufanya motisha na ninaamini kwa uhodari wako Mheshimiwa Jenista jambo hilo kwako siyo tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufanisi wa mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF mfuko huu uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kipindi cha miaka mitano tangu ulipoanzishwa 2015 umekuwa mfuko wenye tija kubwa kiuchumi na ustawi wa waajiriwa katika sekta binafsi na sekta ya umma. Mfuko umeonyesha uwezo wa kujiendesha kwa kuendelea kukua kiuchumi kimfumo mwaka hadi mwaka kiasi kwamba mfuko umeipatia Serikali kodi ya Shilingi bilioni 10 kwa mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kufanyia kazi ushauri wa muda mrefu wa Kamati na Wabunge kuhusu michango, mwaka wa fedha inakwenda kupungua endapo waajiri wataanza kuchangia.
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, waajiri wataanza kuchangia 0.6 kwa msingi huo naomba kuunga mkono hoja, nawapongeza Waziri, Naibu Waziri na wote waliochangia katika hotuba hii. (Makofi)