Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
House of Representatives
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia hotuba hii ndani ya Bunge hili Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, aliyenipa uhai na uzima leo hii kuweza kusimama ndani ya Bunge hili la kuweza kuchangia hotuba hii nzuri ambayo ni very participative ambayo imeshirikisha mawazo ya Wabunge wote katika Bunge hili, wale ambao walichangia kwenye hotuba mbalimbali za kisekta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mwananchi, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kwa uwasilishaji wake mzuri wa hotuba hii. Lakini pia nimpongeze Naibu Waziri wake kwa msaada mkubwa sana kwenye uwasilishaji wa hotuba hii. Sambamba na hilo niwapongeze timu yao yote; Makatibu Wakuu na Manaibu wao, kuweza kusaidiana kuweza kuiandaa na kuiwasilisha hotuba hii nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii ni hotuba ya kwanza kwa Serikali hii ya Awamu ya Sita. Nimpongeze mama yetu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama Samia Suluhu Hassan, kwa majibu mengi sana ya Watanzania, hususan wanyonge kupitia hotuba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii imejibu majibu mengi sana, changamoto nyingi sana za wananchi kwenye majimbo yetu kupitia Wabunge wengi ambao walichangia, nikiwemo mimi mwenyewe. Niliweza kuchangia suala la gharama za mizigo inayotoka Zanzibar kuja Bandari ya Dar es Salaam wakati nachangia hotuba ile ya Muungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limepatiwa ufumbuzi, na nimpongeze sana mama yetu, Samia Suluhu Hassan, tuko pamoja. Nawaomba sana wenzangu, Wabunge na wananchi tuendelee kumtakia dua, Mungu amlinde, ampe afya njema ili aendelee kutujengea nchi yetu hii kwa uchumi endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii imebeba dhima kubwa ya uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Hatuwezi kujenga uchumi shindani ambao utakuwa na viwanda na kwa faida ya maendeleo ya watu kama hatujajenga mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza ndani ya nchi yetu. Ukiangalia sasa hivi mazingira yaliyopo hatuwezi kusema kwamba ni mazingira rafiki kwa wawekezaji kuja kuwekeza ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka kuwekeza katika uchumi wa viwanda na uchumi shindani, ni lazima tupunguze suala la riba. Riba kwenye benki zetu ni kubwa, Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na tunampongeza na kumshukuru mama yetu Samia, juzi naye pia amelizungumza jambo hili. Lakini pia Naibu Waziri wakati una-wind up ile hotuba yako ya Wizara ya Fedha ulilizungumza jambo hili na ukasema kwamba mna nia ya kukutana na Benki Kuu pamoja na wadau wote wa benki kuweza kuangalia namna ya kupunguza riba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu ambao tunashindana nao wkenye viwanda riba zao ziko chini. Sisi bado riba yetu iko juu sana. Hatuwezi kwenda kushindana nao kama hatujaweza kuondoa jambo hili, kama hatujaweza kupunguza riba hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la urasimu; wanapokuja investorswaliomo ndani au walioko nje wanaokuja hapa, bado kuna suala la urasimu, mara pale mara hapa mara huku, anapoona hivyo investor anaondoka na fedha zake anakwenda kuwekeza maeneo mengine, nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawaomba sana, tunaiomba sana Serikali, tunaiomba sana Wizara iondoe suala hili. Ikiwezekana basi iweke one stop center ili anapokuja investor basi iwe ni rahisi kwake kufuata zile procedures za kinchi na kuweza kuwekeza. Wanapowekeza hawa wanatuletea faida nyingi sana kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la malighafi. Viwanda hivi ambavyo vinawekezwa ni lazima viwe na malighafi ya kutosha. Ni lazima twende kama Serikali tukawaelimishe na kuwahamasisha wananchi, hususan katika suala la kilimo maana malighafi nyingi zinatokana na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunaomba sana Serikali ijiwekeze kwenye kuwawezesha na kuwajengea mazingira bora na rafiki, hususan vijana, kwenda kwenye sekta ya kilimo na kujiandaa kwenye malighafi za viwanda hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uchumi wa buluu (blue economy). Kule Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwenye hotuba yake ile ya fedha ya mara hii, amejielekeza katika uchumi wa buluu. Na hii ndiyo agenda kubwa sana kule Zanzibar.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana jambo hili tulibebe kwa sababu bahari ndilo eneo kubwa sana ambalo limezunguka ndani ya nchi yetu. Naomba sana tuwe na dhamira thabiti ya kuliendea suala hili la uchumi wa buluu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwenye bajeti kuna target ya kununua meli nne zinazokwenda kwenye deep sea. Naomba sana jambo hili tulianze kwa kutenga fedha zetu za ndani, tusitegemee misaada kutoka nje kuja kutuletea meli hizi, tuanze sisi. Mimi naamini kwamba kwa dhamira ya Serikali tuna uwezo wa kufanya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeweza kununua ndege 11, tunashindwaje sisi wenyewe kununua meli za kwenda kwenye deep sea. Naamini kama tuna dhamira kweli ya dhati ya kwenda kwenye uchumi wa buluu, hatuwezi kushindwa kununua meli zetu sisi wenyewe na kwenda kwenye uchumi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa matumizi ya fedha; hapa tunajadili matumizi haya ya fedha, tunajadili kupitisha bajeti hizi, lakini jambo kubwa sana ambalo tunalipitisha halitaonakana na maana kama hatuendi kusimamia fedha hizi ambazo tunazipitisha hapa. Nashauri kwamba kuwe na chombo cha tathmini na ufuatiliaji, Wizara ya Fedha iwe na chombo hiki ambacho kinaifuatilia miradi yote wakati wa utekelezwaji wake ili kuona kwamba fedha hizi tunazozipitisha zinakwenda kuzingatia nidhamu ya fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maana kuna vitu viwili tofauti; kuna nidhamu ya fedha, lakini kuna namna ya kuweza kuitumia fedha kwa mujibu wa taratibu na sheria. Watu wetu wa procurement walioko huko kwenye maofisi wanajaribu kutumia sheria na taratibu lakini hawazingatii nidhamu ya matumizi ya fedha. Naomba sana Serikali twende tukazingatie nidhamu ya matumizi haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwenye maofisi unaweza ukakuta kwa mfano kitu cha kununua 500 kimenunuliwa shilingi 1,500, mara tatu au nne ya bei halisi. Tunaomba sana twende tukazingatie nidhamu ya fedha na thamani halisi ya fedha hii ambayo tunaipitisha. Tutakapofanya hivyo, naamini tutapiga maendeleo kwa hatua kubwa zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba atakapokuja Waziri hapa anipe ufafanuzi kuhusu jambo la punguzo hili la PAYE kwa wafanyakazi. Kule Zanzibar wafanyakazi wa Muungano ambao wanafanya kazi kule mapato yale yanakwenda kwenye Serikali ya Zanzibar. Hata hivyo tunaona kwamba hakuna utofauti baina ya mwaka jana na mwaka huu; mwaka jana tulipeleka kule bilioni 21, ikiwa ni PAYE za wafanyakazi wa Muungano walioko kule, lakini mwaka huu pia tunaona kima ni kilekile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza, na hapa naomba pia nipate ufafanuzi, kwamba je, wafanyakazi kwa maana ya watumishi wa Muungano, kule Zanzibar hawajaongezeka? Au hawapandi madaraja, au labda kima cha mshahara hakipandi? Tatizo hasa ni nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba mwaka jana ni bilioni 21, lakini hata mwaka huu ni bilioni zilezile 21; tatizo hapa ni kiyu gani. Je, zimebakia pale kwa sababu ya punguzo la asilimia moja au tatizo ni lipi? Naomba pia hapa atakapokuja Waziri atupe ufafanuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri sana Serikali na Wizara za Muungano na zile ambazo siyo za Muungano ziendelee kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja. Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamahuri ya Muungano tukifanya kazi kwa pamoja naamini tutapunguza gap kubwa sana la maendeleo katika maeneo yetu haya mawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano yapo maeneo ambayo Tanzania Bara yako juu lakini kule Zanzibar bado wapo chini, lakini kuna maeneo ambayo kule Zanzibar tumepiga hatua lakini huku bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kule Zanzibar tuna posho za wazee, huku bado jambo lile halijatekelezeka. Kwa hiyo tukishirikiana naamini tunaweza tukapeana mawili matatu tukajua kwamba na huku tunaweza kulitekeleza jambo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la gharama za kuunganisha, huku ni…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Bakar kwa mchango wako mzuri.
MHE. BAKAR HAMAD BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, ahsante sana.