Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mikumi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya bajeti na ninaomba niaze kwa kuchangia bajeti kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa yale yote ambayo yametokea tangu Bunge hili lilipoanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia niishukuru Serikali ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ambayo ameifanya katika kipindi hiki kifupi lakini kubwa kuliko yote ni kuendelea kutunza imani ya Watanzania kwa Chama cha Mapinduzi, kutunza imani ya Watanzania kwa Serikali yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamefanywa katika kipindi hiki kifupi lakini kwa uchache suala la kupeleka fedha za ujenzi wa miundombinu ya shule hasa maabara na kuongeza vyumba vya madarasa katika Halmashauri mbalimbali wananchi wa wanashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia upelekaji wa shilingi milioni 500 kwa kila Jimbo kimsingi imeweza kwenda kujibu kero nyingi hasa za miundombinu ya barabara na Mikumi tumeamua kupeleka milioni hizi 500 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto wa Ruhembe, mto ambao umeuwa watu wengi, wananchi wengi katika lile eneo lakini ni daraja ambalo kimsingi ni la kimkakati katika uzalishaji wa miwa na usafirishaji katika kiwanda cha Illovo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja hili linaenda kupunguza gharama ya uzalishaji kwa wakulima pia usafirishaji wa mazao yao kutoka mashambani katika Kata za Mikumi, Kidodi, Ruhembe, Ruaha na hata vidunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hotuba nzuri ya bajeti ambayo imejaa ubunifu mkubwa lakini pia inaongozwa na uzalendo wa hali ya juu, hotuba ambayo imechukua maoni ya Wabunge kikamilifu ni hotuba ya bajeti imeonesha uzalendo katika kulinda viwanda vyetu vya ndani na bidhaa ambazo zinazalishwa na viwanda vyetu vya ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupunguza tozo na kodi mbalimbali hili siyo tu kwamba linavutia wawekezaji kuja kuzalishia hapa ndani lakini linaenda kuongeza ajira na linaenda kuamsha uwekezaji wa ndani na hivyo kuboresha uchumi wetu katika namna mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii pia kuipongeza Serikali kwa ubunifu na kubuni njia bora zaidi ambazo hazimsumbui mwananchi lakini ni katika kuongeza tax base hasa kupitia kukusanya kodi ya majengo na viwanja kupitia simu lakini pia kupitia LUKU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya principal za kodi ni kupunguza gharama ya ukusanyaji pia kuongeza kiasi cha ukusanyaji, shida kubwa ya makusanyo yetu ya kodi ni kwamba tunatumia gharama kubwa kukusanya kodi ndogo lakini pia kumsumbua yule mlipa kodi kiasi ambacho mlipa kodi anatakiwa kutumia mara nyingine shilingi 5,000 ama Shilingi 10,000 kwa ajili ya kwenda kulipa shilingi 7,000.
Kwa hiyo, hali hii inapelekea wananchi wetu wengi kutojitoa kikamilifu katika kutimiza majukumu yao ya kiraia hasa katika eneo hili la kulipa kodi. Kwa ubunifu huu naamini kabisa wananchi watajitoa kimasomaso katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika kutimiza wajibu wao wa kizalendo katika kulipa kodi ambayo ndiyo msingi wa ujenzi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii pia kuishukuru Serikali kwa maamuzi ya upanuzi wa kiwanda cha sukari cha Kilombero, upanuzi huu siyo kwamba unaenda kutatua tatizo la soko la miwa kwa wakulima wa Kilombero, unaenda kutatua tatizo la sukari katika nchi yetu ya Tanzania. Uwekezaji huu mkubwa ambao haujapata kutokea katika ukanda huu wa Afrika siyo tu ni mfano wa kuigwa kwa sababu unaenda kuongeza ajira ya wananchi wetu lakini unaenda kupanua soko la ajira la vijana wetu ambao wanamaliza shule hawana kazi ya kufanya ama ajira ambayo ina tija. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linaenda kuongeza kipato cha vijana wetu lakini inaenda kuwawezesha wananchi wetu uwezo wao wa kuweka akiba ambayo inaweza kuwasaidia katika kuwekeza katika maeneo mbalimbali na hivyo kupambana na jitihada za kupiga vita umaskini, haya yote yatachochea uchumi wetu ili ukuwe kwa kasi, hata hivyo naomba maboresho machache yafanyike:
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; wananchi wetu hasa wa pembezoni siyo tu wanatumia simu kama chombo cha mawasiliano lakini kwao ni muhimu sana, wengi siyo kwamba wanatumia kwa sababu wana fedha, kwa hiyo hii tozo kwa wananchi naomba tuwe na kima cha chini. Kwa mfano, unaweza kusema mwananchi yoyote consumption yake ama matumizi yake ya simu hayazidi shilingi 5,000 huyo hatakiwi kutozwa, lakini zaidi ya 5000 pengine ndiyo atozwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili litasaidia sana wananchi wetu hasa wenye kipato cha chini kuendelea kuhamasika kutumia mawasiliano kwa ajili ya jitihada za kupambana na hali yao. Pia naomba Wizara ya Fedha iangalie njia bora za kupanua wigo wa kodi (tax base) katika kuangalia haya makampuni ambayo yanafanya biashara kimtandao wanaita e-commerce. Biashara nyingi sasa hivi zimeamia katika mfumo wa biashara mtandao, biashara hizi zinafanywa kwa kiasi kikubwa lakini hatujui VAT wanalipia wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni makubwa yanafanya biashara hizi za mitandaoni tunaona Amazon, tunaona Alibaba na wengine, mtu anaponunua bidhaa kutoka kwenye makampuni haya VAT analipa wapi, lakini hata corporate tax inaenda wapi? Nani anatoza? Kama tunaweza kuangalia eneo hili tunaweza kuongeza uwezo wetu mkubwa wa ukusanyaji wa kodi na hivyo ku-contribute katika miradi yetu ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nizungumzie Tanzania kwa Geografia lakini kwa historia hegemonic power, hegemonic power katika ukanda wetu, lakini hegemonic power katika siasa za Afrika. Ni wakati sasa umefika kwa Serikali yetu, Wizara zetu kuzungumza kwa pamoja kuangalia nafasi yetu, influence yetu katika Ukanda wa Maziwa Makuu lakini katka Ukanda wa Kusini na Bara zima la Afrika. Katika hilo tuangalie ushiriki wetu katika mashirika ya Kikanda Kama SADC, kama East Afrika, Cooperation lakini pia katika African Union. Je, nafasi yetu ni ile ile kama tumelegalega ni wapi? Nini kifanyike ili Tanzania irudi katika nafasi yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili ni lazima tutumie fedha, Wizara ya Fedha lazima tushirikiane na Wizara ya Mambo ya Nje kuhakikisha kwamba zile business center ambazo tulikuwa nazo lazima zirudi na tuzitangaze kikweli kweli. Pia tusitengemee sana watumishi wa Mambo ya Nje katika Balozi zetu kunadi vivutio vyetu, kunadi sekta mbalimbali za uwekezaji. Wakati umefika sasa wa kampuni mashirika na taasisi nyingine kuanza kuajiri watu wao na kuwa station katika Balozi zetu, Wizara ya Mambo ya Nje iwe ni coordinator ama mratibu wa hawa watu kutoka Bodi ya Utalii na kituo cha uwekezaji lakini pia Taasisi mbalimbali ambazo zinapaswa kutangazwa huko nje. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ilivyo sasa wanadiplomasia wetu ambao wanaenda kwenye Balozi zetu ndiyo tunawatumia kufanya kazi zote ikiwemo kutanganza utalii wetu kitu ambacho naamini tumeona matokeo yake na hatuhitaji mwalimu wa kutueleza wapi ambapo tumeangukia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia kilimo ni uti wa mgongo na Bunge hili limejipa jukumu la ajenda la kufanya mapinduzi ya Kilimo. Kilimo hiki ambacho tunasema ni uti wa mgongo tunakichukulia poa kwa kiasi kikubwa, kilimo ni sayansi na kilimo kinagusa kuanzia natural, social na hata economics na ndiyo maana uwezi kuzungumzia uzalishaji bila kuzungumzia kilimo. Nimshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumteua ndugu yetu Prof. Mkenda kuwa Waziri wa Kilimo, yeye ni Mchumi na kwa sababu kilimo ni uchumi basi tunaamini kabisa anaenda kufanya mageuzi makubwa na mapinduzi katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona ni jinsi gani kilimo chetu bado hatujakitendea haki kwa sababu hata sera zetu za maliasili, sera zetu za ardhi, za uwekezaji bado zinaji- contradict unapozungumzia sera yetu ya kilimo. Kwa hiyo nilikuwa naomba kuwe na mafungamano kati ya sekta ya kilimo na sekta nyingine, tatizo hapa unakuta ile concept ya ceteris paribus kwa Wachumi, ambayo inaanzia kuangalia kilimo na kuangalia uchumi wetu kutokea kwenye jicho la viwanda na huduma. Lile linatuonesha ni jinsi gani tunakosea ni lazima hiyo concept ya ceteris paribus ianzie kuangalia kilimo na kuangalia kwa sababu kilimo ni uzalishaji lakini kilimo kinaenda mpaka kwenye ulaji. Tuangalie sheria zetu zinaangalia vipi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unaweza kuona kwamba hata mikopo ya benki inatolewa katika rate ambazo mtu anatakiwa kulipa kila mwezi, mkulima wa miwa ambaye anavuna kwa season anawezaje kulipa kila mwezi? Lakini mkulima huyu ukimwambia alipe baada ya msimu wa mauzo anaweza akafanya. Unaweza ukampa mortgage ya nyumba unaweza ukampa mortgage ya mashine na anaweza akatumia vitu hivyo na akalipa kwa msimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja nashukuru sana (Makofi)