Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Edwin Enosy Swalle

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lupembe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa ajili ya nafasi ya kuchangia bajeti hii muhimu sana ya Serikali. Nianze kwa kunukuu maneno ambayo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameyasema kwenye ukurasa ule wa 116 wakati akiwasilisha bajeti yake ndani ya Bunge lako Tukufu. Pengine kabla sijanukuu maneno hayo, niseme tu kwamba napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Nchi yetu, Samia Suluhu Hassan. Pia nawapongeza sana Waziri wetu wa Fedha, Naibu wake pamoja na timu nzima ya Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza, kwanza kwa kusikiliza maoni ya Waheshimiwa Wabunge, lakini pia nawapongeza sana kwa sababu wamekuwa ni wasikivu na kujibu kilio cha wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepitia bajeti hii, ukiitazama sura nzima inaakisi kauli mbiu ya Rais wetu, kwamba kazi iendelee. Hii ni kwa sababu bajeti hii ya kwanza imezingatia kuendeleza miradi yote mikubwa ambayo ndiyo imekuwa moyo wa Watanzania katika kupata maendeleo yao. Kwa hiyo kauli mbiu ya kazi iendelee imeakisiwa vizuri sana katika hotuba hii ya Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaendelea kwenye ukurasa wa 116, Mheshimiwa Waziri alisema, naomba kumnukuu: “Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais amenituma niwahakikishie Watanzania kupitia hotuba hii kuwa, tunaendelea kuijenga nchi, ije mvua, lije jua, tunaendelea kuijenga nchi, uwe usiku au mchana, tunaendelea kuijenga nchi.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Lupembe, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba sisi wananchi wa Jimbo la Lupembe, iwe usiku, iwe mchana, tutaendelea kumuunga mkono kwa kazi nzuri ambayo ameanza kuifanya inayoleta matumaini makubwa sana kwa Watanzania wa nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Lupembe wamenituma nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwamba zile milioni 500 kwa ajili ya barabara za vijijini zimewafikia na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya Wizara hii kuhusu kutoza fedha kwenye mafuta kwa ajili ya barabara za vijijini, wananchi wa Jimbo la Lupembe wanayo matumaini makubwa, kwamba barabara ambazo kwa muda mrefu zimekuwa na shida; Barabara kama ya Nyombo – Ikuna – Kichiwa – Mtwango – Welela sasa itakwenda kupata ufumbuzi. Pia barabara ambayo imekuwa na kero ya muda mrefu ya kutoka Ninga – Lima – Ikondo, kwa bajeti hii itakwenda kupata ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo machache ambayo nataka sasa niishauri Wizara hii. Sehemu ya kwanza ni kuhusu sehemu ya TRA. Nilizungumza na Mheshimiwa Waziri wiki mbili zilizopita, kwamba wananchi wa Mkoa wa Njombe, hasa wajasiriamali wadogo wa biashara ya mbao kumekuwa na biashara kubwa sana kwenye biashara ya miti ya mbao. Siyo Njombe tu, mikoa mingi ya Nyanda za Juu Kusini kumekuwa na kero kubwa kwa wasafirishaji wa biashara ya mbao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa, nilimwambia Waziri hapa, kwamba kumekuwa na hitaji la kisheria la watu ambao wanafanya biashara ya mbao kusajiliwa kwenye VAT. Mfanyabiashara wa mbao akisajiliwa kwenye VAT anakwenda kununua mbao kwa wakulima wadogowadogo kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yuko babu yangu, au mtu ambaye ana msitu, ameufuga kwa zaidi ya miaka kumi, anauza mbao mara moja tu kwa miaka kumi au 15, lakini kwa mujibu wa sheria hii, inamtaka huyu mkulima mdogo anavyouza huo msitu wa mbao awe na mashine ya EFD. Kwa hiyo huyu mfanyabiashara aliyesajiliwa kwenye VAT akienda kwa yule mwananchi wa kule chini hana risiti ya EFD.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafsiri yake hapa ni nini? Kumekuwa na udanganyifu mkubwa wa wafanyabiashara na kukwepa kodi ya Serikali. Pia Maafisa wa TRA ambao siyo waaminifu wamejenga mazingira ya kuchukua fedha kwa wafanyabiashara wa mbao. Kwa hiyo biashara ya mbao Mkoani Njombe imeshuka na baadhi ya wafanyabiashara wameamua kuacha kabisa hii biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, nilimwomba Waziri na leo namwomba tena, tukimaliza Bunge hili la Bajeti afike Mkoani Njombe akazungumze na wafanyabiashara hawa ili kutatua changamoto ya VAT na biashara ya mbao ambayo kimsingi imekuwa na shida sana. Wafanyabiashara wako tayari kulipa kodi lakini wanahitaji uwekwe mfumo mzuri ambao utakadiriwa na wakajua kwamba ukipakia mbao kiasi fulani, malipo yake ni kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kuishauri Serikali ni kuhusu elimu kwa mlipakodi. Nimesoma kwenye bajeti hii kuna suala ambalo halijasemwa vizuri. Makamu wa Rais akiwa Waziri wa Fedha aliongea ndani ya Bunge hili kwamba alipokwenda kugombea jimboni aligundua wananchi wengi ni maskini na aligundua kuna ukwepaji mkubwa sana wa kodi na ubadhirifu wa fedha za umma kwenye miradi ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hajawa Makamu wa Rais, aliahidi Bunge hili kwamba angetoa elimu kwa Wabunge tujue mianya ya upotevu wa fedha za umma. Naomba nimshauri Waziri; kwa sababu ahadi hii aliitoa Makamu wa Rais wa sasa, namwomba sana Mheshimiwa Waziri atoe semina kwa Wabunge na Madiwani ambao ni wasimamizi wa shughuli za maendeleo kwenye majimbo haya, wapate semina kujua mianya ya ubadhirifu wa fedha za umma kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana kudhibiti upotevu wa fedha ambao Serikali kwa siku za karibuni wanapeleka fedha nyingi sana kwenye halmashauri, lakini bila kuwa na usimamizi fedha hizi zitakwenda kupotea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu ambalo napenda kusema ni kwamba, naishukuru sana pia Serikali kwa kutupia macho Mradi wa Liganga na Mchuchuma kule Njombe. Ninachomwomba Waziri wa Fedha, kwa kuwa Rais ameonesha mwelekeo wa mradi huu ukamilike mapema, Mkoa wa Njombe hauna uwanja wa ndege, na nilishauri kwenye mpango wa Serikali kwamba ni vizuri vipaumbele vya Serikali vikaendana na maeneo muhimu ambayo Serikali imekusudia kuweka fedha nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Mkoa wa Njombe ambao sasa unafungua uchumi mkubwa kwenye Mradi wa Liganga na Mchuchuma na ule mkoa una biashara kubwa ya matunda ya parachichi na ni mkoa wa tatu kwa uchumi nchini, hauna uwanja wa ndege. Kwa hiyo namwomba sana Waziri kwenye bajeti yake hii basi aendelee kutazama maeneo ambayo kuna mambo mengi ya kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo naomba pia kulisema ni kuhusu suala zima la kuwasaidia wananchi kuwa na uelewa wa kudai risiti baada ya kupata huduma. Siku za karibuni kumekuwa na kujisahau kwa Watanzania wengi kudai risiti. Ukienda kwenye sheli sasa hivi, sheli nyingi hawatoi risiti kwa wanaoweka mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo namwomba sana Mheshimiwa Waziri, pamoja na bajeti hii kuwa nzuri ni vizuri akajielekeza kutoa elimu kwa Watanzania ili wajue kodi wanayolipa ndiyo kodi ambayo inawafanya wao kupata maji safi na salama; kodi wanayolipa wanapata elimu bora; kodi wanayolipa ndiyo wanapata maji na kadhalika. Bila kutoa elimu hii kwa Watanzania wakawa sehemu ya kusimamia uchangiaji wa fedha hizi hakutakuwa na maana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata Waheshimiwa Wabunge sisi kama sehemu ya kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi ni vizuri pia tukawa na sehemu kubwa ya kuwaelimisha wananchi wetu waone furaha kulipa kodi kwa sababu kodi ni maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)