Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Kwanza na mimi naungana na wenzangu kukupongeza sana kwa kuaminiwa na kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuipongeza Wizara kwa hotuba yao nzuri. Katika kuwapongeza pia nitawakumbusha baadhi ya mambo yanayohusu Jimbo langu la Sengerema lakini pia nitaomba maombi katika baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nina ombi langu la muda mrefu, naikumbusha Wizara, naamini watendaji wa Wizara pia wako hapa wanasikiliza. Wilaya ya Sengerema tuna Hospitali Teule ambayo kimsingi inamilikiwa na watu binafisi, ni Shirika la Kidini la Roman Catholic lakini ndiyo hiyo hiyo hospitali ambayo imekuwa ikisaidia wananchi wa Sengerema na maeneo mengine yanayozunguka eneo letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku zote nimekuwa nikikumbusha na leo nakumbusha tena kwa mara nyingine na naamini nitapata majibu sahihi leo kwamba formula inayotumika pale kutoa ruzuku ya Serikali ambao ni utataribu wa kawaida ina-base kwenye vitanda 150 lakini leo hii hospitali ile ina uwezo wa kutoa huduma kwa wagonjwa kwa kuzingatia uwezo wa sasa wa vitanda zaidi ya 375. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu liko Wizarani, naamini Katibu Mkuu yupo anaelewa, ambacho namuomba Mheshimiwa Waziri pamoja na Mheshimiwa Naibu Waziri, wakati wanatoa majumuisho ya ufafanuzi wa hoja zao kesho basi hoja hiyo ya ombi letu la Sengerema ambalo ni ombi la muda mrefu walitolee majibu. Hospitali ya Sengerema kwa kweli inasaidia Wilaya nyingi zilizoko upande wa Magharibi mwa Mkoa wa Mwanza, kwa hiyo, naomba nipate ufafanuzi kuhusu ongezeko la ruzuku kwenye Hospitali Teule ya Sengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na Waheshimiwa Wabunge wenzangu walioshauri kwamba Bohari ya Dawa ifungue maduka yake katika kila Hospitali za Wilaya. Tunafahamu juhudi zinazofanywa katika Hospitali za Rufaa pamoja na Mikoa, lakini haitoshi. Inawezekana kabisa kwamba changamoto yake ni kwenye bajeti lakini kama nilivyoshauri wakati nachangia Ofisi ya Rais na kama Wabunge wengine walivyoshauri, mafungu haya bado hatujaridhia, eneo hili la huduma ya afya ni muhimu sana, usambazaji wa dawa ni mojawapo ya jambo muhimu sana katika uendelezaji wa Taifa letu. Tungependa kuona huduma hii inawasogelea zaidi wananchi hasa katika hospitali za Wilaya. Tuangalie namna ambavyo tunaweza kurekebisha bajeti zetu tukawezesha hii Bohari ya Dawa kupitia Wizara ya Afya tuwasogezee wananchi huduma katika kufungua maduka ya dawa katika hospitali zetu za Wilaya. Hilo ni jambo la pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilikuwa nasoma hotuba ya Wizara, uko ukurasa umeelezea Hospitali za Kikanda hasa za rufaa, nadhani ukurasa wa 52, wameelezea mambo mengi. Nina ombi hapa, Taifa kwa muda wote limekuwa linajitahidi sana kujenga hospitali za rufaa kikanda kurahisisha huduma kwa kusaidiana na sekta binafisi na hasa masharika ya dini. Nafahamu zipo hospitali kubwa ambazo zina hadhi ya rufaa ambazo zinamilikiwa na makampuni ama mashirika binafisi. Hata hivyo, bado Serikali pia haijawahi kusimamia juhudi zake za kufungua hospitali kubwa za rufaa zinazomilikiwa na Serikali. Ombi langu kwa Wizara ya Afya izingatie na itafakari upya mwelekeo wa ufunguaji wa hospitali za rufaa. Ombi langu naloliweka mbele ya Bunge lako Tukufu ni ujenzi wa hospitali inayomilikiwa na Serikali yenye hadhi ya rufaa katika Kanda ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ukurasa wa 52 hapa utaona zipo kanda ambazo zimeainishwa zingine zina mikoa miwili, sitaki kusema hizi zenye mikoa miwili zidharauliwe, hapana! Ninachotaka kusisitiza pamoja na kwamba Kanda ya Ziwa tuna hospitali inayoitwa Hospitali ya Bugando kwa kweli imezidiwa. Sisi tunaotoka kule tunafahamu huduma zilizoko pale sasa hivi, sitaki kuwabeza juhudi wanazozifanya wauguzi na madaktari waliopo pale, lakini kimsingi wamezidiwa. Hii ndiyo Kanda ambayo ina mikoa mingi zaidi lakini ina hospitali moja tu ya rufaa ambayo kwa kweli kwa mazingira tuliyo nayo sasa hivi haimudu na haikidhi! Huko nyuma tulishatoa ombi hili na tukaahidiwa kwamba Serikali ilikuwa inatafakari kujenga Hospitali ya Rufaa katika Kanda ya Ziwa. Tunaomba sana Serikali kupitia Wizara hii itafakari na baadaye mtupe maelekeo na matumaini tunakoelekea ni wapi. Uwezekano wa kujenga Hospitali ya Rufaa kwa Kanda ya Ziwa upo au haupo? Hilo ni jambo moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kushauri na kwa kweli ni kwa kuzingatia hali halisi tu ilivyo ni kuhusu hizi huduma za wazee. Tunaona juhudi za Serikali zinafanyika, madawati ya wazee yamefunguliwa kwa kila Hospitali ya Wilaya lakini jambo hili linahitaji ufuatiliaji wa makini. Nashukuru mmesema sasa hivi kutakuwa na madawati ya kutoa taarifa lakini sisi tulioko site tunafahamu, kama alivyosema Mheshimiwa Shabiby na Waheshimiwa wengine, kwa kweli madawati yale yamekuwa kama vile ya kutoa huduma za vipimo na kuandikiwa tu ambacho wewe kinakusibu maana wazee wakifika pale mara nyingi hawapati dawa. Naomba jambo hili tuliangalie kwa umakini na kwa macho mawili ili kuimarisha huduma za afya kwa wazee. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri sisi wote tuliopo hapa hata kama siyo wazee ni wazee watarajiwa tu, ndiyo nature ilivyo tutafika hatua hiyo, kwa hiyo, naomba sana wazee wetu tuwazingatie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, naishukuru sana Wizara, Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pia Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Ummy ameniahidi kwamba baada ya bajeti hii atafika Wilaya ya Sengerema, tunamkaribisha sana. Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, miezi miwili iliyopita alikuwa Sengerema tunamshukuru sana kwa juhudi zake alizofanya. Tunaomba tena msichoke kuwazungukia wananchi kwa sababu kadri mnavyofika ndivyo mnavyoimarisha utoaji wa huduma zinazotakiwa katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.