Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyamba
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nichangie hoja iliyopo mezani kwetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaifanya, niwapongeze wasaidizi wake; Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango na Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa kazi nzuri ambayo anaifanya. Na tumeona jinsi anavyoshughulika kwenye sekta mbalimbali; kilimo, elimu, madini na shughuli zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nitumie nafasi hii kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango, kaka yangu, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba na Naibu wake, Mheshimiwa Eng. Masauni, kwa kazi nzuri wanayoifanya. Watu hawa wamedhihirisha wazi kwamba ni wasikivu, na ni watu ambao wanafikika na wanapokea ushauri ambao wanapewa.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwapongeze watendaji wa Wizara hii, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu. Lakini vilevile kipekee, nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Wajumbe kwa kuja na ushauri na maoni ambayo yatasaidia katika uboreshaji wa bajeti yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa kujielekeza kwenye usimamizi, ufuatiliaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Kwanza nianze kuipongeza Wizara kwa kasi kubwa ya kupeleka fedha kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hii imejidhihirisha wazi kwa sababu zimepelekwa fedha, milioni 500, kwa ajili ya TARURA. Lakini vilevile kuna ongezeko kubwa la fedha ambazo zitakwenda baadaye kwenye TARURA. Kuna fedha za ukarabati na fedha za maboma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu ni kwamba hizi fedha sasa ni nyingi, na kusimamia miradi hii kutoka Dodoma hatuwezi kufanikiwa. Ushauri wangu ni kwamba tuimarishe sekretarieti za mikoa. Nimpongeze dada yangu, Mheshimiwa Ummy, kwa wazo la kuimarisha sekretarieti za mikoa. Ni wazi kwamba tukiimarisha sekretarieti za mikoa watafanya ufuatiliaji kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na miradi yetu itatekelezwa kwa uhakika.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ikiwezekana marekebisho ya sheria yafanywe; ile Sheria yetu ya Tawala za Mikoa (Regional Administration Act) Na. 19 ya mwaka 1997, sheria zile za Serikali za Mitaa na Sheria ya Utumishi. Kwa sababu kwa sasa hivi Katibu Tawala wa Mkoa ni mamlaka ya nidhamu kwa watendaji waliopo kwenye regional secretariat, anapokwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa hawezi kumgusa mtendaji yeyote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaweza tukarekebisha sheria hizo ili kuhakikisha tuna usimamizi imara katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na hivyo kusababisha usimamizi imara katika miradi yetu ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa pili unahusu mradi wa Liganga na Mchuchuma. Nitumie nafasi hii kumpongeza Rais kwa maelekezo yake aliyotoa hivi karibuni akiwa ziarani Mwanza. Rais ameelekeza mambo makubwa mawili; kwanza kupunguza urasimu, na pili, kuondoa vikwazo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ninaomba ninukuu; “Tumeimba toka nikiwa Waziri, mpaka leo nimefika hapa nilipo Mchuchuma na Liganga haijatoa matunda.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa maelekezo haya. Mradi huu ni mkubwa na ni kichocheo cha maendeleo kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na mikoa ya kusini. Mradi huu ukitekelezwa utaongeza kasi ya mahitaji ya ujenzi wa reli kwa kiwango cha SGR kutoka Mtwara kwenda Mbambabay. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, ile dhana sasa ya Mtwara Corridoe itaonekana. Na utaongeza matumizi ya Bandari ya Mtwara; hapa imeonekana kwamba Bandari ya Mtwara sasa hivi matumizi yake ni machache, lakini Bandari ya Mtwara umefanyika uwekezaji mkubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, una bilioni 157 zimewekezwa pale; una mitambo ya kisasa; vilevile sasa hivi inaweza kuhudumia metric tons milioni moja, lakini mizigo pale ni michache. Mradi wa Liganga na Mchuchuma ukianza kutekelezwa basi Bandari yetu ya Mtwara itatumika ipasavyo na hivyo kuongeza uchumi wa wana Mtwara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kodi ya VAT na ushuru wa bidhaa wa vifungashio na mashine za kufungashia korosho na karanga. Sekta ya ubanguaji wa korosho bado ni changa, inahitaji kuendelezwa. Na kuna changamoto nyingi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tunabangua asilimia 20 tu ya korosho ambayo tunazalisha, tunauza korosho ghafi asilimia 80. Maana yake ni nini; tunapeleka ajira kwa wenzetu. Kama tukibangua korosho kwa asilimia kubwa ina maana tunazalisha ajira, lakini tunaongeza thamani ya korosho yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa pamoja na kushushwa kodi katika maeneo mbalimbali, kuna sehemu ndugu yangu, Waziri wa Fedha, naomba uiangalie tena. Kuna mashine za kufungashia korosho ambayo ni HS Code 8422300; kuna vifungashio SH Code 3923210; hivi mmevisahau na matokeo yake wabanguaji wadogo wanapata vifungashio kwa shilingi 3,000 mpaka 3,500. Tukitoa VAT kuna uwezekano kabisa wabanguaji wadogo watanunua vifungashio hivi kwa shilingi 600. Na hivyo itaongeza uwezo wetu wa kubangua kwa makundi ya vijana na akina mama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba sana kwamba VAT iondolewe katika maeneo hayo ili kukuza sekta yetu ya ubanguaji na hatimaye tuuze nje korosho zilizobanguliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la export levy kwenye korosho. Ni matarajio yangu kwamba wakati wa majumuisho Waziri wa Fedha na Mipango atakuja kutuambia kwamba nini kitafanyika katika export levy. Na hapa lengo kubwa ni kuchukua sehemu ya export levy kwenye korosho tupeleke kwenye sekta ya korosho. Tutoe motisha kwa wabanguaji, lakini vilevile itafute pembejeo kwa wakulima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo haya maeneo mawili; incentive kwa wabanguaji na upatikanaji wa pembejeo za kutosha, utasaidia kusukuma au kuendeleza sekta ya korosho ambayo sasa hivi kwa miaka minne uzalishaji unaendelea kupungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema pale awali, vilevile ubanguaji wetu tunabangua asilimia 20 tu ya kile ambacho tunazalisha. Kwa hiyo namuomba Waziri wa Fedha wakati anafanya majumuisho aliangalie hili na atueleze waziwazi kwamba sehemu ya export levy itapelekwa kwenye sekta ya korosho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu yangu ya mwisho ni suala na Madiwani na Udiwani. Mheshimiwa Waziri wa Fedha amezungumza vizuri kabisa, kwamba Madiwani ni Wabunge katika kata zetu. Madiwani wanafanya kazi nyingi, wana changamoto nyingi na wanafanya kazi zetu nyingi wakati sisi Wabunge hatupo majimboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa kuamua kulipa posho kutoka Hazina. Lakini bado kuna kazi ya kufanya hebu tukiangalie kile anachokipata Diwani. Kama kweli ni Mbunge wa kata tumuongezee maslahi yake, tuongeze posho yake ili aweze kutekeleza majukumu yake vizuri, ili aweze kufanya kazi yake vizuri. Asiwe ombaomba kwa wakuu wa idara, asiwe mnyonge kwa mkurugenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kukiwa na Madiwani dhaifu kutakuwa na halmashauri dhaifu, tukiwa na Madiwani imara tutakuwa na halmashauri imara. Kwa hiyo, naomba, uamuzi wa kupia posho zao kutoka Hazina ni mzuri lakini twende mbele zaidi tuangalie kile kinachotoka Hazina ni shilingi ngapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Madiwani wengi baada ya kuingia kwenye Udiwani wamepata mikopo kama tulivyofanya sisi Wabunge. Kwa hiyo, Madiwani sasa hivi wanapata kitu kidogo sana. naomba turekebishe ili na wao ukifika mwisho wa mwezi wawe na appetite ya kuangalia kwamba nini kilichopo kwenye akaunti zao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo tutawahamasisha Madiwani, watakuwa madhubuti, wataweza kuwa na ujasiri wa kuwahoji watendaji na kumsimamia mkurugenzi. Lakini tukiwa na Madiwani ambao vipato vyao ni vidogo, hawana kipato cha kutosha, watakuwa dhaifu na hivyo wao watakuwa kazi yao ni kuitikia kile ambacho kimewasilishwa na wakurugenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)