Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye Bajeti ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais tunasema ameanza vizuri mno. Huku mtaani kauli ni kwamba Mheshimiwa Rais anaupiga mwingi, kule kwetu tunasema Mheshimiwa Rais ameanza na mguu wa kutoka na mguu wa kutoka Mtume ameuombea. Mambo mengi ya awali kabisa ambayo Mheshimiwa Rais ameanza kuyafanya yanatupa imani kwamba nchi ipo kwenye mikono salama na sasa Mama ndiyo ameshika usukani na tunako elekea kunatupa matumaini makubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, milioni 500 kwa kila Jimbo kwa ajili ya TARURA zimefika hata Wilayani Muheza na Mimi na Engineer wangu wa TARURA Engineer Kahoza pale tumeshajadiliana ziende zikatengeneze barabara zipi tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupandishwa madaraja kwa wafanyakazi na ahadi ya ongezeko la mishahara mwakani najua wafanyakazi wanalisubiri hili sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue nafasi hii kumpongeza Kaka yangu Comrade Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, Waziri wa Fedha na Mipango, Naibu Waziri Injinia Hamad Masauni, Katibu Mkuu na Wasaidizi wao kwenye Wizara ya Fedha kwa bajeti hii, bajeti iliyonyooka, bajeti yenye matumaini makubwa na ambayo inaonyesha kwamba Wizara ya Fedha na nchi kwa ujumla ipo pia kwenye mikono salama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kusema kweli Comrade Mwigulu ningependa kulisema hili huku namuangalia usoni huku mtaani tunasema hana baya, anafanya vitu vyote, majukumu yote anayoyafanya kwa usahihi mkubwa, shida yake inakuja tu anapoanza mambo yake ya Yanga. Yaani najua amejizuia kwelikweli kutoweka japo Bilioni Tano kwenye hii bajeti kwa ajili ya kuisaidia Yanga kuwa bingwa mwakani, lakini ndiyo hivyo tusingekubali. Nimpe pongezi sana Comrade Mwigulu na naamini kwamba hata namna zake za ukusanyaji wa mapato ambazo amezipanga unaona kabisa bajeti yetu safari hii inaenda kutekeleza kwa zaidi ya asilimia 67.9, ambapo bajeti iliyopita ilitekeleza kwa vile inaonyesha kwamba kasungura kake katakua kakubwa safari hii. Nimpongeze kwa mara nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina machache tu ya kuweka kwenye bajeti hii kwa vile kama nilivyosema bajeti imetimia kusema ukweli, lakini ningeweza kuongezea hakuna ziada mbovu waswahili wanasema na la kwangu ninalotaka kuliweka ni kuhusiana na mifuko yetu ya uwezeshaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa tovuti ya uwezeshaji tunayo mifuko 45 ya uwezeshaji. Hakuna namna tukawa na mifuko 45 na majukumu yake yasiingiliane kwa namna moja ama nyingine. Kuna mifuko ambayo kazi zake zitakuwa zinagongana na kwa namna hiyo inaipunguzia ufanisi na inatupunguzia pia uwezo wa kui-monitor kwa kadri ambavyo tulitakiwa tufanye. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, najua kwamba kuna mchakato wa kuunganisha baadhi ya mifuko maoni yangu ni kwamba mchakato huu uongezewe nguvu na ufanywe kwa makusudi makubwa kabisa mifuko mingi zaidi iunganishwe ili mradi tuwe na mifuko michache ambayo tunaweza kuisimamia, pia ambayo tutahakikisha kwamba ufanisi wake unakuwa wa kiwango cha juu kama lengo la kuanzishwa kwake lilivyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya mifuko hii 45 hatuna hata mfuko mmoja wa ubia venture fund ambacho kimsingi tuna mifuko ya dhamana kwanza hakuna taarifa za kutosha kuhusu uwepo wake, takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia 30 tu ya wananchi wanaufahamu kuhusu mingi ya mifuko hii kati ya mifuko hii 45. Kwa hivyo, haifanyi kazi yake na kuna mifuko ambayo inafikisha mpaka mwaka mzima haijaweka fedha popote na inachofanya ni kuweka fedha benki ili ku-play safe isipate hasara, sasa hili siyo lengo hasa la kuanzishwa kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna biashara nyingi huku kwenye field uraiani ambazo kimsingi zinachohitaji siyo tu kupewa mikopo na ikusanywe baadaye, lakini kinachotakiwa hasa ni uwezeshwaji wa moja kwa moja. Biashara nyingi zinafanywa na wajasiriamali ambao hawana kweli ufahamu wa kutosha kuhusiana na biashara na tunaishia tu kwenye kukopesha vijana kwa kutumia mifuko ya Halmashauri, lakini wanafanya miradi ya boda boda na miradi ya kuku na unapata malalamiko mengi kuhusiana na ufanisi wa mifuko hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sijawahi kukaa siku tatu kwenye Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Muheza na nisikutane na malalamiko, mawili ndiyo yanakuja sana either kwamba mifuko hii haijawafikia watu wengi wanakuja watu wengi ambao wametekekeleza vigezo vyote lakini wanashindwa kupata mkopo kwa sababu sasa ukiwa na milioni 200 ambazo unatakiwa kuwakopesha makundi yote haya matatu unawakopesha vijana wangapi kati ya wananchi takribani 300,000 wa Wilaya nzima ya Muheza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusiana na wanaopata mikopo hii lakini wanashindwa kuirejesha na hii inatokana na uwezo mdogo wa namna ya kuwekeza kwa hiyo unakutana na kwamba…

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, kengele ni ya kwanza?

NAIBU SPIKA: Ni kengele ya kwanza.

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, unakutana na suala kwamba Mkurugenzi wa Halmashauri anamshtaki raia kijana kutoka Wilayani kwako kwa vile wameshindwa kufanya marejesho sasa unakaa katikati unataka marejesho yafanyike ili watu wengine zaidi wafaidike na mikopo hii, lakini juu ya yote hutaki mwananchi wako apelekwe mahakamani kwa kukosa kurejesha mikopo. Kwa hiyo, unakuta upo mahali kama mwanasiasa, kama mtumishi wa wananchi ngoma yako inakuwa ngumu, kwa vile lengo la mikopo hii ikafanye kazi iliyokusudiwa, lakini irejeshwe, lakini kwa sababu hatuna upeo wa kutosha kuhusiana na biashara tunazotaka kuzifanya inaishia kupotea hewani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki mbili zilizopita nilimsikia ndugu yangu Waziri Patrobass Katambi anasema Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa imetoa shilingi bilioni 4.9 na kati ya hizo zilizorejeshwa ni shilingi milioni 700 peke yake, bilioni 4.2 imepotea hewani, hakulisema lakini nina wasiwasi hata yeye anaamini hiyo hela haitarudi na kazi ya Serikali ni kuhudumia wananchi wake, sasa utashindana na wananchi kwenda nao mahakamani kila wakati mpaka lini? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maoni yangu ni kwamba sasa ni wakati wa kuzihusisha taasisi binafsi za fedha zitusaidie kufanya jukumu hili badala ya kuwakopesha tu na kukusanya mikopo hii kwa wananchi sasa tunachotakiwa kwenda kufanya ni kuwashirikisha kwa kuwa na ubia kati ya Serikali, taasisi binafsi za fedha na wananchi hawa wajasiriamali ili kuhakikisha kwamba mikopo hii, haiwi ni mikopo lakini inakuwa ni uwezeshaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara nyingi kwa mfano za Katani kule Kigombe, Ngomeni, Pande, Darajani, Wilayani Muheza hata ukiziambia zirudishwe baada ya mwaka mmoja zinakuwa bado hazijakomaa sawasawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Katani inaanza kuvunwa baada ya miaka mitatu unampa mtu mkopo ambao anatakiwa kurudisha baada ya miezi kadhaa anazipata wapi, inabidi atoe kati ya hizo hizo kuanza kufanya marejesho. Kwa hiyo tukiwa na venture fund zitasaidia kwa sababu tunachoenda kufanya sasa inakuwa ni kuwekeza kwa pamoja kati ya Serikali, taasisi hizi binafsi za fedha na wajasiriliamali wale wadogo na marejesho yake yanaenda kupanua zaidi mifuko yetu hii na itasaidia watu wengi zaidi kuliko ambavyo inafanya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili halitoki tu hewani lipo katika SME Policy ya nchi yetu ya mwaka 2003 na nchi ambayo inafanya vizuri mifuko hii kwa ubia ni Ghana na Ghana walipata sera hii kutoka kwetu, sasa sisi tuliandika lakini hatujawahi kuifanyia kazi wenzetu wameichukua na inafanya kazi sawa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha, naomba niseme kwamba naunga mkono hotuba ya bajeti ya Waziri Mwigulu na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)