Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Same Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuzungumza machache kutokana na bajeti yetu hii. Nitazungumza masuala matatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, bajeti ya kilimo ya mwaka huu kwanza ni ndogo. Kilimo kinachangia asilimia 85 ya kazi ambazo Watanzania wamejiajiri. Kilimo hiki kwenye pato la Taifa kinachangia asilimia 26.9 lakini kimetengewa kwenye bajeti asilimia 0.8. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba hizi shilingi milioni 500 kwa kila jimbo zitasaidia kutengeneza barabara za TARURA na hivyo kutoa mazao kwenye maeneo mbalimbali kupeleka kwenye soko. Kwa hiyo, hiyo nayo imechangia kwenye kilimo. Vilevile natambua kwamba tuna miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inahitaji fedha nyingi, ndiyo maana pengine bajeti ya kilimo ni ndogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nashauri kwamba baada ya bajeti hii, kwa sababu hii tunaipitisha na imeshapita, ni kwamba mwaka kesho Waziri wa Fedha na Waziri wa Kilimo waweze kukaa mapema na kuangalia umuhimu wa kuendeleza sekta ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuimarisha skimu mbalimbali zile za umwagiliaji na kukarabati ambazo zipo. Tunahitaji takribani shilingi trilioni moja kwa miaka mitatu mfululizo kwa ajili ya kukarabati na kujenga skimu mbalimbali za umwagiliaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tukumbuke na tukubali kwamba miundombinu ya umwagiliaji na miundombinu ya barabara zetu ni sawa kwa sababu food security inategemea kuwepo kwa chakula na chakula kile lazima kitokane na irrigation. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa alitoa waraka kwamba District Cess ambayo inakusanywa kwenye Halmashauri, asilimia 20 irudi kwenye kilimo, lakini tumekaa muda mrefu, haijawahi kutekelezwa. Kwa hiyo, nilikuwa namwomba Mheshimiwa Waziri kipindi hiki iweze kuwekwa kwenye Finance Bill ili angalau asilimia 20 ya makusanyo yanayokusanywa kutokana na kodi ya mazao basi irudi kwenye kilimo kuliko kumkamua ng’ombe bila kumpa majani, anaweza akafa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nature ya kilimo inahusisha pia masuala ya utafiti ambapo tunatakiwa tutoe fedha mapema. Fedha zote hizi zikitoka, shilingi bilioni 294, basi itasaidia sana katika kuhakikisha kwamba tunaandaa masuala ya kilimo ambayo yanahitaji maandalizi ya haraka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili katika bajeti hii ambalo nilitaka nizungumzie ni sera ya fedha. Serikali kama ilivyo kawaida, haifanyi biashara, lakini BoT inawabana Watanzania. Inawabana wafanyabiashara kutoweza kufanya biashara kwa kutosha kabisa kupitia mabenki ya biashara. Wanabana namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kama nilivyosema, sekta binafsi ndiyo engine ya kuendeleza uchumi, lakini Benki Kuu inabana mabenki ya biashara kwa kusababisha ukwasi, matatizo ya ukwasi. Mabenki ya biashara hayana fedha za kukopesha wafanyabiashara na Watanzania ili waweze kufanyabiashara pamoja na kulipa kodi za Serikali. Sasa yanasababisha matatizo ya ukwasi namna gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanzoni Serikali na taasisi zake zilikuwa zinaweka fedha zake kwenye mabenki ya biashara, lakini sasa hivi fedha zile zinalipwa moja kwa moja kwenye Benki Kuu ambapo mabenki ya biashara yanakosa fedha za kukopesha wafanyabiashara wadogo. La pili, hati fungani ambazo Serikali inakopa, inatoa riba kubwa sana kiasi ambacho mabenki ya biashara yanashindwa kufanya biashara ya fixed deposit. Kwa hiyo, watu wanakimbilia kwenye hati fungani kufanyabiashara na Serikali badala ya kufanya biashara na mabenki ya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuna riba kubwa sana ambapo wananchi na wafanyabiashara wanalipa mabenki ya biashara. Hii inatokana na kwamba Benki Kuu inapokopesha mabenki ya biashara inawatoza riba kubwa. Sasa hivi inawatoza asilimia 6.5 na mabenki ya biashara na yenyewe yanatoza asilimia 20; iwe ni mortgage au biashara nyingine yeyote, lakini ni asilimia 20. Sasa cha kufanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kushauri yafuatayo: La kwanza uwekwe utaratibu ili Serikali iweze kupitishia fedha zake kwenye mabenki ya biashara kusudi kuwe na fedha za kutosha za kukopesha watu ili wafanye biashara na waweze kulipa kodi ili tuweze kufikia shilingi trilioni 22 ambazo tunatakiwa tuzilipe kupitia kwenye kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Benki Kuu ishushe riba zake inapokopesha mabenki ya biashara kusudi na mabenki yale yaweze kushusha riba yanapohudumia wafanyabiashara. Lingine ni kwamba, kwenye hizi hati fungani tunaomba kabisa Serikali kupitia Benki Kuu pia washushe riba angalau ifikie asilimia 10 kusudi mabenki yaweze kukopesha, kuchukua fedha za wafanyabiashara kwa fixed deposit na wenyewe angalau waweke asilimia kidogo. La sivyo tutakuwa tumeshaua kabisa kabisa, tutapunguza uchumi wetu. Kwa sababu sasa hivi kusema ukweli tuko kwenye middle income economy lakini tusipolinda uchumi huu, itafika pahala ambapo tunarudi kule kule kwenye umasikini mkubwa kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha aweze kuongea na mabenki ya biashara ili waweze kufungua matawi mbalimbali ya mabenki huko mikoani kwa sababu mabenki mengi yamefungua matawi mengi Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Moshi pamoja na Mbeya wakati mikoa mingine yote haina mabenki kama hayo. Hiyo ingesaidia kupunguza gharama kwa sababu wakopeshaji wangekuwa ni wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, sera za BoT ziangaliwe. Sasa hivi sera zilizopo ni za kunyanyapaa vijana. Vijana kila wanapotaka kukopa wanaambiwa uwe na nyumba, uwe na landed property. Sasa vijana wataweza wapi kupata landed property ili waweze kukopa? Kwa hiyo, hilo nalo liangaliwe kusudi vijana waweze kukopa na waweze kuendelea na biashara vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu, ningependa kuzungumza suala la Sera ya bajeti lakini kwa ushauri, bajeti hii ni nzuri na tunaipitisha kwa asilimia 100 lakini ningependa kushauri mambo machache yafuatavyo; jambo la kwanza suala lilikuwa linaathiri sana bajeti zetu ni matumizi ya dharula ambayo hayakupitishwa na Bunge, tunaiomba Serikali ijitahidi sana sana isiwe na matumizi ya dharura ambayo yanaathiri bajeti zetu ambazo zimetengwa na Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala lingine ni kwamba labda tufanye utafiti kwa sababu nimeangalia hapa kuanzia mwaka 2005 mpaka leo kuna fedha zinazotengwa na Bunge na zile zinazotolewa kwenye mawizara inafikia tu asilimia 58 mpaka asilimia 67. Nadhani tuangalie inawezekana labda tuna over estimate bajeti zetu halafu tunashindwa kufikia malengo kutokana na uwezo wetu wa kukusanya kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwamba tunaomba Serikali iangalie athari za COVID au UVIKO-19 ili tuweze kusaidia baadhi ya biashara ambazo zimekuwa affected kwa mfano mabiashara ya mahotel ambayo pengine yangeweza kusamehewa baadhi ya kodi ili waweze kusimama kwa sababu wamekua affected sana sana na huu ugonjwa wa corona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuona faida ya miradi mikubwa ya kimkakati lazima tuhakikishe kwamba tunaimaliza mapema tuweze kuona faida yake na iweze kusaidia kujenga uchumi kupitia miradi mingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwamba Serikali iweze kulipa ihakiki madeni ya ndani na iweze kuyalipa ili tuweze kuongeza mzunguko wa fedha na wananchi waweze kuendelea na biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi naunga mkono hoja.