Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. CHARLES J. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango wa kuchangia kwa kuzungumza katika Bunge lako Tukufu kupitia maandishi narejea na kuendelea kuchangia Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza awali msisitizo wangu ni juu ya njia na shughuli zinazoweza kutuongezea mapato ya kutekeleza bajeti yetu na kuendeleza Taifa letu kwa ujumla. Fursa ya kuongeza mapato kwa kuuza bidhaa nje zilizoagizwa kutoka nje na kuongezwa thamani hapa au kuuzwa nchi nyingine kama zilivyo maarufu kama re-export. Bidhaa ya kwanza ni mafuta jamii ya petroli. Katika historia ya biashara ya mafuta kuna wakati makampuni, watu binafsi na idara za Serikali toka nchi jirani walikuwa wanakuja Dar es Salaam kununua mafuta na kuyasafirisha kwa njia ya malori au na mabehewa ya treni. Matumizi ya mfumo huu ni kuwa kampuni ya Tanzania inapo re-export Taifa linafaidika na lile ongezeko katika bei (mark up) ambayo huongeza faida ya kampuni husika na hatimaye kutozwa kodi na tozo nyinginezo kwa manufaa ya Taifa. Lakini uwepo wa utaratibu huu ulioratibiwa vizuri huwezesha Taifa kuwa na hifadhi kubwa ya mafuta bila kuilipia ambayo inapelekea kuwa na mafuta mengi ya kimkakati (strategic stock).

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu huu utawavutia na kuwafunga wateja wa nchi lengwa kwa kuwa na uhakika wa kupata mafuta kwa bei inayojulikana toka kwao, lakini pia uwepo wa volume kubwa ya mafuta toka hapa kwenda nchi jirani itaongeza matumizi ya mafuta (fuel for truck use on safari) yaliyolipiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nifafanue kidogo dhana ya mafuta yaliyolipiwa, mafuta yanayotumiwa na malori yanayokwenda nje ya nchi (transit) au re-export shughuli zake huleta pesa za kigeni ambazo huchangia kununua mafuta mengine. Kwa mafuta yanayotumika nchini wingi au ongezeko lake linaweza kuwa na tija pale inapopelekea kutafuta fedha za kigeni kuagiza mafuta mengine. Ikumbukwe kuwa tuna mahitaji ya kununua mafuta kama bidhaa muhimu na mafuta jamii ya petroli ndiyo bidhaa ya kwanza kuchukua fedha zetu adimu za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, jinsi ya kuchota fursa hii ni kwanza kujipanga kuisimamia ili kuepuka watu wasio waadilifu kuitumia vibaya kwa manufaa yao/kuifisadi. Hili zaidi ni jukumu la TRA na idara zake wakisaidiwa na vyombo na taasisi nyingine za dola. Utaratibu huu ulikuwepo ila kwa kushindwa kuusimamia basi zikatungwa sheria zilizoua fursa hii. Sasa tunao vijana wengi wenye elimu wanaweza kupewa ujuzi na stadi za kusimamia sekta hii na kwa faida ya matumizi ya teknolojia tukachangamsha sekta hii na kupata mapato ya Serikali .

Pili ni kuruhusu hifadhi ya mafuta ya forodha iliyozuiliwa (bonded customs warehouses/terminals). Kama nilivyodokeza mafuta yaliyoko katika hifadhi za namna hii yanahamasisha kampuni husika kuagiza mafuta mengi kwani hawawajibiki kulipa kodi na tozo mara moja, lakini kwa upande wa nchi stock hizi ni kinga ya kiusalama kwani nchi inakuwa na haki ya kwanza kuyatumia inapotokea tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, fursa nyingine inayofanana karibu na hiyo ni hifadhi ya mafuta inayoelea (floating stock). Tanzania tunayo fursa ya kufanya biashara hii kwa kuruhusu sekta binafsi kujenga matanki makubwa ya kuhifadhi mafuta nchini kwa lengo la kuuza mafuta hayo popote duniani. Kimsingi mafuta yanayotunzwa katika hifadhi hizi huwa yananyumbulika kufuata bei za soko la dunia. Faida kwa nchi ni kodi na tozo kwa uwekezaji, huduma za bandari na haki ya kuwa mteja wa kwanza. Biashara ya namna hii iliwahi kufanyika kwenye maji ya bahari ya Tanzania kwa kutumia mtindo wa meli mama na mtoto (mother daughter vessels). Chini ya utaratibu huo na kutokana na ukosefu wa matenki makubwa na sheria” za nchi yetu, meli kubwa zenye ujazo wa kati ya tani 150,000 mpaka 200,000 hutinga nanga kwenye maji ya Tanzania ambapo hufaulisha mafuta kwenye meli za ujazo wa tani 40,000. Shughuli hii kulingana mwenendo wa bahari ya Hindi inaweza kufanyika Tanzania usawa wa Tanga-Bagamoyo na Zanzibar kwa usawa wote wa chini ya Jangwa la Sahara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mafuta ipo fursa ya kuboresha mfumo wa bei elekezi ili kuchota faida kubwa itokanayo na kushuka na kupanda kwa bei za mafuta kwenye soko la dunia (backwardation - contango). Busara yake ni rahisi kuelezeka, bei katika soko la dunia inaposhuka na hapa nchini bei ikashuka kwenye vituo vya mafuta nauli au bei ya bidhaa huwa haishuki. Hii ina maana mlaji wa mwisho hafaidiki mara nyingi na anguko kubwa la bei ya mafuta. Lakini mafuta yanapoanza kupanda na bei elekezi ikaonesha bei ya mafuta kuwa juu kwa kutegemea huo mzigo mpya walaji hawafaidiki endapo kuna stock kubwa ya zamani. Lakini soko la Tanzania kulingana na sheria na taratibu zetu hatuna mipango na mikakati ya kuchota na kuhifadhi mafuta yenye bei nafuu katika mazingira ambayo wazi inaonesha kuwa muda si mrefu bei itapanda. Yote haya yanaweza kufanyika kirahisi kwa kuweka sheria na mazingirra ya kuvutia uwekezani wa namna hiyo kupitia sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie fursa nyingine ya re-export kwa bidhaa zingine zisizo mafuta jamii ya petroli.

Kwanza nieleze kuwa viwanda vya mafuta ya kupikia na ngano vilivyoko nchi za jirani ikiwemo Rwanda, Burundi na hata Uganda vilijengwa huko baada ya wawekezaji waliokuwa wakitumia viwanda vilivyoko Tanzania kushindwa kuhudumia masoko hayo kutoka kwetu. Yote hayo yalitokana na sheria na usimamizi usiowezesha kufanya biashara ya aina hiyo toka Tanzania. Tathimini ya biashara hii itakuonesha kuwa kuna fursa kubwa sana tukijenga sekta hii kwa lengo la kutengeneza ajira, kupata kodi na kuchangamsha uchumi. Kuna wakati re-export kwenda nchi jirani ilifikia dola milioni 840 kwa mwaka lakini kati ya mwaka 2015 mpaka 2020 kiasi cha juu ni dola milioni 340.7 na kiwango cha chini ni dola milioni 143.16 mwaka 2017. Ni imani yangu kuwa kwa kuweka mazingira mazuri re-export value inaweza kufikia dola biilioni 1.5 kwa mwaka katika miaka mitatu ijayo. Hii ni sekta ya re-export, si mauzo ya bidhaa nje (export).

Mheshimiwa Naibu Spika, shughuli nyingine inayoendana na re-export na ambayo inaweza kuchangamsha uchumi kwa kutengeneza ajira na kupanua wigo wa walipa kodi ni vituo vya biashara hapa nchini, kwa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na zile zinazotoka nje ya nchi, kwa mfano, soko la Kariakoo kabla ya kuanguka kutokana na sheria na udhibiti. Ni kweli yalikuwepo mapungufu katika biashara hiyo ambayo pamoja na kuzalisha ajira kwa kiasi kikubwa kulikuwepo mianya ya kukwepa kodi, bidhaa hafifu na bidhaa za bei ndogo zinazoathiri viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hapa ni kuwa mapungufu yanaweza kurekebishwa na faida za kuwa na masoko kama hayo zikaweza kuchotwa kwa manufaa ya Taifa. Mfano wa wazi ni Kariakoo ya Kampala, Uganda iliyoanzishwa baada ya kudorora kwa Kariakoo mwenye jina. Wafanyabiashara kutoka Malawi, Congo, Zambia na kwetu Tanzania wananunua bidhaa Kariakoo Kampala. Hapa kuna hoja tatu, ajira, kodi na kuchangamsha jamii. Ajira inatangulia kodi lakini mwenye ajira analipa kodi iwe moja kwa moja au indirect. Eneo hili liangaliwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni uhamasishaji wa mauzo nje (export). Kama nilivyoeleza kwenye mchango wangu kwa kuzungumza Tanzania mwaka 2019 tuliuza nje bidhaa zenye thamani ya bilioni 2.9 pesa ya Marekani na 2/3 ikiwa ni dhababu lakini fursa ya mauzo nje (potential export) yetu ni bilioni 2.37 pesa ya Marekani bila kuhesabu dhahabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja hapa ni fursa zilizowazi ambazo tunaweza kuzitumia na kuongeza mauzo nje. Nieleze wazi hapa kuwa kama Taifa lazima tutembee na lengo letu la kuuza bidhaa nje kwani pamoja na kuleta pesa za kigeni linatuhakikishia soko la bidhaa zetu na kuleta ustahimilifu wa sekta zetu za uzalishaji nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bidhaa/mazao 19 niliyoyarejea sikuona nyama au ng’ombe hai, maziwa, mawese, maharage aina ya soya kwa kutaja baadhi. Uchambuzi wa haraka ni labda watakwimu walichukua bidhaa ambazo zina fursa zaidi ya dola milioni 20.8 kwa mwaka. Hoja yangu ni kuwa iweje nchi yenye fursa ya kufuga tushindwe kuzalisha nyama bora na maziwa kutosheleza soko la ndani na kuuza nje? Iweje Uganda na Botswana wafanye vizuri kwenye sekta hizi kuzidi nchi yetu yenye ardhi na uwanda mzuri wa kufuga ng’ombe. Hili ni eneo muhimu la kuwekeza kwani mbali ya fursa ya kuuza nje sekta hizi zinasaidia kujenga uchumi jumuishi jambo muhimu katika Taifa lenye amani na mshikamano. Pia kwa mazao ya shamba kama mawese au mafuta ya mawese ambayo kimsingi yana soko kubwa DR-Congo na tunakuwa na faida ya kuwa karibu na soko kwani yanalimwa mikoa ya Magharibi, ni muhimu tuongeze jitihada za kuhamasisha sekta hii kuliko tunavyofanya sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, jibu hapa ni kualika sekta binafsi kushirikiana na wananchi kwanza kwa kuhakikisha wanalima mashamba makubwa kwa uwiano wa familia, lakini mwekezaji anayeweza kujenga kiwanda kikubwa kitakachofanyakazi kwa tija kubwa. China wametupa nafasi ya kuuza maharage aina ya soya tani milioni 42 kwa mwaka kwa bei ya shilingi 3,000 kwa kilo ni takribani mauzo ya shilingi trilioni 126. Kiasi ni kikubwa sana hata ingekuwa ni mauzo ya miaka kumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni kuwa kwanza Serikali ihakikishe mkataba huu unalindwa, pili lazima iwepo mipango na mikakati ya kuhudumia soko kwa kukidhi viwango vya soko kwa faida kwa wazalishaji. Tatu, ni kuhakikisha wananchi kwa matabaka yote wanashirikishwa hasa kwa kusaidiwa kuingia kwenye mnyororo huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya mazao ya soya ni vizuri tukaielewa kwa ujazo na uzito wake. Tanzania kwa ujumla wake tunazalisha vyakula vya aina zote tani million 19, soya tu ni tani milioni 42; huu ndio ukubwa wa jukumu tulilonalo. Hii ni fursa kubwa na nzito na inahitaji nguvu ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni kuwa kwa kuuza nje (export & re-export) kwa kiasi kikubwa tutapata fedha nyingi za kigeni lakini kujenga uhakika wa soko hali itakayochochea sekta za uzalishaji hapa nchini kuzalisha zaidi. Mchakato wa uzalishaji utasaidia kutengeneza ajira, kuzalisha bidhaa, kusaidia kukusanya mapato ya Serikali kwa maendeleo na kuchangamsha uchumi. Pamoja na bajeti hii kama ilivyowasilishwa, tunaweza kufikia mapendekezo haya kwa kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji tukirekebisha sheria na taratibu za utendaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nihitimishe kwa kushauri juu ya usimamiaji wa zuio la sukari la asilimia 15 kwenye sukari ya viwandani na hiyo VAT refund. Nakubaliana na Serikali kwa kukubali kuondoa hiyo 15% kwenye sukari ya viwandani lakini lazima Serikali iendelee na taratibu za kusimamia sukari hiyo. Hupo uwezekano wa sukari ya mezani kuingizwa na kuuzwa kama sukari ya viwandani. Sukari aina hii iratibiwe kwa kuwa na customs bonded rooms kwenye viwanda vikubwa na kwa wawekezaji wadogo iwepo bonded warehouse ya ujumla. Naomba na kushauri wazo la kurudisha kiwango hiki lisifikiriwe kwani madhara yake kwenye sekta ya viwanda hatutakaa tuyamalize makali yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado Serikali haijatamka juu ya kikwazo kikubwa cha uendeshaji wa viwanda na uwekezaji kwa ujumla. TRA wawe wazi kubainisha stahili ya PMG - VAT revenue na stahiki ya CG TRA - VAT expenditure. Kama awali tunapopokea VAT au kuratibu VAT ni vema tujue yapi ni mapato ya Serikali na kiasi gani kitarejeshwa kwa mfanyabiashara. Vipo viwanda vya Tanzania vimeshindwa kuzalisha na kuuza masoko ya nje kutokana na mapungufu yetu katika kusimamia VAT refund.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.