Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Korogwe Vijijini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kutoa neno la ahsante na vilevile sitafanya vizuri kama sitawashukuru Wabunge wote wa Chama cha Mapinduzi kwa kuniamini na kunichagua kuwa Mjumbe wa NEC. Nataka niwaambie, siendi kufuata riziki, naenda kuwatetea ninyi wana-CCM wenzangu, hakuna kukatwa Mbunge wa aina yeyote. Niko tayari kutoa chozi la mwisho kwa ajili ya ninyi Wabunge kuwatetea kule. Tulikuwa tunafanywa kama wanyonge lakini nataka niwaahidi, siendi kwa ajili ya biashara, naenda kwa ajili ya kuwatetea ninyi ndugu zangu Wabunge, Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nianze kuwashukuru wapiga kura wangu kwa kuniamini. Pamoja na kwamba nilikuwa nafanya kazi katika mazingira magumu, nilikuwa naumwa lakini waliniamini na leo hii nimekuwa mwakilishi wao tena, naomba Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwa Mheshimiwa Waziri wa Afya, Naibu Waziri wake pamoja na Naibu Waziri wa TAMISEMI. Nawashukuru sana kwa kazi nzuri mnayoifanya. Usiposhukuru kwa kidogo, hata kikubwa ukipewa hutashukuru. Nawashukuru kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri na Wizara yake wameweza kuja kwenye Jimbo la Mkoa wa Tanga mara chungu nzima na kujua kero za wananchi na wakaamua kuzifanyia ufumbuzi wake. Mungu awabariki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niwashukuru sana viongozi wa Wizara ya Afya; bila ninyi Wizara ya Afya, leo hii hapa ndani ya Bunge hili asingekuwepo Stephen Ngonyani, mlinitetea sana, mkanipeleka India na leo nimerudi. Pamoja na kwamba naumwa, lakini Wizara ya Afya ni Wizara mama sana, inatakiwa tuiangalie kwa macho yote. Mungu awabariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vitu ambavyo vinatakiwa viangaliwe kwa macho yote ni Wizara ya Afya. Kwa nini nasema hivyo? Kwa sababu Wizara ya Afya, hata kama utakuwa unafanya kazi ya aina yoyote, bila kuwa na afya njema hakuna chochote cha maana ambacho utaweza kufanikiwa nacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza Serikali, zile hospitali za Mtwara, Tarime na Dar es Salaam ambazo hazijakwisha, kwanza itengwe pesa ili Serikali ihakikishe zile zahanati au vituo vya afya au hospitali zinakwisha, kwa sababu tutaendelea kujenga hospitali nyingi lakini ziko ambazo wananchi wenyewe waliamua kuzianzisha, lakini hospitali hizo zimefika ukingoni, hazipati msaada wa aina yoyote, hasa kule kwa ndugu yangu Mheshimiwa Matiko, naomba ziangaliwe sana ni vitu muhimu sana hivyo. (Makofi)
Ndugu zangu, kumekuwa kuna mchezo hapa, ambapo mtu akishaanza kuchangia anataka kujifananisha na Waganga wa Kienyeji. Why!
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za nyuma hapa nataka niwaambie ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, hakukuwa na hospitali hata moja; mlikuwa mnatumia tiba asili, tiba mbadala. Leo hii kila atakayefanya makosa; jana Askari Polisi, hapa Askari wa Magereza na Askari wa Jeshi mmewafananisha kwamba wakikosa kazi watakuwa Waganga wa Kienyeji. Hii ni biashara kweli mnafanya hapa? Ndicho kilichowaleta kuchangia! jaribuni kubadilisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Uganga wa Kienyeji ni fani kama fani nyingine. Msiwaweke Waganga kama ni watu dhaifu sana. Niliyeko hapa nina hospitali Nairobi. Hulazimishwi kumtibu mtu. Mtu anakuja kwa kupenda kwake. Ninyi mnakuja kututolea mifano hapa! Wakati wa uchaguzi mpo milangoni kwetu! Inakuaje? Wakati wa uchaguzi mko milangoni kwetu, leo hapa mnakuwa ndio watu wa kuwatolea mifano Waganga wa Kienyeji, kwa nini! (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, msiwadharau watu ambao usiku mko majumbani kwao. Nashangaa! Mimi ni Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili, Tiba Mbadala Tanzania. Hatuwezi kukaa hata siku moja tukaja kusema ni namna gani tunaweza kutatua tatizo la tiba asili, tiba mbadala! Badala ya kutaja kwamba hospitali zenu zinakosa dawa, ninyi mnaona fani kutaja Waganga wa Kienyeji. Inawasaidia? Hivi ninyi hakuna aliyekwenda kutibiwa hapa! Msiseme haya mambo ya kininii hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuanzia leo, msitufananishe. Mkichangia, changieni hoja zenu. Msiwafananishe watu ambao usiku mko majumbani kwao mnakwenda kutibiwa. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yamepita jamani, yamepita. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina hospitali nyingi sana ambazo zinahitaji zipatiwe upembuzi na tiba. Leo hii kuna matatizo ambayo yanakwenda katika mahospitali. Kuna hospitali nyingi Madaktari wenyewe wanafanya kazi katika mazingira magumu, lakini kuna watu ambao sio Madaktari, wakifika pale wanaharibu kabisa taaluma ya Madaktari wetu.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuja hapa atuambie kuhusu wale watu ambao wanavaa nguo za manjano ambao sio Madaktari, lakini wanajifanya ni Madaktari, wanachukua pesa za wapiga kura, pesa za walalahoi halafu dawa hawapati, matokeo yake fani yote ya Madaktari wanapewa majina mabaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo Muhimbili, nilitibiwa vizuri na Madaktari mabingwa wa pale, lakini kuna watu wamevaa vinguo vya manjano eti wasaidizi wa Madaktari ukifika pale wanakupokea wao, hao watu waandikeni namba kwenye mashati yao ili tuwajue. Mkifanya namna hii mtafanikiwa sana na hamtakuwa mnapata matatizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ndugu zangu tusiendelee tu kuangalia, mwangalie dawa. Dawa ni kitu muhimu sana kwa Watanzania. Leo hii hospitali nyingi hazina dawa na tatizo ni kwamba siyo ninyi, huko nyuma watu walikuwa wanapeana uongozi. Huo uongozi walivyokuwa wanapeana, imefika mahali mtu anakwenda kuchukua dawa feki ilimradi hela zinaingia mfukoni mwake halafu tunakuwa hatupati chochote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja aangalie kabisa; anapasua majipu, amepasua majipu vizuri sana, lakini aangalie watu wengine, wanunuzi wa madawa hawa; wanunua dawa zinakwenda wapi? Dawa zinaonekana zimetoka MSD zimekwenda mikoani, mikoani hazijafika, ziko kwa akina nani!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona niyaseme hayo, lakini naomba kitu kingine. Hospitali yangu ya Korogwe ni hospitali kubwa sana, ina mikoa karibuni mitatu, Mkoa wa Pwani, Mkoa wa Tanga, Mkoa wa Kilimanjaro. Kila ajali inayopatikana barabara kubwa wagonjwa wote wanaingia pale Magunga Hospitali, lakini inatengwa sana hii hospitali. Ni kwa sababu gani? Kama Tumbi imekuwa hospitali teule, kwa nini Korogwe isiwe hospitali teule na kila kigezo kiko tayari? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mtuangalie na sisi watu wa Tanga; Mheshimiwa Waziri anatoka Tanga. Yeye anafanya mambo makubwa sana kwenye mikoa mingine, hata Mkoa wake! Amekuja kwangu mara tatu na amefanya kazi kubwa, ametoa madawa, ametoa mashuka hebu apandishe hadhi. Mheshimiwa Simbachawene yupo. Nilikuwa niombe hilo na kwa sababu ana Makamu wake makini na anafanya kazi kwa kujitolea sana, hebu fanyeni kazi mhakikishe kwamba Tanzania hii kwanza mwongezewe pesa, mlizotengewa hapa ni ndogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufatana na mazingira ya sasa, miaka ya nyuma watu walikuwa milioni 12 wakaja kuwa milioni 25 sasa hivi ni milioni 48, milioni 48 kwa mabilioni haya mnayoyatenga, watu watatosheka kiasi gani? Hebu tubadilike! Kama kweli tunataka kuisaidia hii Wizara ya Afya, bajeti hiyo ni ndogo, iongezwe ili dawa ziende na mashuka yaende.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unakuta hospitali nzuri haina vitanda, haina shuka, haina Madaktari. Madaktari pia ni watu wa kutakiwa waonekane sana.
Wengine mnafika mnawatukana Madaktari. Mnawatukana kwa lipi, wakati mgonjwa umekuja pale, umemkuta Daktari ana mgonjwa mwingine; unataka atolewe mgonjwa mwingine aingizwe babu yako eti kwa sababu ni ndugu yake na Maji Marefu. Naomba hili tatizo Mheshimiwa Waziri aliangalie sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri wa Fedha yupo hapa, hebu bwana mipango rafiki yangu, ongezeni pesa pale. Mnasema kilimo, maji, umeme, lakini hakutakuwa na umeme bila kuwa na afya; hakutakuwa na elimu nzuri bila kuwa na afya; hebu tuyamalize haya. Tukiyamaliza haya, mambo mengine yote yatakuja. Tufanye vitu vichache ambavyo vitasaidia, watu wataviona kwamba, vimekamilika kuliko… (Makofi)
MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Nashukuru sana.