Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya na Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula, East African Community Protocol on Sanitary and Phytosanitary Measures – EAC SPS ambalo linalenga Kuwa na viwango ambavyo vitaleta ushindani katika soko la Afrika Mashariki pale ambapo tutakuwa tunapeleka mazao na wanyama wetu kwenye hili soko la Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nchi yetu ya Tanzania imechelewa kwa miaka nane kama ilivyoelezwa tangu mwaka 2013, lakini nafahamu kwamba ilikuwa ni uwoga. Kama nchi tulikuwa hatuko tayari na tulikuwa tuna mashaka kama hizi fursa zitatolewa pengine wenzetu wanaweza kufaidi zaidi kuliko sisi. Hili lilikuwa ni jambo la msingi kwa sababu ukiangalia misingi yetu kama nchi, tumekuwa na mfumo ule wa kiutawala wa kiujamaa, wakati mwingine umekuwa ukijitenga sana na mifumo hii ya kidunia. Tukafikiri kwamba tukiwa sisi peke yetu pengine ndani ya nchi tunaweza tukafanya mambo yetu, lakini ukiangalia mabadiliko yanayoendelea sasa duniani hatuwezi kusimama peke yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata ukisoma katika Maandiko Matakatifu, katika Kitabu cha Mwanzo 11:6 pale, inazungumzia umoja; anasema, watu hawa ni wamoja, lugha yao ni moja na sasa hili ndilo wanalifanya na hakuna atakayewazuwia. Sasa tukifikiri sisi kama Taifa tunaweza tukasimama peke yetu hiyo haiwezekani. Ni kweli, ukiangalia ki-teknolojia kama Taifa hatuko tayari, wenzetu wamesha- advance kwa mambo mengi, lakini sasa tutasubiri mpaka lini? ukiendelea kusubiri baadaye tutafungiwa milango na tukishafungiwa milango inaweza ikawa pengine ni kazi kubwa kuja kuifungua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi naona hili jambo ni la msingi sana, kama nchi tuchukue hatua tuingie. Yale mapungufu ambayo yapo tuchukue hatua ya kuanza kuyatekeleza na kuziba mianya hiyo ili sasa tuingie kwa miguu miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ambalo naliona katika kutekeleza Itifaki hii ni muhimu sana kuhusisha sekta binafsi. Kwa mfano, ukizungumzia habari ya kulima parachichi kule Njombe, Serikali haiko, lakini watu binafsi wanalima na wanauza kwenye masoko ya nje na haya maparachichi yanakubalika. Ukiangalia wakulima kama akina ASAS wanatengeneza vyakula vyenye viwango vya kimataifa. Kwa hiyo, kama tukihusisha sekta binafsi ni rahisi sana kuwakilisha nchi yetu na kuleta ushindani kwenye soko la Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimeona kwamba kama tutaingia kwenye Itifaki hii kuna manufaa makubwa; kwanza ushirikiano wa pamoja lakini tunaweza kuteteana kama Jumuiya. Kama tunaamua kuuza bidhaa zetu pengine Ulaya, Marekani, kwa kuwa sasa tuna Itifaki ya pamoja kama nchi moja inapeleka kule inazuiliwa nchi nyingine inaweza ikaitetea. Kwa hiyo, unakuta kwamba tukiungana kwa namna hii inakuwa ni kazi rahisi tutaweza kuendelea kwa Pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunaweza kufaidishana kati ya nchi na nchi hasa kimaarifa. Kama tunafanya kazi kwa pamoja tukishirikiana na Wakenya na Warundi na Waganda, tukikaa kwa pamoja tuna-share ile wanasema maarifa. Kwa hiyo, kama tukijenga maarifa na ufahamu wa pamoja ni rahisi sana kujenga nguvu ya pamoja na tukaweza kufanikiwa kama Jumuiya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nishauri kwa kuwa tayari Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Biashara Duniani hii Itifaki pia inaweza kuisaidia Tanzania kufanya biashara hata kwenye masoko ya kimataifa. Ukiangalia pia tumeshapitisha mikataba mingine ya kimataifa inayohusiana na usalama wa mimea na wanyama pamoja na mazao. Kama tulishapitisha hii mingine miaka mingi iliyopita hakuna sababu ya kuikataa hii tunakuwa tunajichelewesha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nachoomba hii iwe changamoto kwa Taifa, kwamba tuingie, lakini changamoto ambazo tutazikuta huko tukabiliane nazo kwa sababu tukiendelea kuchelewa haitusaidii kama nchi. Tunaweza tukapima matokeo tangu tumeanza kukataa nchi yetu imefika wapi? Tukiangalia kiuchumi tuko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi nawashauri Wabunge wenzangu kwamba tuipitishe Itifaki hii, lakini changamoto tutakazozikuta kule mbele tukabiliane nazo na baadaye tutavuka na tutapata manufaa makubwa katika kuuza bidhaa zetu zinazotokana na mazao ya kilimo katika nchi za Afrika Mashariki lakini pamoja na nchi za nje. Ni kweli kumekuwa kuna mashaka, ukiangalia hii miaka nane iliyopita kulikuwa kuna vipengele viwili ambavyo tumeona vilikuwa vinaleta mashaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, ilikuwa inaonesha kama tukisaini Itifaki hii tutalazimika pia kufuata mikataba mingine ya EPA ambayo inazungumzia ulinzi wa kimazingira ambayo ilianzishwa na Marekani. Pia kulikuwa kuna mashaka kuhusiana na mambo ya GMO lakini wenzetu wametueleza kwamba hatulazimiki kwenda kutumia hizi GMO, hasa mbegu, kuleta kwenye ardhi yetu. Kwa hiyo, hicho kipengele kimeangaliwa na sisi tumejiridhisha kwamba kama hilo halitakuwa ni kigezo basi tuko tayari kuingia na kuisaidia nchi yetu iweze kupata manufaa ya kibiashara kwanye hili soko la Afrika Mashariki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa hayo machache, niwashauri Wabunge wenzengu kwamba tuunge mkono halafu twende tukakabiliane na changamoto ambazo tunaziona ziko huko mbele. Nashukuru sana. (Makofi)