Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi nami niweze kutoa mchango wangu kwenye itifaki hii. Kwanza nawapongeza Serikali kwa kuona sasa ni wakati umefika wa kuweza kutuletea azimio hili au itifaki hii. Itifaki hii ina maslahi mapana sana na wakulima wetu pamoja na wafugaji. Pale wafugaji na wakulima wanaponufaika ni moja kwa moja Taifa letu linakwenda kunufaika.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali kwenye mambo kadhaa ili tuweze kufanya vizuri. La kwanza, kwenye itifaki hii, kwenye suala zima la mifugo, afya ya mimea pamoja na mazao yote, tuna upungufu mkubwa wa wagani ambao wao ndio wana uwezo wa kwenda kuhakikisha bidhaa zetu kwa maana ya mifugo yetu, mimea yetu, matunda yetu, mboga zetu na kila kitu itakwenda kukidhi mahitaji ya itifaki hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kumekuwa na kigugumizi cha muda mrefu cha kutokuajiri Maafisa Ugani. Sasa naiomba Serikali, kwa kuwa tumeamua kuingia kwenye itifaki hii, ni wajibu wetu kama nchi kuona umuhimu wa kwenda kuajiri Maafisa Ugani wa kutosha ili tuweze kunufaika na hii itifaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni suala zima la watafiti. Bila utafiti pia bado hatutaenda kuleta tija kwenye hii itifaki. Watafiti wetu wametengwa, wametelekezwa, hawana chochote ambacho wanakifanya. Wapo tu wanaitwa watafiti, lakini kwa maana sasa ya kwenda kutekeleza na kupata tija kwenye itifaki, naomba Serikali ione namna bora ya kwenda kuwaongezea fedha za kutosha watafiti wetu ili waweze kufanya kazi nzuri itakayoleta matunda kwa Taifa letu kwa ajili ya hii itifaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamesema suala zima la wadhibiti ubora; na Mheshimiwa Ndakidemi amesema kwamba TBS imezidiwa, ni kweli. Sasa wakati Serikali inakwenda kuangalia ni namna gani ya kuanzisha chombo kingine ambacho kitakwenda kumsaidia TBS, naiomba Serikali iende ikaongeze nguvu ya bajeti, pamoja na wataalam na vitendea kazi TBS ili waweze kuifanya hii kazi kwa ufanisi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, kuna suala zima la elimu kwa watendaji wetu ambao wako mipakani. Pia naomba nchi wanachama tukiwemo sisi Watanzania, twende tukatoe elimu kwa watendaji wetu ambao wako mipakani ili waweze kuelewa mkataba huu ni namna gani ulivyoingia? Ni vitu gani vinavyozingatiwa? Ubora ni upi? Hii itaondoa changamoto kwa Watanzania wetu ambao watakwenda kufanya hizo biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo natamani pia kuishauri Serikali, ni kuona sasa itifaki hii inaenda kuwa ni mwarobaini wa changamoto mbalimbali zinazotokana na upungufu wa bidhaa zetu tunapokwenda kuzipeleka kwao ama zinapokuja kwetu. Tuliona miaka michache iliyopita, miwili au mitatu, tuliteketeza vifaranga, lakini tuliona mahindi yetu yakikataliwa mpakani. Sasa kwa mujibu wa hii itifaki, iende ikatuweka wamoja na tutafute njia mbadala nzuri itakayokwenda kutusaidia kuondokana na hizi changamoto za kuwa tunaendelea kunyoosheana vidole na nchi za wenzetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine kwa msisitizo tu ni suala zima la sheria kwamba Wizara sasa mtuletee Muswada wa Sheria, Kanuni na Sera ili tuweze kupata kitu kitakachokwenda kutusaidia kuisimamia itifaki hii. Msipotuletea mapema, ina maana tutaidhinisha leo, then tutaenda kuweka makabatini kwenye shelves zetu, hatutaweza kufanya kitu chochote na mwisho wa siku itakuwa hakuna kitu chochote kinachokwenda kufanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru kwa nafasi. Ahsante. (Makofi)