Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa Chakula

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye hili Azimio la kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Afya ya Wanyama na Usalama wa Chakula na mchango wangu utajikita kwenye eneo zima la usalama wa chakula.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kuishauri Serikali kwenye eneo zima la usalama wa chakula kwa maana ya inasimamiwa chini ya wapi? Good practice ni kwamba masuala ya usalama wa chakula yanapaswa kuratibiwa chini ya Wizara ya Afya kwa sababu kimsingi maana ya usalama wa chakula ni kuona namna gani ambavyo utalinda walaji wasipate changamoto zozote zinazotokana na madhara ya chakula. Jambo hili ni jukumu la Wizara ya Afya, lakini sasa hapa kwetu tulichofanya
tumeweka jukumu la usalama wa chakula kwa maana ya food safety chini ya TBS.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuishauri Serikali, maadam tumeamua kuridhia azimio hili, basi lazima tukatafakari upya na tufanye mabadiliko ambayo yatawezesha suala la usalama wa chakula yawe chini ya Wizara ya Afya na siyo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo hapo naipongeza sana Wizara ya Kilimo kwa sababu wameimarisha usimamizi kwenye afya ya mimea chini ya TPRI, lakini hivi sasa TBS ina majukumu mengi na haiwezekani aendelee kuwa na majukumu yale yale. Kwa hiyo, naendelea kusisitiza suala hili liwekwe chini ya Wizara ya Afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile moja ya matakwa ya itifaki hii duniani chini ya Well Trade Organization, ni lazima nchi iwe ina Sheria ya Usalama wa Chakula. Tanzania bado hatuna Sheria ya Usalama wa Chakula. Kwa hiyo, napenda kusisitiza kwa Serikali, maadam tumeamua kuridhia azimio hili, basi Serikali ifanye jitihada ya haraka kutuletea Sheria ya Usalama wa Chakula ili tuendane na takwa hili la kidunia. Ndani ya nchi zetu za Afrika Mashariki, ni Kenya peke yake ambayo tayari wanayo Sheria ya Usalama wa Chakula. Kwa hiyo, kwa mantiki hiyo, sisi kuendelea kutokuwa na Sheria ya Usalama wa chakula, ina maana yako maeneo ambayo hatutaweza kunufaika ipasavyo. Kwa hiyo, nasisitiza Serikali ije na Sheria ya Usalama wa Chakula kwa maana ya Food Safety na siyo Food Security. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nishauri kuhusu suala la usimamizi wa usalama wa afya ya mazao ya kilimo. Usimamizi wa afya ya mazao ya kilimo inapaswa iwe chini ya Wizara ya Kilimo na siyo TBS. Kwa hiyo, naomba niishauri Serikali kupitia Wizara ya Kilimo ione ni namna gani baada ya azimio hili litakapokuwa limeridhiwa na Bunge lako Tukufu, basi usimamizi wa masuala yote ya usalama wa afya ya mazao ya kilimo yawe chini ya Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kumalizia mara baada ya sisi kuidhinisha na kuridhia azimio hili, ni muhimu sana Serikali kupitia Wizara ya Kilimo iweke jitihada kubwa ya kutoa elimu kwa wakulima wetu na wananchi wetu ili tuwe na uelewa wa haya matakwa na ituwezeshe kuhakikisha kwamba tutakuwa tunazalisha mazao yanayoendana na itifaki husika ili tusije tukajikuta tumeridhia hili azimio, lakini hatujajengea uwezo wakulima na wananchi waweze kuzalisha, kusafirisha, kusindika na kuhifadhi kadiri ambavyo itifaki inahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nirudie tena kwamba tunahitaji kuwa na Sheria ya Usalama wa Chakula; naomba nirudie tena, tunahitaji suala la usalama wa chakula liwe chini ya Wizara ya Afya; naomba nirudie tena, tunahitaji suala la usimamizi wa afya ya mazao ya kilimo yawe chini ya Wizara ya Kilimo; na kwa kumalizia tunahitaji wananchi wetu na wakulima wetu wajengewe uwezo juu ya hii itifaki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kuunga mkono hoja. Ahsante. (Makofi)