Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kutoa mchango wangu katika Azimio la Bunge kuridhia Itifaki ya Bunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Viwango vya Afya ya Mimea, Wanyama na Usalama wa chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kwamba hili jambo ni jema kwa maslahi ya Taifa letu na tunaamini sisi kama Watanzania tunakwenda kunufaika. Niwapongeze Wizara kwa kuliona hili na kulileta kwetu ili tuweze kulijadili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa niongelee sana kwenye Sera ya Chakula na Lishe. Unapoongelea chakula na lishe, ndipo ambapo utaona kwamba mimea, wanyama na usalama wa chakula unapoenda kuangukia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Sera ya Chakula tunayoitumia mpaka sasa ni ya mwaka 1992. Kiuhalisia tunaona ni Sera ambayo imepitwa na wakati na inahitajika kufanyiwa marekebisho ili kuendana na wakati na mahitaji ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kwanza niwapongeze kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuhakikisha hali ya lishe ya Watanzania inaendelea kuwa vizuri. TFNC walianza zoezi la mapitioa ya Sera ya Lishe mwaka 2015/2016 na kimsingi mwaka 2017 waliweza kutoa Waraka ambao waliuwasilisha kwenye Baraza la Mawaziri ambao sekretarieti na Bunge zilipitia zikaona ipo haja ya kuwa na Sera ya Chakula na Lishe. Mpaka sasa hivi Sera ya Chakula na Lishe bado haijapitishwa kwa marekebisho ambayo yalikuwa yamefanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, na tunachofahamu mpaka sasa hivi kama Taifa tunazo Kamati za Lishe ambazo zimekuwa zikiendelea kufanya kazi na Kamati ya Lishe hii ni mtambuka. Hapa najaribu kuonesha ni kwa nini tunahitaji Sera ya Chakula na Lishe. Unapoongelea lishe ni kitu mtambuka kinagusa idara nyingi. Kitu ambacho huwezi ukaongelea usalama wa chakula peke yake bila kuiweka kwenye Sera ya Chakula na Lishe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilitamani tunapokuwa tunaenda kukimbizana na hili Azimio tukumbuke kwamba katika nchi yetu kuna baadhi ya mambo ambayo hayajakaa vizuri ikiwamo na Sera ya Chakula na Lishe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi, tunafahamu kwamba usalama wa chakula umekuwa ukiathiri lishe za wananchi wetu na masuala ya usalama wa chakula yanagusa mambo ya kuanzia ngazi ya uzalishaji kwenye kilimo kwa maana unapolima lakini pale unapoenda kwenye usindikaji wa hivi vyakula lakini pia utakuta wakati wa transportation, usafirishaji wa haya mazao na hawa wanyama na pia katika eneo la matumizi yaani uhifadhi wa hivi vyakula. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na ninapokuwa nasema haya, nilitamani wasizingatie suala moja tu la sumu kuvu, wakumbuke kwamba kuna maeneo mengine ambayo mfano kuna maeneo ambayo yanakuwa na heavy metals mfano maeneo yenye zebaki. Kwa hiyo, tunapokuwa tunatengeneza maabara zetu zizingatie vitu vyote ambavyo vitakuwa na athari ya vyakula vinavyoingia nchini mwetu lakini hata vyakula ambavyo sisi tunatakiwa tuvitoe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na wenzangu waliosema ipo haja ya kuwa na maabara za kisasa kwa maana ya kwamba wananchi wetu wasipate hasara ya kusafirisha mizigo ambayo inaenda kukataliwa baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu ninaiomba Serikali kupitia kikao hiki iweze kuona haja ya kuanzisha chakula na hata wanapoileta hiyo Sera ya Chakula, kwa miaka hii ambayo imekaa naona ipo bado haja ya kufanya amendment tena kwa sababu kuna mabadiliko ambayo yametokea hapa kati ndani ya miaka mitatu/minne hii ambayo yatakuwa hayamo mle kwenye ile sera. Kwa hiyo, badala ya kuendelea pale walipokuwa wameishia, wairudishe nyuma kidogo, hivi vitu vidogo vidogo viweze kuwa amended ili iendelee na mchakato, ahsante. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, ahsante. (Makofi)