Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Njombe Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
3
Ministries
nil
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia kwenye hoja iliyo mbele yetu ya Kuridhia Mkataba wa Eneo Huru la Afrika. Napenda kuanza kwa kusema kwamba Mkataba huu tunaelewa kabisa umeridhiwa na baadhi ya nchi na nchi hizo ziko katika eneo letu la Afrika Mashariki. Hata hivyo kuchelewa kwa Tanzania kuridhia mkataba huu kumeleta hisia kwamba pengine wafanyabiashara wa Tanzania wanaogopa au wana uoga. Napenda kukudhihirishia, wafanyabiashara wa Tanzania hawana uoga wa kuingia kwenye ushindani, wafanyabiashara wa Tanzania wanaamini ushindani ndiyo utakaoboresha biashara zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa na nafasi ya kuwa Mjumbe wa Baraza la Biashara la Tanzania nikiwakilisha sekta binafsi katika nafasi yangu ya huko nyuma. Tatizo kubwa la wafanyabiashara wa Tanzania ni kuhakikishiwa kwamba kutakuwa na ushindani ambao upo level au uko sawa au una usawa, Waingereza wanaita level playing ground.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo naomba niwashauri Wabunge kwamba wafanyabiashara wetu wanaiona hii ni fursa, nao ndio watakaokwenda kwenye soko hili. Wafanyabiashara/sekta binafsi ndio watakaokwenda kwenye soko hili na tuna kila sababu ya kuwasaidia na kuwa-support. Nao wanachotaka siyo Serikali iwape fedha, Serikali iendelee kuboresha mazingira ya biashara. Tumeisema kwenye Kamati kwamba Serikali iendelee kuboresha mazingira ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami napenda kusema kwenye hili, Serikali ina forum ya kuongea na wafanyabiashara on almost quarterly basis. Tunaomba sana forum hii itumike vizuri ili kuweza kujua matatizo ya wafanyabiashara wa Tanzania kila wakati ambapo yanajitokeza, isiwe inangojewa mpaka malalamiko yanafika mbali au yanakuwa makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan hapa kwa juhudi zake kubwa sana za kuliweka hili jambo wazi na kuwaambia Watendaji ndani ya Serikali na kuonyesha mwelekeo wa nchi yetu kwenye masuala yote ya uwekezaji pamoja na kutoa kauli ambazo sasa zinatabirika katika Jumuiya ya Wafanyabiashara. Jambo hili ni zuri kwa nchi yetu, jambo hili ni zuri kwa wafanyabiashara wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ni la muhimu sana ili tuweze kufanikiwa kwenye suala hili ni kuhakikisha tunakwenda kwenye ushindani. Ushindani ni suala la bei na ubora. Sasa kwenye ubora, kwa kiasi kikubwa ni suala la mwekezaji mwenyewe au mfanyabiashara. Serikali kazi yake ni kuhakikisha kwamba standards zinakuwa met. Kuna suala la bei. Kwenye bei wafanyabiashara wetu lazima tuwasaidie. Nasi msaada wetu kama nchi au kama Serikali ni kuhakikisha kwamba tunawapunguzia gharama ambazo siyo za lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wameliongea, kuna gharama nyingi ambazo siyo za lazima; nyingi tunasema ni kama tozo, lakini kuna gharama nyingine. Kwa mfano, ukichukua mkataba unaohusiana na masuala ya electronic stamp, tumeliongea sana hili hapa Bungeni. Gharama ya mkataba ule ni kubwa mno. Wenzetu watakaokuwa wanazalisha vitu hivyo na kuvileta katika soko letu, pengine hawana hiyo gharama au kama wanayo ni ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasi tuliangalie. Kwa mfano, TBL wanatumia dola milioni tisa kwa mwaka kwa kuweka hizo stamp tu. Hiyo gharama ni kubwa sana, nayo inakwenda kwenye masuala mengine vilevile. Tuangalie pia utaratibu mzima wa wafanyabiashara kuhakikisha kwamba tunaweza kuwarudishia kile ambacho wanadai kama VAT. Ni jambo la muhimu sana. Wengi tunashindwa kuelewa kwamba mtaji wa mfanyabiashara siku zote unahesabiwa kwa shilingi. Anapokuwa anadai Serikali marejesho na yanachukua muda mrefu, inampunguzia mtaji wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda niliseme, naomba sana Serikali ifanye uchambuzi vizuri. Najua ndani ya mkataba huu unatoa nafasi ya kuhakikisha kuna maeneo ambayo tunadhani kwamba bado hatujafikia uwezo wa ku-compete au pengine tuna-comparative advantage. Serikali iyachambue vizuri. Nitatoa mfano, kuna maeneo ya nguo tumeambiwa kwamba haya yatabakia kuwa yetu, lakini kuna maeneo mengine uchambuzi ufanyike na hasa maeneo yale ambayo SMEs zetu zitashiriki. Iko haja ya kuona namna gani tutawasaidia ili waweze kuingia kwenye soko hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hii hoja na naomba sana Wabunge wenzangu tuipitishe kwa nguvu zote. Ahsante sana. (Makofi)