Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kukushukuru sana kwa jinsi ambavyo umeendesha mjadala huu na kutupa nafasi ya kuweza kuwasilisha Azimio hili. Nimshukuru sana Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu Mkataba huu uwasilishwe hapa Bungeni kupitia Baraza lake la Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka nichukue nafasi hii pia kumshukuru sana Mwenyekiti wa Kamati yetu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Mheshimiwa David Kihenzile na Makamu wake Mheshimiwa Eric Shigongo na Wajumbe wote kwa nafasi ambayo walipata ya kuchambua kwa kina sana Mkataba huu. Nikutaarifu tu kwamba siku tunajadili Mkataba huu, tulikuwa na Wenyeviti wa Kamati wengine walikuja kushiriki zaidi ya Wenyeviti watano. Kwa hivyo, siku ile ilikuwa ni mjadala mzuri sana na Waheshimiwa walipata nafasi ya kuchambua na kuuliza maswali na sisi ni wataalamu tuliweza kuwajibu ipasavyo. Pia nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wamepata nafasi ya kuchangia, kwa hoja zao lakini pia kwa uwingi wao na ujumla wao kwa kuunga mkono hoja hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kwa kiasi kikubwa karibu Wajumbe wote wameunga mkono hoja hii, sitaki kutumia nafasi hii kuchukua muda wako mwingi katika kujibu. Naomba nitoe ufafanuzi kwa maeneo machache sana katika kuhitimisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kutoka kwa Kamati walitoa maoni na mapendekezo kwamba ni muhimu sana tukachagua bidhaa za kulindwa kwa umakini mkubwa. Nataka tu nilitaarifu Bunge lako kwamba katika Mkataba huu na katika majadiliano ambayo tumeyafanya kwa sasa tumekamilisha majadiliano kwenye Itifaki tatu; Itifaki ya Biashara ya Bidhaa; na Itifaki ya Biashara ya Huduma na Utatuzi wa Migogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukubaliana huku tumegawa bidhaa katika makundi makubwa matatu. Kuna kundi la kwanza ambapo tunajadiliana tufikie asilimia 90 na Wakuu wa Nchi na Serikali waliagiza kwamba ili biashara ianze kufanyika tukubaliane kufanya biashara katika angalau asilimia 90 ya bidhaa. Sisi tuna-negotiate kama Afrika Mashariki na tumeshakubaliana asilimia 86, majadiliano yanaendelea ili tupate bidhaa tufike asilimia 90.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kundi la pili ni asilimia 7 ambazo hizi hatutaingia kwa sasa, tutaingia katika kipindi cha miaka 13 ijayo. Hizi ni bidhaa ambazo zitaingia katika soko hili baadaye katika miaka 13.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna kundi la tatu ambalo ni asilimia 3, hizi ni bidhaa ambazo hatutaingia kabisa. Hizi ni bidhaa ambazo nchi zimekubaliana zipo kwenye kitu kinaitwa exclusion list kwamba zenyewe hazitakuwa sehemu ya bidhaa ambazo zitafunguliwa masoko haya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, wataalamu na Serikali tumekaa tayari tunaendelea na majadiliano kuona kwamba ni bidhaa gani ziingie kwenye asilimia 3, zipi ziingie kwenye asilimia 7 na zipi ambazo ziingie kwenye asilimia 90. Kwa hivyo, Serikali ipo makini kwenye jambo hili lakini pia Mkataba umetoa mawanda mapana kuhakikisha kwamba nchi zinalindwa katika hatua zake za viwanda na biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya pili, nataka tu niseme kwamba tayari sisi kama Tanzania tuna-advantage ukilinganisha na wenzetu kwa sababu sisi tayari tupo katika nchi 19, kwa maana ya kwamba sisi ni Wajumbe wa EAC na Wajumbe wa SADC, kwa hiyo, tayari tulishafunguliana masoko yetu. Kwa hivyo, sisi ni wazoefu wa kutosha, katika nchi zote 54 tayari sisi tunafanya biashara na nchi 19, kwa hivyo, hili jambo siyo jipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema wengine, tathmini imefanyika kwa kina sana na Wizara ya Fedha na Mipango kuona matokeo chanya na hasi ya kujiunga na Mkataba huu. Hitimisho ni kwamba matokeo chanya ni mengi zaidi na kwamba ni lazima twende kwenye Mkataba huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema wengine, nikitoa mfano tu takwimu za mwaka jana tumeuza EAC dola milioni 812 ukilinganisha na zile ambazo tumeingiza Tanzania dola za Kimarekani milioni 324. Kwa hivyo, tunauza zaidi kuliko vile ambavyo tunavyonunua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, SADC tumeuza dola za Kimarekani milioni 999 wakati ambazo tumenunua sisi ni dola za Kimarekani milioni 604. Kwa hivyo, hakuna kipya ni kwamba uzoefu tunao na kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge tunafanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine niitolee ufafanuzi kuhusu hizi tozo, Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo kwamba lazima tufanye review na kuna review kubwa inaendelea kuhusu tozo mbalimbali jinsi ambavyo tunakamilisha biashara. Tunaamini kwamba mwaka huu tutapata suluhu kwa baadhi ya maeneo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nieleze hili la ETS na VAT refund ambalo Mheshimiwa Mwanyika aliliongelea, kama ambavyo mnafahamu, tayari Serikali imeshaanza kulipa VAT refund. Sisi tumeshapokea pongezi nyingi kutoka kwa wafanyabiashara wakishukuru sana kitendo ambacho Serikali imefanya cha kuanza kuwalipa VAT refund. Pia ETS tunafanya majadiliano na Wizara ya Fedha na wafanyabiashara ili kuona kwamba gharama za huduma hii zinapungua, tumeshakubaliana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja nyingine ambayo ni ya msingi pia imetolewa na Waheshimiwa Wabunge kuhusu utafiti za kina na hili aliliongelea Mheshimiwa Aida juu ya faida na hasara. Kama nilivyosema Serikali imefanya utafiti wa kutosha sana lakini pia watafiti huru wameshiriki kwenye suala hili. Tunao utafiti wa REPOA na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na wame-publish study mbili hapa muhimu kabisa na zote ni mpya za mwaka jana. Moja, inaitwa: “Cost and Benefits of Regional Integration in Tanzania: Case Study of African Continental Free Trade Area”. Hitimisho lao ni kwamba Tanzania ijiunge na eneo hili mapema sana kwa sababu kuna faida kubwa kuliko hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini study ya pili ambayo wameifanya inasema: “Regional Integration and Tanzania’s Export Performance” wakiifanyia EAC na SADC. Katika study yao wameonyesha wazi kwamba Tanzania katika miaka 10 iliyopita imekuwa ikifaidika sana kuwa Mjumbe wa EAC na Mwanachama wa SADC katika suala zima la biashara. Hitimisho lao ni kwamba hatuna sababu ya kuogopa, tujiunge haraka kwa sababu kwa kweli nchi inakwenda kufaidika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama walivyosema Waheshimiwa Wabunge hatuna sababu ya kuogopa. Tupo tayari na Serikali imefanya maandalizi ya kutosha sana kwa ajili ya kujiunga na eneo hili. Pia wafanyabiashara tumefanya nao kazi sambamba na kwa kweli wao wangetaka tujiunge juzi sio leo. Kwa mfano, hata leo asubuhi wameniandikia email kunitakia kila la kheri katika kuwasilisha Azimio hili na kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge waridhie. Kwa hiyo, napenda kusema kwamba Serikali imejiandaa, wafanyabiashara wamejiandaa na tupo tayari kufanya kazi na wenzetu katika eneo hili la biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, nihitimishe kwa kusema kwamba nchi yetu iliongoza mapambano ya ukombozi wa kisiasa katika Bara la Afrika. Sisi ndio tulikuwa viranja, tunapoanza mapambano ya ukombozi wa kiuchumi hatuwezi kubaki nyuma. Mkataba huu unatupa fursa ya Tanzania kuchukua nafasi yake katika Bara la Afrika katika kuongoza mapambano ya kujikomboa kiuchumi. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge waridhie Azimio hili ili tuanze safari hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.