Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Buyungu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunipatia nafasi kuchangia kwenye Mapendekezo ya Mwongozo wa Bajeti kwa mwaka 2022/2023. Kwa nafasi hii, nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, kwa fedha nyingi sana ambazo ametuletea sisi Wilaya ya Kakonko kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kakonko kwa fedha ambazo tumepata, zinakwenda kufungua na kujenga barabara maeneo mengine ambayo tangu dunia inaumbwa tulikuwa hatujawahi kupata barabara. Mheshimiwa Rais katupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Waziri wa Fedha kwa Mpango mzuri aliotuletea. Hii inakwenda sambamba na Kamati yenyewe, Kamati ya Bajeti. Nawapongeza sana kwa kazi nzuri ambayo wameifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nitachangia katika maeneo machache, moja ni uandaaji na utengaji wa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi ya kimkakati, ipo miradi ya kimkakati kama umeme, mpango wa bwawa la umeme maharufu kwa jina la Mwalimu Nyerere, reli ya kisasa Standard Gauge na miradi mingine kama hiyo. Muda mwingi fedha ambazo zinapangwa katika maeneo hayo zimekuwa ni fedha kidogo naomba sana fedha ziandaliwe za kutosha ili miradi hiyo iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni miradi ambayo ni ahadi ya Viongozi wa Kitaifa, nimekuwa nikifuatilia muda mwingi Waheshimiwa Wabunge wengi wanauliza maswali kufuatia maeneo ambayo viongozi wa kitaifa waliahidi ujenzi wa miradi ya maji, ujenzi wa barabara na kadhalika. Niombe pia fedha ziandaliwe za kutosheleza maeneo hayo ili kuondoa changamoto ambayo inajitokeza muda mwingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, napongeza sana kwamba fedha nyingi zimetolewa na zimepangwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa lakini haijaonyesha kwenye mpango huu fedha kwa ajili ya nyumba za walimu. Kujenga madarasa bila kujenga nyumba za walimu hakutapelekea ukamilifu wake hii ni kwa sababu fedha zimepelekwa kwenye maeneo mfano shule shikizi, ukifuatilia kwa ukaribu shule shikizi zimejengwa katika maeneo mapya, mengi ni maeneo ambayo ni ya wafugaji, mengi ni maeneo ambayo ni ya wakulima kwa hiyo ukijenga madarasa katika maeneo hayo bila kujenga nyumba za walimu katika maeneo hayo kwa ukaribu maana yake wanafunzi watakuwa wanasoma na madarasa yatakuwa yanaachwa wazi, maana yake hayatakuwa na uangalizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba fedha zitengwe kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu na hii itapelekea walimu kukaa karibu na shule lakini hii pia itapelekea shule kuwa na ulinzi kwa maana kwamba walimu watakaa karibu na shule. Vilevile madarasa yale yataweza kutumika vizuri. Kwa hiyo hamuendi kama ambavyo tumeamua kupeleka fedha nyingi upande wa ujenzi wa madarasa basi tupeleke fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la mabweni, mabweni ni muhimu sana kwa ajili ya watoto hasa watoto wa kike kwa upande wa shule za sekondari, kutokuwa na mabweni kunapelekea wanafunzi hawa kusafiri umbali mrefu, kutokuwa na mabweni kunapelekea wanafunzi hawa kukutana na vishawishi njiani. Niombe fedha za kutosho zipelekwe katika maeneo hayo tuwe na mabweni ya kutosheleza wanafunzi waishi maeneo hayo ili kuwa na uhakika kwamba watakuwa na muda mzuri wa kujisomea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ajira kwa walimu tumefanikiwa vizuri kwenye mpango wa elimu bila malipo, wanafunzi wapo wengi wa kutosha na muda huu tunapeleka madarasa ya kutosha lakini walimu bado hawajaonekana kwamba kuna mpango maalumu wa kuweza kuajiri. Ninaomba fedha ziandaliwe mpango uandaliwe mzuri ili walimu waajiriwe wa kutosha waweze kusaidia vijana wetu katika maeneo hayo, hii iende sambamba na ujenzi wa maabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule zetu za sekondari sawa tunapeleka fedha tunajenga madarasa lakini ukamilishaji wa maabara, ninaomba fedha ziandaliwe za kutosha kwa ajili ya ujenzi wa maabara. Ujenzi wa maabara unapelekea moja wanafunzi kupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo, wakijifunza kwa vitendo inapelekea uelewa mkubwa zaidi niombe hii iende sambamba na ujenzi wa maktaba katika shule zetu za sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ni muhimu sana hasa miundombinu ya barabara, Mkoa wetu wa Kigoma haujaweza kuunganishwa kwenye Mikoa mingine kutoka Tabora kwenda Kigoma, Mpanda kwenda Kigoma, Kagera kwenda Kigoma. Ninaomba fedha ziweze kupelekwa katika maeneo hayo, barabara ziweze kukamilishwa na kuweza kupelekea huduma muhimu sana kwa wananchi wetu hasa kwa Mikoa ile ambayo haijaweza kuunganishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)