Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Subira Khamis Mgalu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa na mimi jioni ya leo kuweza kuchangia mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango na bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kusimama jioni ya leo, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, mama Samia Suluhu Hassan; Makamu wa Rais, Dkt. Mpango; Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wote, kwa kazi inayoendelea kufanywa katika kuona kwamba nchi yetu inapiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa maandalizi ya mwongozo wa mpango huu. Na pia nampongeza Mwenyekiti wetu wa Kamati pamoja na taarifa ambayo imewasilishwa na ninaendelea kuunga mkono hoja ambayo tumewasilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mapendekezo ya mpango ambayo yamewasilishwa inaonesha Serikali imejipanga kukusanya na kutumia zaidi ya trilioni 39 kwa mwaka 2022/2023. Maoni yangu katika item hii ya makusanyo na matumizi kwa kuwa Serikali ina mzigo mkubwa wa miradi mbalimbali ya kimkakati, na kwa kuwa Serikali yenyewe iliahidi kwa mwaka huu wa fedha 2021/2022 kwamba itakamilisha kujifanyia tathmini ya namna ambavyo inaweza kukopesheka kwenye masoko ya kimataifa (sovereign credit rating), naomba mpango ujao sasa itakayouandaa Serikali ije na taarifa mahususi ya kukamilisha tathmini hii ili iweze kuingia kwenye soko la fedha la kimataifa kupitia infrastructure bond, kupitia Eurobond.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kupitia pia hatua ambayo hata Mheshimiwa Rais ameielekeza Wizara ya Fedha hizi municipal bond ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kugharamia miradi hii ya kimkakati ambayo inachukua muda mrefu kuweza kuanza kutumika na kuweza walau kuanza kurejesha sehemu ya gharama na Serikali ijikite katika kugharamia shughuli zile za msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tukizingatia imeshaongeza ajira mpya, imeshapandisha madaraja watumishi, imeshaongeza kwenye masuala ya mikopo ya wanafunzi, kwa hiyo ni wazi kabisa itahitaji fedha, na ili kuwapunguzia pia Watanzania zile kodi zingine kwa mfano tozo, Serikali ijikite kwenye masoko ya kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na tumeona namna gani Serikali imefanikiwa kwenye huu mkopo wa masharti ya bei nafuu, uwezo wa Mheshimiwa Rais wa kushawishi, wa kujenga hoja ndani ya muda mfupi tumeweza kupata trilioni moja na bilioni 300, ni wazi hata hili pia linawezekana.

Kwa hiyo ninaomba katika mpango unaokuja Mheshimiwa Waziri wajielekeze huko ili kupunguzia gharama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, ninaomba katika taarifa yake Mheshimiwa Waziri ameainisha kwenye ukurasa wa 20, ametoa msisitizo kwamba bado kuna mianya ya uvujaji wa mapato, lakini bado pia kuna mianya ya kuvuja mapato kupitia risisti EFD. Nashauri atakapokuja na mpango kamili aeleze kinagaubaga ni namna gani Serikali itadhibiti uvujaji ambao yeye mwenyewe ameusema katika taarifa yake, kwamba hali bado haiyumkiniki, hali bado siyo shwari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipongeze hatua ya Serikali ya kuweza kutoa kibali cha kuajiri watumishi zaidi ya 1,000 wa TRA. Hatua hii iendane na mkakati mahususi watakavyoweza kudhibiti mianya ya uvujaji wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nijielekeze kwenye suala zima la mwenendo wa mfumuko wa bei. Katika mapendekezo ya mpango huu yaliyowasilishwa inaonekana bado mwenendo wa mfumuko wa bei upo ndani ya viwango ambavyo vimeainishwa kwenye Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa, lakini hata hivyo mpaka sasa hivi mfumuko wa bei uko asilimia nne ukilinganisha na asilimia tatu ya kipindi kama hiki mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali ni tete mtaani. Bei za bidhaa cementi, bei za bidhaa nondo, bei ya mafuta, kwa kweli hali bado ni tete. Lakini niishukuru Serikali kupitia Wizara ya Nishati na nimpongeze Waziri wa Nishati, Mheshimiwa January Makamba, amekuwa akitufahamisha hatua mbalimbali na mwelekeo wa Serikali wa kuweza kuona bei ya mafuta inapungua au hata kama inaongezeka lakini si kwa kiwango kilichokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe Serikali kwa hizi bidhaa za nondo, cementi, mabati, tuiombe Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha nao watuambie, wawaarifu Watanzania mkakati wao wa kuona namna gani bei zinapungua. Na ukizingatia kupitia bajeti ya 2021/2022 Serikali iliweka hatua mbalimbali za kulinda viwanda vinavyozalisha bidhaa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza leo bei ya nondo ukilinganisha ya Julai kwa tani zinazozalishwa hapa nchini BS 300 ilikuwa milioni moja laki nane thelathini. Tunapozungumza leo mwezi Novemba, kwa tani moja ya nondo ya aina hiyo BS 300 inayozalishwa hapa nchini ni milioni mbili laki mbili themanini, ongezeko la laki nne na nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kwa kuzingatia kazi kubwa iliyofanywa na Mheshimiwa Rais ya hizi pesa za 1.3 trillion, na ujenzi unaoendelea zaidi ya bilioni 500 zimepelekwa kwenye ujenzi. Na ninaomba niikumbushe Serikali ilituletea pesa kipindi cha Aprili na Juni za ujenzi wa madarasa, milioni ileile 20, na sasa hivi kiwango cha ujenzi wa darasa moja ni milioni 20. Naiomba Serikali iliangalie hizi kupanda kwa bei ili isikwamishe utekelezaji wa hizi pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli katika suala zima la mwaka wa fedha huu unaoendelea, kama ambavyo amesema Mheshimiwa Waziri, mchango wa trilioni moja na bilioni 300 kuchochea uchumi katika maeneo mbalimbali. Mkoa wetu wa Pwani umepata zaidi ya bilioni 17, haijapata kutokea. Kwa hiyo, naomba nimshukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hasa sekta ambazo zimeainishwa ni zile zinazompa fursa mwanamke kupata muda wa kujishughulisha na masuala ya uchumi. Imeshughulishwa sekta ya maji, mitambo ikinunuliwa na visima vikichimbwa maana yake wanawake watapata fursa ya kujishughulisha na shughuli za uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kukushukuru kwa kunipa fursa. Lakini niseme tu kwamba…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa, kengele ya pili imegonga.

MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)