Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2022/2023. Kwanza nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipatia nafasi hii.
Pili, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri sana anayoendelea kuifanya kwa Nchi yetu ya Tanzania. Mwenyezi Mungu amwongezee maisha marefu. Amina. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kwenye vipaumbele vya Mwongozo wa Mpango huu ambao tunauongelea na sana sana nitajikita kwenye vipaumbele viwili kati ya vipaumbele vitano. Navyo ni vile vipaumbele vinavyogusa kilimo. Nitaongelea kilimo tu. Nikisema kilimo ni zile sekta ambazo ni kama hazipewi kipaumbele, kwenye kilimo naongelea kilimo, uvuvi pamoja na mifugo. Hizi sekta ni za uzalishaji, lakini ukiangalia kwa kweli hazipewi kipaumbele na ningependekeza kuwa kwenye Mpango unaokuja zipewe kipaumbele namba moja kwa umuhimu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiongelea kilimo, wananchi wote asilimia 100 wanategemea kilimo kwa upande wa chakula, nyote humu ndani mmekula, kama hujala utakula, hiyo yote ni kilimo. Wafanyakazi wanakula, wananunua chakula kinachotoka shambani, hiyo yote ni kilimo. Asilimia 66.3 ya Watanzania wanategemea kilimo kama ndiyo ajira yao na ndiyo uchumi wao, lakini bado hatujakipa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikija kwa upande wa asilimia kwa kukua kwa kilimo ni asilimia tatu mpaka nne tu, hii kwa kweli inasikitisha kwa sababu kwa nini! kwa sababu hakuna uwekezaji, lakini tungekuwa tunawekeza kwenye kilimo kingekuwa na chenyewe kinakua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo chetu kinachangia asilimia 26.9 ya pato la Taifa, lakini bado hakipewi kipaumbele. Naomba mwaka huu katika Mpango huu na kwenye bajeti inayokuja ya 2022/2023, kipaumbele namba moja kiwe kilimo. Tukiweza kuwakwamua wananchi wetu wanaoishi huko vijijini na mijini wanaotegemea kilimo, ndiyo tutaweza kutoa umaskini na kuleta ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi humu Bungeni wanawakilisha asilimia kubwa ya wakulima huko wanakotoka kwenye majimbo yao. Wabunge wengi humu ndani zaidi ya asilimia 60 na wenyewe ni wakulima. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuungane na Serikali, tuiambie Serikali kilimo iwe kipaumbele namba moja, ndiyo tutaweza kuondoa umaskini na kuweka ajira kwa Watanzania wetu na vijana wengine na akinamama ambao tunategemea kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa nini? Maazimio ya Malabo, tuliazimia kuwa asilimia 10 ya bajeti nzima iende kwenye kilimo, lakini sasa sisi bado hatujafika popote kwenye maazimio haya ya kilimo, bado bajeti ipo chini.
Naungana na Kamati ya Bajeti kwa mambo yote waliyoyasema kuhusu kilimo. Hongera sana kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Wajumbe wa Kamati ya Bajeti kwa mambo yote waliyoyaongelea. Wameongea na Kamati yangu ya Kilimo nikiwa Mwenyekiti I declare the interest, tumeongea kuhusu mambo ya Bajeti, kuwa bajeti ya kilimo iweze kupandishwa. Bajeti ya kilimo kwenye upande wa Kamati ya Bajeti ambayo nimeisifia na kuipongeza, wamesema Bajeti itoke kwenye bilioni 250 ya mwaka uliopita iweze kufikia angalau bilioni 450. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati yangu na mimi mwenyewe, nasema bado na hiyo ni kidogo, iweze kupanda zaidi ya hapo, ikiwezekana iende kwenye bilioni 500 kwa kuangalia Mpango wetu ambao unategemea kuwa mazao ya kilimo ndiyo yanalisha na viwanda, malighafi za kilimo ndiyo zinazolisha viwanda vyetu. Sasa tunasema twende na dhima hiyo ambayo inasema kuwa tuweze kuwa ina viwanda, lakini je, viwanda vitatoka wapi kama hatuna mazao ya kilimo? Lazima tuweke kipaumbele kwenye kilimo kwenye uzalishaji, uzalishaji ndiyo namba moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mambo haya ya uzalishaji kuna mambo mengiā¦
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Sijui hiyo ni kengele ya pili au ya kwanza.
MWENYEKITI: Ya pili.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, lakini kubwa ninalosema, bajeti ya kilimo ipandishwe juu, ndiyo tutaweze kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)