Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Muleba Kaskazini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia mada iliyopo mbele yetu. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu, lakini niipongeze Mamlaka, niipongeze Serikali kwa jinsi tulivyoweza kupita kwenye rejea mwaka mzima, wakati nchi nyingine zina uchumi hasi, sisi tumekuwa na uchumi chanya. Watu wanakula, kazi zinafanyika, hili ni jambo kubwa sana, inatosha kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie kuchangia kwenye kuboresha vipaumbele vya Mpango na nini tufanye. Jambo moja tunapaswa kufahamu, huu ni Mpango wa Mwaka wa Pili katika miaka mitano ya Mpango wa Tatu wa miaka mitano mitano. Tatizo la miaka mitano hii, ndiyo miaka mitano inayokwenda kutupeleka kwenye kilele cha Dira ya Taifa. Sasa tatizo tulilonalo, yaani ndiyo tunafika fainali hivyo, tunafika fainali ambako tunategemea kuwa tumeondoa umaskini, ile biashara ya income ya per capita ya Dolla 3,000, lakini tunafika finali katika linge lengo la kujenga uchumi imara wa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unapozungumza kuondoa umaskini ina maana unalenga uchumi jumuishi, wengine wanaita uchumi shirikishi, hapo mimi Kiswahili kinapingana. Uchumi jumuishi, yaani tunataka tufike kwenye uchumi wa kati, Watanzania wote tusiwe tumeachana sana, siyo kushiriki. Unaweza kwenda kwenye harusi ukamwona bibi harusi kule umeshiriki, lakini kujumuika ni kumtunza na kuhangaika naye yule bibi harusi, hapo umejumuishwa. Sasa kuwajumuisha Watanzania wote, lazima Watanzania wote washirikishwe, wajumuike wapate huo uchumi, ndipo inapokuja tatizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia dhima ya Mpango wa Pili wa Miaka Mitano ulilenga kwenye miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi. Ndiyo hii sasa Mheshimiwa Waziri ameibeba tena ikawa vipaumbele vya Mpango wa Tatu. Vipaumbele vya Mpango wa Tatu vilipaswa kulenga zaidi shughuli za kiuzalisha (the productive sectors) hajazizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipotoka, huko nyuma sawa kwa sababu miradi haikukamilika, sawa aje nayo, lakini sasa anapofika hapa kuna wenye shughuli, tunajenga reli, reli inapaswa isafirishe bidhaa, isafirishe maziwa, yapo wapo? Inapaswa isafirishe matunda, yako wapi? Kwa hiyo lazima productive sectors ziweze kushughulikiwa na productive sectors ndizo zitatengeneza ajira, ndiyo zitalisha viwanda na ndiyo zitajenga uchumi wa nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyeki, unapozungumza uchumi imara, unazungumza uwezo wa nchi kuuza nje. Tanzania tuna mapungufu yetu tunapaswa tuyaangalie, kama walivyosema Wabunge wengine kwa kujilinganisha na nchi nyingine. Wamezungumza Uganda, kahawa Uganda wanauza Dola milioni 500 kwa mwaka, sisi 135, lakini sisi tuna potential, tuna ardhi tunaweza kwenda juu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri katika Mpango wetu unapokuja tutengeneze jedwali la kuangalia kila sekta inaweza kutuletea nini. Hatari tuliyo nayo, mapato yetu ya Taifa kwa fedha za nje kwa kiasi kikubwa inategemea uziduaji. Two third ya mapato yetu yanategemea dhahabu na madini ambayo ni hatari, ni kipato kwa Taifa, lakini siyo jumuishi. Kwa hiyo tunapaswa tuwekeze kwenye shughuli za ujumuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu. Jambo la kwanza kwenye Sekta ya Mifugo, lazima Serikali iwekeze zaidi katika kuhakikisha kwamba wafugaji wanaacha kuhamahama. Huwezi kujenga Sekta ya Nyama na Maziwa kwa watu wanaohamahama na ili kudhibiti hilo lazima Serikali iweke fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwa upande wa kilimo, sisi Tanzania tuna hekta milioni 29 zinazofaa irrigation na tunalima 0.4 million hectors, Serikali wawekeze, waweke fedha, kama Mwalimu Nyerere alivyojenga Mbarali, waweke fedha nyingi watu walime halafu wawaachie, halafu watengeneze Mfuko wa kuwalipisha wale watu ili tuachane na kilimo cha kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu kitu kingine, ningependa nishauri, limezungumzwa suala la mbolea litatusumbua sana. Nimewahi kulizungumza, naishauri Serikali, juhudi za kuweza kutengeneza Kiwanda cha Mbolea lisisubiri, achana na visima vyenye well and bottleneck, waende wakachimbe visima vingine. Bahati nzuri Sekta ya Nishati naona wamewarudisha wakongwe wa mafuta akina Mzee Halfani wanarudi, wanajua gesi ilipo, waende kuchimba visima tutengeneze gesi, hii bei itapanda na kushuka na kupanda na kushuka ndiyo historia ya gesi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nalifurahia, Serikali wameanza kuzungumza suala la Bagamoyo, wamefanya kazi ya Bagamoyo, waizungumze, siyo siri, tuzungumze Bagamoyo kama Industrial City, tuzungumze Bagamoyo kama Bandari, tuzungumze Bagamoyo kama Logistic Centre. Wamezungumza suala la DRC Congo kwamba Tanzania mnataka kuwa njia, unapotaka kuwa njia lazima uwe na uwezo wa kupokea Panama Versal, uwe na uwezo wa kupokea meli kubwa ziweze kuja hapa. Nalipendekeza hilo waliangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi mwingine ni mradi wa ajira. Ziko nchi duniani zimeendelea kwa kukopa na kuwaajiri watu. Hizi Sekta za Uzalisha, Productive Sectors hazina wafanyakazi, tusione aibu kwenda kukopa. Jambo moja la faida, Productive Sectors ukikopa ni malipo ambayo utayaona katika kipindi kifupi. Ukichukua model ya Swaziland ambao wana ng’ombe laki sita, sisi tuna ng’ombe milioni 33.9, wao wanapata Dola milioni mbili Dola export kwa extrapolation sisi tunaweza kupata Dola karibu milioni 150.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukiwekeza kwenye sekta hizi unakopa na katika kipindi kifupi unaweza kupata mapato. Kwa hiyo, pamoja na hii miundombinu wezeshi na saidizi, sasa tunapaswa kutupa kwenda kwenye Productive Sectors. Hata hivyo, jambo la muhimu twende tukope, tuajiri watu, watu wafanye kazi. Kwa sababu watakapofanya kazi utaweza kupokea zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mengine nitawasilisha kwa maandishi. (Makofi)