Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Iringa Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Mpango huu wa mwaka 2022/2023. Pia nami niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kuendelea kumshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo anajali sana hali za wananchi wetu, hasa kwa kuangalia kuwekeza kwenye elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara. Tunamshukuru sana na tunamwombea Mungu aendelee kumpa afya na hekima katika kuliongoza Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapomshukuru Mheshimiwa Rais naomba pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha anapoandaa hii Mipango, kwa kuwa Mama sasa ameshafanya lile jukumu lingine ambalo lilikuwa ni madarasa na sehemu nyingine, kwenye afya na vituo vya afya, basi awe anatuletea pia na taarifa ya yale mengine tuliyoyapanga sisi wenyewe humu ndani, yanakwenda vipi? Zile chenji za fedha ambazo zingebaki au zilitakiwa zitumike, hazijatumika, zimeendaje? Tunaomba hilo tuwe tunaambiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Waziri wa Fedha awe anatuambia pia, katika Mpango huu aliousoma na Kamati ya Bajeti imeelezea kwamba, kuna wakati fedha hazikupelekwa MSD kwa sababu ya wizi uliokuwa unatokea pale MSD. Basi tuwe tunapewa pia mrejesho, chenji, wakati ule walipozuia zisiende; zile ambazo zilizuiwa ziko wapi? Au zimefanya nini? Itakuwa ni vizuri sana tukijua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuchangia Mpango huu, moja kwa moja kwanza, nichukue fursa hii kuuelezea Mpango wenyewe na kuangalia kwamba Mpango huu ndiyo mwanzo, ukiwa ni mwendelezo wa Mpango wa Miaka Mitano ulioanza mwaka 2016/2017, ambao unaisha mwaka 2021 na sasa tunaingia Mpango mwingine wa Miaka Mitano. Katika vipaumbele vya ule Mpango wa nyuma, mojawapo ilikuwa ni kukuza uchumi na kuendelea kujenga msingi wa uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapoongelea msingi wa uchumi wa viwanda, huwezi kuacha miundombinu ya barabara, miundombinu ya umeme, vile vitu ambavyo vitachochea kukua kwa uchumi. Sasa nimepita katika Mpango na tuna miradi yetu ya kimkakati na tuliposema ni miradi ya kimkakati, maana yake ni miradi ile ambayo inajenga msingi ambao utakuza uchumi wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunasema miundombinu ya barabara, miundombinu ya reli na mambo ya umeme. Sasa tuna barabara na tuna miradi ya kimkakati ambayo sehemu nyingine ilikuwa inatupelekea kuingiza mapato zaidi au kuongeza pato zaidi la Taifa ambalo lingeweza kufufua sekta nyingine za viwanda. Kwa hiyo, tuna barabara kwa mfano, tuna miradi ya utalii kama ambavyo katika Mpango wake anasema; kukuza utalii ili kuongeza pato la Taifa na tunajua Ilani ya CCM inatutaka tuongeze pato la Taifa kufikia dola bilioni sita ifikapo mwaka 2025. Pia tuongeze watalii wafike milioni tano ifikapo mwaka 2025 na tunategemea sana kutanua uwanda wetu wa utalii ikiwepo utalii Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mbuga kubwa ambayo ni ya pili Afrika ambayo ni Ruaha National Park. Tunaposema utalii wa kusini, unachukua Mikoa yote ya Kusini. Tunaiona Katavi, tunaangalia Kimondo cha Songwe, tunaangalia Njombe Kitulo, tunaangalia Selous, tunaangalia ule utalii wote wa kusini pamoja na Ruaha yenyewe. Sijaona kama Serikali imeweka kwenye Mpango suala la kutengeneza barabara zinazoingia kwenye ile Mbuga. Zaidi sana naona shilingi bilioni 90.2 ambayo itashughulika na miundombinu kufidia hasara zilizotokana na Uviko kwenye Mashirika yale yale ya Utalii kama TANAPA na wengine, lakini hatuoni Mpango ukituambia kuna kutengeneza zile barabara zinazoingia kwenye ile Mbuga ili watalii wanapofika waweze kuingia kwa urahisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna barabara ile kuanzia Iringa, kilomita 104 kuelekea Ruaha. Tuna barabara nyingine ambayo inaanzia Iringa pia inaingilia Idodi Jimbo la Isimani huko. Hatuoni kama Serikali ina Mpango, zaidi sana waliweka Mpango wa kutengeneza madaraja. Sasa tunatengeneza madaraja wakati sehemu nyingine za barabara ni mbovu. Hii ni miradi ya maendeleo ambayo ingechochea uchumi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine, tunaishukuru sana Serikali kwa namna ambavyo inaonyesha uchumi wetu wa Tanzania, pamoja na athari za Uviko bado uchumi wetu umekua chanya. Tusipojiangalia, sisi ni nchi mojawapo katika nchi 11 zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakua kwa chanya. Nchi nyingine zote 33 zinakua hasi, ukiondoa Gabon na ile Afrika ya Kati ambayo uchumi wake ni zero. Sasa tusipojiangalia tulikuwa tunakua uchumi chanya, lakini tutakuja kupitwa na wale waliokuwa na uchumi hasi, kwa sababu ya (nitumie neno lile lile) utelezi ambao tunauweka wenyewe kwenye mipango yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kurudia hapa ni hiki hapa; moja ya sababu kubwa ya kufanya uchumi ukue hasi au kushuka kwa uchumi imeonekana ni Uviko na sababu zilizosababisha ni kufungwa kwa uzalishaji kwenye nchi nyingi kwa jina la kuaminika ambalo lilikuwa ni lockdown. Sisi Tanzania Mwenyezi Mungu alitusaidia tukiwa na Serikali yetu mahiri na shupavu, hatukuwa na lockdown, lakini viongozi wetu walifuatilia ile misingi ya afya tukaweza kuwa salama, tukaendelea na uzalishaji na uchumi wetu ukaendelea kukua katika hali ya kuwa chanya, siyo hasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine kilichoathiri; kwa nini sisi tulikuwa tunaendelea na shughuli za uzalishaji? Kwa sababu, kwa kawaida pia linapotokea tatizo ni fursa, ni mwanya pia wa kuendelea kiuchumi. Kama ninyi ambao mtakuwa mmejipanga vizuri mnaendelea kuzalisha, mngeweza kuwa-serve wenzenu wengine ambao walikuwa wamejifungia.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Kengele ya pili imeshagonga Mheshimiwa. Ahsante sana.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru sana. Basi naomba kuunga mkono hoja. Mengine nitachangia kwa maandishi. (Makofi)