Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Ahmed Mabukhut Shabiby

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Gairo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya mimi kuwa mmoja wa wachangiaji lakini mimi leo nitachangia tofauti na watu wengi kidogo. Mimi nataka nizungumzie habari ya watumishi wa nchi hii hata sisi Wabunge ni watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukweli tuzungumze ukweli bila ya kupepesa pepesa, hii ndiyo tutakuwa tunaisadia hii nchi, lakini kama kwenye ukweli tunaweka woga au kutozungumza ukweli wakati ukweli tunauona haifai. Sawa sawa na mtu unakaa na Rais hapa na Waziri Mkuu na Naibu Spika na Spika wanakuambia angalia yule farasi anapendeza kweli wakati wewe machoni kwako unaona yule ni punda, unatakiwa umwambie hapana huyu siyo farasi Mheshimiwa umekosea ni punda, lakini kwa ajili ya woga unasema aah! farasi mzuri kweli kwa ajili woga wako, hii hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alishawahi kusema maendeleo ya nchi yaendane na maendeleo ya watu, huwezi kufanya maendeleo ya nchi bila ya maendeleo ya watu. Leo tupo kwenye mpango wa bajeti, Mheshimiwa Waziri wa Fedha fanya maarifa yako ya aina yoyote 2022, ujue vyanzo utapata wapi sijui wapi lakini hakikisha mishahara ya watumishi inapanda wala tusidandanganyane. Nchi hii imekuwa na hali mbaya watu wamezungumza maneno mengi sana, hela zimebanwa, hela hazipo, lakini mimi katika utafiti wangu nilichokuja kugundua bila ya watumishi kupandishiwa mishahara hali itazidi kuwa mbaya kwa watu wote, kuanzia hao machinga, makulima na watu wengine wote watakuwa na hali mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wengi ambao wakipewa pesa na inaweza ikasambaa kwa wananchi ni watumishi peke yake, huo ni ukweli wala tusidanganyane! Leo watumishi miaka sita, saba hawajaongezewa mishahara mnategemea hela hiyo itakuwepo mtaani wakati vitu vimepanfa bei lakini mishahara ipo pale pale? Haiwezekani! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo mnaongeza vi-percent viwili, vitatu, hakikisheni Serikali mnakuja na mpango muangalie mapato mtapata wapi, tumewaambia mapema mhakikishe watumishi wanaongezewa asilimia kubwa ya kutosha ili waweze kukidhi, watumishi ndiyo watumiaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi akitoka hapa anaenda Dar es Salaam njia nzima atanunua, akitoka hapa atanunua karanga, akifika Gairo atanunua viazi, akifika Dumila atanunua mahindi, akifika Mikese mpaka aje afike nyumbani laki moja kishapoteza, hawa ndiyo wanaosambaza pesa, ukienda hata sehemu za starehe ni watumishi ndiyo wanasambaza pesa! Watumishi wakiongezewa pesa mjue kila kitu kwenye hii nchi kitakaa vizuri na pesa itaonekana, hii lawama ya kwamba pesa haipo mifukoni mwa watu, tusidanganyane eti Wakandarasi hawajalipwa, Mkandarasi nikiwa mimi Shabiby ukinilipa hiyo hela yangu ya kuchezea nitagawagawa kwa kila mtu, nina wafanyakazi kumi hadi kumi na tano, watumishi wapo wangapi? Halafu tuangalie kodi ya nchi hii asilimia kubwa inalipwa na nani kati ya wafanyabiashara na watumishi, wanaolipa asilimia kubwa ni watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hii naomba sana kwenye bajeti yako, Mheshimiwa Waziri wa Fedha tunajua Mama yetu aliahidi lakini tumekupa mapema ili uangalie na vyanzo vyako utakavyovipata mishahara ipande asilimia ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la Machinga alichozungumzia Ndugu yangu Mheshimiwa Musukuma, naungana na Serikali katika mipango ya kuweka mji vizuri sana, kweli mji unapendeza vizuri lakini tukumbuke hawa machinga nao wakiwekewa mazingira mazuri wanaweza wakaleta mapato makubwa sana kwenye hii nchi, ni mazingira tu! Hivi leo mimi najiuliza hii Serikali hawa watu wataalam wetu wa Serikali wanapokwenda Vyuo Vikuu huwa wanaenda kule kujifundisha kumwagilia maua kwenye bustani au utaalam? Maana yake hata huelewi mtu ana akili timamu unaenda kupeleka majengo ya machinga kule Ilala ndani Shaurimoyo, kuna kibarabara kimoja hata mahali pa kufika hakieleweki, hamna stendi ya daladala unampeleka mtu kule, nani anaweza kufanya biashara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kuiga nchi nyingine zilizoendelea? Dunia nzima tuangalie hata tuende pale Nairobi, majengo yote yaliyopo mijini ni ya Serikali, tukitoka hapo majengo yote ya National Housing yalikuwa ya Msajili wa Majumba haya yote ya kwetu, ukiangalia yale majengo makubwa ukichukua kodi wanayochukua Serikali lile jengo zima labda utachukua milioni Mbili au Milioni Tatu, lakini ukiyavunja yale majengo ya mjini hapa kama pale mtaa wa Congo, Msimbazi mpaka kule anakozungumza ndugu yangu hapa Musukuma, ukivunja yale majengo yale ya Serikali ujenge Malls tena Shopping Malls za ghorofa hazina gharama kwa sababu Malls zipo waziwazi halafu waingize watu.

MBUNGE FULANI: Au jangwani.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, au jangwani kokote pale, ndani lakini katikati ya Miji siyo ukampangie mtu huko katikati ya miji, hivyo mtaingiza machinga wangapi? kwa hiyo ni lazima kuwe na mipango tuchukue haya majengo ya Serikali tufanye kama Guangzhou - China, tufanye kama Dubai, tufanye kama nchi zingine, tuvunje yale majengo ya Serikali. Serikali ni yetu, Serikali ndiyo yenye machinga, Serikali ndiyo yenye watu wake, tuwajengee kwenye Miji katikati siyo kuziba barabara hapa, eti umchukue machinga ukamuweke sijui wapi huko hakuna hata stendi ya daladala nani atakaekwenda kununua? Unajua kuna vitu vingine tuzungumze ukweli siyo Mkurugenzi anapanga tu hapa ndiyo penyewe nimewajengea choo, sasa mtu anataka choo ataenda kuomba tu akibanwa huko hata porini ataenda, watu wanataka kupata huduma na wanaotaka kutoa huduma nao wanataka nao kufata watoa huduma na wapate faida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ushauri wangu ni kuhakikisha pale Msimbazi hebu angalieni majengo yale yote ni ya Serikali National Housing, ukienda kule mjini kote ni majengo ya Serikali, hivyo kweli wanaambulia tu kupata milioni mbili, tatu watu wamekaa kule majumba yenyewe kupiga rangi wanashindwa, vunja yale weka Malls, weka ghorofa mbili, tatu, nne tena haina gharama kabisa, halafu machinga wakae mle, hapa msimbazi watakuwepo machinga, hapa sijui Lumumba watakuwepo machinga, hata katikati ya mjini kule karibu na hii station yetu ya railway tunayoijenga watakuwepo wamachinga, watu wata-enjoy, lakini hii kufukuzana halafu mpango hamna! Mimi nimeamua kutoa mpango kabisa ili kuelekeza mpango uweje sitaki kulalamika.(Makofi)

MBUNGE FULANI: Na mishahara ya Wabunge!

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwingine hapa anasema mishahara ya Wabunge, hiyo utasema kesho hamna wasiwasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukweli ndiyo huo. Lingine, kabla dakika zangu hazijaisha, kweli watu wanajitangaza tu tunatoa mikopo kwa wakulima, kuna Mheshimiwa alizungumza hapa nafikiri, Mheshimiwa Almasi alizungumza kwamba zinajitoa benki na Mheshimiwa Waziri unaangalia na wewe tunakuamini sana na tunajua utalifanyia kazi. Hizi zote zinakopesha matajiri…

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha Mheshimiwa Shabiby…

MHE. AHMED M. SHABIBY: Ah?

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha.

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nipe dakika moja tu nimalizie.

MWENYEKITI: Muda wako umekwisha!

MHE. AHMED M. SHABIBY: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya, naunga mkono hoja.