Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Halima James Mdee

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii. Nikiwa sehemu ya Wajumbe wa Kamati ya Bajeti nitachangia mambo kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, Kamati ya Bajeti imependekeza kwamba Shirika letu la Ndege (ATCL) liangaliwe ili liweze kuboreshwa zaidi ili liweze kufanya kazi kwa ufanisi. Lakini nikiwa naunga mkono hiyo hoja nitazungumza mambo kadhaa kwa sababu lazima tujue tulikotoka ili kuweza kujua tunakwendaje mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyozungumza sasa ATCL ina madeni yenye thamani ya bilioni 472, thamani ya mali za ATCL ni bilioni 256. Tafsiri yake ni kwamba ATCL ina mtaji hasi wa shilingi bilioni 216. Na unapokuwa na mtaji hasi tafsiri yake ni kwamba umekufa tu lakini upouopo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kingine, malengo ya biashara ya ATCL wakati tunaifufua, na watu tulizungumza tukasema tunaingiza fedha lakini wakati tunaingiza hizi fedha nyingi lazima tuhakikishe shirika liko tayari, Taifa liko tayari, wananchi wako tayari. Zikapigwa porojoporojo hapa, mambo yakaenda, tumefika hapa tulipo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo yalikuwa bilioni 600, malengo ya kibiashara, kutengeneza, wamefanikiwa bilioni 157; asilimia 24 tu ya lengo. Naunga mkono tui-boost, tuifufue, sikatai, ila lazima tujue tulitoka wapi, tumeteleza wapi, tunakwenda wapi na tusifanye maamuzi yanayohusu pesa za Umma kimihemkohemko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa 2015/2016 – 2021/2022 malengo kwa ATCL peke yake ilikuwa ipewe trilioni 3.39, mpaka sasa imefanikiwa kupata trilioni 1.9 kwenye hiki kipindi cha miaka mitano. Sasa nikiwasikiliza ndugu zangu hapa wanazungumza kilimo, mkongwe hapa, tumepiga hizi sound za kilimo tu kwenye mipango, tumezipiga yaani hawasikii. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kilimo ambacho tunajua kinachangia asilimia 26 ya GDP, Pato la Taifa, yaani kwenye zile trilioni 163, kilimo anachofanya mkulima mmojammoja kwa support kiduchu ya Serikali inachangia trilioni 44. Tumeipenda sana tumeipa bajeti 294, ukija utekelezaji utakuta wamebajeti bilioni 100, ikizidi sana bilioni 60. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ndugu zangu hawa wa ATCL wamepigwa trilioni zao 1.9, ukiuliza hivi inachangia pato la Taiifa kiasi gani, sidhani kama asilimia moja inafika. Kuna wenzangu na mimi hapa walikuwa wanajifanya, oh, wanaleta watalii; ndege gani ya ATCL inatoka Mpanda inaleta watalii Bongo? Nendeni Kilimanjaro pale, nendeni huko Mwanza muangalie kuna ndege gani ya ATCL inaleta Wazungu kutoka Ulaya kuja Tanzania kwa utalii? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia safari za ndani ufanye analysis ujue kama hizi ndege zina mchango kwenye utalii. Nazungumza tujitathmini. Tujitathmini. Sina nia mbaya. Kwa sababu midude iko hapa, yalikuja 11 yameshalipiwa mengine sasa hivi tunaambiwa 16 halafu hadi kuelekea ule uchaguzi zitatimia 19. Yaani hili ni eneo pekee ambalo mtatekeleza bajeti kwa asilimia mia lakini output ikoje, productivity ipo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima na taadhima, hili shirika tunavyozungumza limepewa asilimia 600 ya bajeti ya kilimo kama ikipelekwa kwa ukamilifu. Hebu tujiulize tu, hiki kilimo hiki kingepewa hata trilioni moja, ingekuwa boosted kwenye mifumo ya umwagiliaji. Hatusemi muwape hela mfukoni, wakulima wetu wanahitaji miundombinu wezeshi, wanahitaji kupewa channels za masoko. Kupanga ni kuchagua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi mna-enjoy nini kwa mfano. Ndiyo, tuna ndege 19, taarifa ya ATCL wenyewe wanatuambia eti wanahudumia abiria 60,000; halafu eti wamepungua kwa sababu ya Covid mpaka 11,000 halafu watu wazima tunakaa hapa tunapitisha mpango. Tumetoka kulipa bilioni 500 juzi, ndege nyingine mpya tano. Hatuoni aibu, tupo tu, hatuoni aibu.

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu… msinichanganye jamani, acheni nina uchungu.

MWENYEKITI: Ni upande gani hiyo taarifa? Endelea, nakuruhusu. Nimekuona Mheshimiwa Shigongo.

T A A R I F A

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumpa taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Mdee, namheshimu kwa sababu ni mtu anayeelewa vitu vingi lakini natofautiana naye sehemu moja tu; katika biashara kuna suala linaitwa trading na investing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapo-trade unachukua kitu unauza na unapata faida immediately, tunapozungumzia investing kuna incubation period ya kusubiri ndiyo uanze kupata faida. Itachukua muda ATCL ianze kutupa faida, lakini finally ATCL will pay. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya ndege siyo trading ni investing. Let’s be patient, ATCL itatulipa. (Makofi)

MWENYEKITI: Taarifa hiyo unaipokea Mheshimiwa Halima?

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shigongo naye anajua biashara mwenyewe hayuko vizuri sasa hivi, kwa hiyo atulie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni nini? Sipingi ndege kununuliwa, napinga maandalizi. Nitawasomea kitu kimoja hapa, taarifa ya ATCL wenyewe, wanasema hivi; Serikali inakabiliwa na mashauri ya kesi zilizokwishaamuliwa mahakamani, utekelezaji wa maamuzi ya kesi hizo haujafanyika na hivyo madeni haya yanaweka mali za Serikali katika hatari ya kukamatwa kwa ajili ya kukazia utekelezaji wa hukumu. Hatari hii inafanya tuogope kupeleka ndege zetu nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu fikiria sisi watu wazima tumenunua ndege, tumetumia trilioni 1.9, tunaogopa kulipa madeni ya kesi za Wazungu huko kwa hiyo ndege tuko nazo nyumbani. Hivi hizo ni akili ama nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema tunapenda sana shirika letu changamoto iliyopo kulikuwa hakuna business plan, ndiyo maana leo madeni ya ATCL mwaka 2014 ilikuwa ni bilioni 74, ilikuwa haifiki hata milioni 100 mwaka 2014/2015, leo bilioni 400 pamoja na ku-inject 1.9 trillion, hivi hamuoni?

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia, wanao mtindo wa kuninyima michango yangu nikichangia, ninashtaki kwako leo ili wanipe, tunasaidia Nchi jamani hatutafutani mchawi hapa. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)