Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kalenga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru hata na mimi kunipa nafasi ya kuweza kuchangia jioni ya leo katika mapendekezo haya ya mpango wa bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa ufupi tu kumshukuru Rais kwa kazi kubwa anayoifanya, tumtie moyo kwa hatua kubwa ambazo ameweza kuzifanya, hata pia kukaribisha uwekezaji na kufungua milango, najua nchi itakwenda kufunguka kwa mapana yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia sehemu ya kilimo, kama ulivyosema twende moja kwa moja. Kwa kweli na mimi ninataka nizungumzie kidogo habari ya kilimo. Tukiangalie kweli kilimo, kama Serikali kwa kweli tumekuwa na mipango mingi lakini tumeitawanya mno, kama tunasema kwamba kilimo kinachukua asilimia 66 ya Watanzania wote, basi kwa kweli tuwe na mikakati ambayo baadae itaweza kutuletea matokeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikizungumzia habari ya ruzuku bado na mimi naona kuna umuhimu wa Serikali kuweka ruzuku kidogo kwa sababu nikiangalia hali ilivyo huko sokoni kwa maana hasa ya pembejeo, kuna sababu ya Serikali kuangalia katika mpango huu. Ruzuku siyo jambo geni, ukiangalia nchi ambazo zinaongoza duniani kwa ruzuku, kwa mfano anasema Ufilipino na Indonesia wao kwenye Pato lao lile la Taifa wanaweka asilimia 3.1. Lakini ukiangalia kwa mfano India asilimia 25.1 ya fedha zote zinazokwenda kwenye ruzuku kwa maana ya kwenye madini, ujenzi, miundombinu, wao asilimia 25 inakwenda kwenye kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiangalia Marekani pia kwa miaka minne tangu mwaka 2017 mpaka kufika 2020 walianza na dola Milioni Nne na sasa wamefika dola Milioni 20 wakiongeza ili kuweza kufidia yale mapungufu ambayo yametokea kwenye kilimo na sababu ni kwamba ni lazima kuweza kuboresha uchumi wa nchi unaotokana pia na kilimo kwa sababu pia ni lazima tule, lakini pia inasaidia kuweza kuboresha bei, kuhakikisha kwamba bei zinaendelea kuwa imara na wakulima wanapata kipato chao. Kwa hiyo, Serikali hili iliangalie kwa huruma yake. Najua inafanya mambo mengi lakini na hili la ruzuku iangalie ili mwakani tusiingie kwenye baa la njaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi haina shida ya chakula, kwa mfano ukiangalia sasa mahindi ni mengi, lakini shida tuliyonayo ni masoko. Sasa suala la masoko hili ni muhimu sana. Ukiangalia Nchi ndogo kama ya Swaziland ambayo wana ng’ombe kama laki sita, unakuta wao wana mikataba na nchi za Ulaya, wanauza nyama nyingi kuliko sisi ambao tuna ng’ombe milioni karibu 33.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa walichofanya ni nini ni kusiani bilateral agreements, yaani mikataba ya nchi na nchi ya kufanya biashara, lakini sisi ni nchi kubwa tumeshindwa kusaini mikataba ile fungamanishi na nchi mbalimbali ambazo tunaweza tukafanya biashara kubwa zinazotokana na kilimo. Kwa hiyo hilo nalo ni la kuliangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu nyingine ambayo nilitaka kuangalia ya kuongeza mapato kama ulivyosema, nilikuwa nafikiria hapa kwenye upande wa transfer ya properties, hasa majengo na viwanja. Eneo hili unakuta kwamba kuna pesa nyingi sana ambazo zimeendelea kushikiliwa. Ninaishauri Serikali kwamba ikiona inafaa tunaweza tukapunguza ile asilimia 10 ya transfer ikaenda asilimia tano, siyo lazima iwe ya kudumu, inawezekana tukafanya kwa mwaka mmoja wa bajeti, labda mwaka tu mmoja wa bajeti tukasema kwamba tunapunguza asilimia tano ili tuchochee watu ambao wana mali ambazo hazihamishiki wakahamisha maana ni eneo lingine ambalo pia Serikali inaweza kupata mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia habari ya kuongeza gati, kwa mfano pale bandarini. Sasa uchumi wa mbogamboga, matunda, ni uchumi ambao unakua sana duniani. Sababu kubwa ambayo Tanzania tumekuwa tukishindwa kupata soko kwenye hili eneo la uchumi ni mazingira yetu katika bandari zetu. Kwa mfano, ukiangalia Bandari ya Mombasa, wao wana cold rooms - hivi vyumba baridi, zaidi ya 1,000 kama 1,200 na kitu. Lakini ukiangalia kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam nimesikia kuna mia na kitu, yaani hata mia mbili hatufiki. Sasa eneo hili pia Serikali ni lazima tuliangalie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunataka huu uchumi wa mbogamboga na matunda uweze kukua, na ni eneo kubwa linalokuwa duniani, ni lazima tuangalie namna gani tunavyopanua bandari zetu, basi na hizi cold rooms, hivi vyumba baridi vya kuhifadhia mazao vijengwe kwa wingi kulingana na hali halisi ya soko. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia hatuwezi kujenga, kuweka mipango ya maendeleo ya uchumi bila kuangalia mazingira. Tukiangalia mazingira duniani hali ya mazingira imekuwa mbaya, yaani hata hapa Tanzania mazingira yameharibika sana, nimemsikia Mheshimiwa Rais akiwa Glasgow kwenye mkutano wa mazingira anasema kila mwaka tunapanda miti Milioni 276 ni taarifa nzuri Watalaam wanampatia lakini Je, nikiangalia reflection ukitembea huku Dodoma na Iringa ukiangalia kwa macho yako hiyo miti Milioni 276 kwa mwaka unaiona? Kwa hiyo, inawezekana wakati mwingine hawa Watalaam wanaotoa ripoti, sisemi wanaandika siyo zenyewe lakini ukiangalia misitu inavyoteketea, Je, misitu uteketeaji wake na hii miti tunayopanda vinawiana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mnavyokwenda kuangalia suala la maendeleo lazima suala la mazingira tuliangalie kwa ukaribu sana, ni muhimu sana na hili mimi kwa vile pia ni mpenzi wa mazingira siku zijazo nitakuja...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ni kengele ya pili.
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Basi naunga mkono haja. Nilijaribu kwenda haraka, nilifikiri nitamaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.