Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi ya kuchangia Mpango wa Maendeleo. Nitajikita kwenye mambo mawili, jambo la kwanza litakuwa sekta ya kilimo, lakini pia nitazungumzia suala la umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kwenye sekta ya kilimo ambapo hata Mjumbe aliyepita ameishia. Kwanza niipongeze Serikali kwa kazi ambayo inaendelea na kwa mpango ambao imeusoma, lakini nataka kuzungumzia kilimo kwenye mambo ya mabenki, sekta ya mabenki ndani ya Taifa letu, jinsi ambavyo yana wajibu wa kuchangia kwenye kilimo lakini tumekwama hapo kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo ndicho kinachoongoza kwenye pato la Taifa kwa asilimia 26.9 kama ambavyo kwenye Mpango inaoneshwa, lakini mabenki ya Taifa hili ambayo tunafanya nayo kazi na yanachangiwa sana na Serikali ni moja kati ya maeneo ambayo yamekuwa yakikwamisha kilimo kwa muda mrefu kutokana na taratibu zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mabenki yanapokea mitaji kutoka kwenye Serikali yetu, lakini pia kwa kipindi hiki yamepunguziwa riba ili yaweze kuhudumia wakulima wa Tanzania na Watanzania wote. Lakini nataka nitoe takwimu chache, kwa mfano wa Benki za NMB au CRDB kwenye sekta ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2018, Benki ya NMB imekopesha wafanyakazi kwa asilimia 54, lakini kwenye kilimo imekopesha kwa asilimia 4.0 tu. Mwaka 2019, Benki ya NMB imekopesha wafanyakazi asilimia 58, lakini kwenye kilimo imekopesha asilimia 5.0 tu. Benki ya NMB mwaka 2020 kwa wafanyakazi imekopesha asilimia 65, kwenye kilimo imekopesha asilimia 6.0 tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya CRDB mwaka 2019 kwa wafanyakazi imekopesha asilimia 45, kwenye kilimo imekopesha asilimia 1.0. Mwaka 2020 kwa wafanyakazi imekopesha asilimia 48, kwenye kilimo wamekopesha asilimia 2.0.

Mheshimiwa Mwenyekiti, angalia benki za mataifa yanayotuzunguka kwa mfano Cooperative Bank ya Kenya, mwaka 2019 kwenye kilimo wamekopesha asilimia 88. Mwaka 2020 kwenye kilimo wamekopesha asilimia 91…

MWENYEKITI: Hiyo ni Kenya Commercial Bank?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naam?

MWENYEKITI: KCB?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo ni KCB. Tunakwenda ZANACO Bank, Zambia; mwaka 2019 Benki ya Zambia, ZANACO, wamekopesha asilimia 53 kwenye kilimo. Mwaka 2020 wamekopesha kwa asilimia 65 kwenye kilimo. Sisi Tanzania tunacheza na asilimia 4.0 kwa mabenki yetu yote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa tuna swali la kujiuliza, Wizara ya Fedha; ni wapi ambapo tunakwama kwenye kilimo kwenye Taifa hili? Mabenki yanatukwamisha. Wanapokea mitaji ya Serikali, wamepunguziwa riba, lakini wao wameshindwa kupunguza riba kwa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natoka Mkoa wa Njombe. Mkulima akienda kukopa anakopa kwa asilimia 17, 18 hadi 20 riba. Huyu mkulima leo ni nani atakwenda kukopa? Akienda kupeleka collateral hata ya shamba lake wanamkatalia, wanataka kuona collateral ya vitu ambavyo vinaonekana ambavyo ni vikubwa ambavyo wakulima wetu wa Tanzania wengi wanashindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Wizara ya Fedha, wapitie mchakato upya kuangalia jinsi gani mabenki yanatukwamisha sisi Watanzania kwenye kilimo. Hizi benki zinatumia mitaji ya Watanzania mingi na BOT imewaondolea riba na wao wana wajibu wa kuondoa riba kwa wakulima wetu ili waweze kupata fedha, waweze kuendeleza kilimo, tofauti na hapo tutaendelea kulia. Wenzetu wa Kenya wametuacha mbali, wanakopesha asilimia 98 kwenye kilimo, lakini sisi tumekwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umezungumza suala la mbolea hapa, natoka Mkoa wa Njombe, gunia la mahindi Makete gunia la mahindi linaunzwa shilingi 15,000, mkulima ananiuliza Mheshimiwa Mbunge ninatakiwa niuze magunia saba ili kupata mfuko mmoja wa mbolea lakini leo kwenye Mpango hatuoni makusudi yoyote ya Serikali ya kutoa dharula, yakutoa hata ruzuku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu alitusaidia tulipata kwenye mahindi bilioni 50 kwa ajili ya NFRA. Lakini bado tuna msiba hapa kwenye mbolea kwa sababu mwakani kama hatuta waokoa wakulima leo mwakani tutaingia kwenye crisis ya njaa. Kwa sababu wakulima hawawezi tena kulima, mabenki hayawakopeshi, mbolea hakuna, wanalia na mbolea tunaomba ruzuku sana kwenye hii mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba, Serikali itusikilize, itafute fedha iweke kwenye ruzuku kwa wakulima, ili wakulima wetu hawa tuwaokoe mwakani tusiingie kwenye crisis Tanzania na itakuwa ni aibu, Taifa ambalo tuna ardhi ya kila kona lakini leo tunaingia kwenye crisis ya njaa kwa kukosa ruzuku kwenye mbolea hilo lilikuwa ni la kwangu kwenye Sekta ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nije kwenye Sekta ya Nishati, ukienda kwenye Sekta ya Nishati hotuba ya Waziri ukurasa wa 14, anazungumzia usambazaji wa umeme vijijini. Kwanza tushukuru kwamba ni kweli umeme vijijini umeendelea kusambazwa naonesha kwenye ripoti mmetumia zaidi ya Bilioni 88.1 kwenye kusambaza umeme vijijini. Lakini hoja inakuja, umeme huko vijijini umewafikia Watanzania haujafikia, kwa sababu asilimia kubwa umeishia kwenye taasisi, kwenye mashule zahanati lakini ukienda kufuatilia, hapa nimefanya uchunguzi wa haraka, TANESCO, TANESCO sasa hivi hawana bajeti ya kusambaza umeme kwenye makazi ya watu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na kama Serikali inanisikiliza, ifanye sensa ya kujua ni Watanzania wangapi wamesuka umeme toka 2019 hadi leo wamekwamba kuunganishiwa umeme kwa sababu TANESCO hawana fedha. Tumewaachia REA wanatupa kilomita moja moja kuelekea kwenye Makanisa, Zahanati, Vituo vya Afya, ukishafika huko makazi ya watu ambao ni wapiga kura wa Taifa hili wengi hawana umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wamebaki kuomba nguzo kwa Wabunge, wanaomba nguzo kwa Wabunge, wanaomba angalau hawa watoe fedha maana yake wapo tayari kutoa fedha zao wanunua lakini TANESCO wamekwama hawana fedha za kwenda kusambaza umeme kwa wananchi. Na nimuombe Waziri wa Nishati afanye sensa kila jimbo, kila wilaya…

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahishwa na mchango wa mdogo wangu nataka tu kumuongezea taarifa kwamba, pamoja na kwamba asilimia 78 REA wamesambaza umeme lakini ni asilimia 18 mpaka 20 tu ya Kaya zote zimeunganishiwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika watumiaji potential milioni 11.4 waliounganishiwa umeme ni milioni 2.8 peke yake. Kwa hiyo, hali ni mbaya pamoja na kwamba tumeufikisha vijijini lakini unaingia kijijini, umeingia Kaya mbili tatu sisi tunadhani umeme umefika lakini ukweli ni kwamba namba za vijiji zinatupotosha sasa twende kwenye namba za Kaya. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sanga, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo taarifa kwa sababu ndiyo uhalisia uliopo kwenye majimbo ye tuna kwenye mikutano na Wabunge wenzangu wananiunga mkono. Kwamba hapa tu simu ambazo tunazipokea ambazo zinahusisha wananchi wakiomba kuunganishiwa umeme ni nyingi yaani Wabunge ndiyo tumegeuka TANESCO kwa sasa, wakati TANESCO wanawajibu wa kupata fedha kwa ajili ya kusamba umeme kwa Watanzania. Kwa hiyo, tusijidanganye na namba ya kwamba tumefikisha kila Kijiji lakini je mpiga kura wa Tanzania hii, mpiga kura ambaye tunamtegemea 2025 atusaidie amefikishiwa umeme? Unakuta kwamba asilimia 90 wengi hawajapata umeme na wapo tayari kuunganishiwa umeme na wapo tayari kutoa fedha zao mifukoni lakini TANESCO imekwama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naunga mkono Mpango wa Bajeti lakini natoa mapendekezo haya; waangalie mabenki kwenye kilimo, waangalie ruzuku kwenye mbolea, lakini pili TANESCO wasijifiche kwenye kichaka cha umeme kufika kila Kijiji waende wakaangalie uhalisia wafanye sensa kila Mbunge alete hapa ni Kaya ngani ambazo hazijaunganishwa umeme halafu wataona maajabu yaliyopo. Mimi Makete nikianza nina zaidi ya nyumba 2000 zimesukwa lakini umeme toka 2019 hadi leo hazijaungwanishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante ni hayo mawili tu. Ahsante sana. (Makofi)