Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia machache katika mpango huu ambao umeletwa kwetu na Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwanza naanza mchango wangu kwa kuuliza swali. Je, nchi yetu sasa ipo na uchumi upi? Uchumi wa Kati au ule Uchumi wa Kimaskini tulipokuwa kule nyuma. Nasema hayo kwa sababu kwa mujibu wa Mapendekezo ya Mpango wametueleza kwamba mwaka 2019 nchi yetu uchumi ulikua kwa asilimia Saba, lakini mwaka 2020 umeporomoka mpaka asilimia 4.8 na sababu kubwa ni ugonjwa wa Covid, sasa Covid inaendelea, lakini uchumi umeporomoka sasa tupo wapi? Tunaomba Serikali itueleze ili wananchi wajue kwamba je, tunaendelea kuwa katika uchumi wa Kati au tunarudi kule? Tunaporomoka na uchumi wetu kurudi kwenye uchumi wa kimaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopanda katika uchumi wa kati ni kwamba tunakosa hata vigezo vya kukopa mikopo ya masharti nafuu. Tunakwenda kukopa mikopo ya biashara, wamesema wengi kuhusu deni, lakini mimi ningependa kujua nchi sasa itaendelea kukopa kwa vigezo vipi? Tunarudi kule tunakwenda ku-negotiate upya ili tuweze kukopa masharti nafuu au tunaenda na mikopo ile ambayo inaiva kwa muda mfupi na ina riba kubwa na inaweza kusababisha Watanzania kushindwa kulipa kodi au baadaye kutufanya sisi tuweke miradi yetu ambayo tumekopa kutengeneza ili iwe sasa tuiweke rehani kuweza kulipa madeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujua hayo ili wananchi wajue kwamba sasa hivi tupo wapi tupo kwenye uchumi wa kati kama ilivyokuwa au tumerudi kule chini kwenye uchumi wetu tuliokuwa nao wa kimaskini. Ni maswali tu hayo nataka kujua ili na watu wengine tuelewe kwamba sasa tunakwenda mwendo upi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa vijana hapa wananiambia kwamba sasa na Bibi achangie michango, mimi kweli nachangia na sasa hivi nataka niongelee wazee. Nimegundua kwamba kwenye Bunge hili wazee tupo wengi, lakini tunanyamaza kuhusu mambo yetu yanayotuhusu. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikikupeleka kwenye kitabu cha mpango nimejaribu kukipitia ule ukurasa wa 127 nimejaribu kuchukua hiki kitu kidogo hapa ambacho nimeona walivyotuweka wazee katika Mpango huu. Ukurasa wa 127 wametuambia kwamba katika kile kipengele cha Ustawi wa Maendeleo ya Jamii kwamba kuimarisha na kusimamia utoaji wa msaada wa kisaikolojia kwa makundi mbalimbali ya kijamii yenye uhitaji hususani wahanga wa majanga, watu wenye ulemavu, wazee basi niishie hapo. Sasa mimi nikajiuliza hasa huu mpango unaenda sisi wazee kutusaidia kisaikolojia ili iweje, kwa sababu tumeshindwa kulipwa pension hatutibiwi bure, sasa mmetuweka katika hali ya kutusaidia kisaikolojia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nayasema haya kwa sababu nilichotegemea katika mpango na nilisema sana kwenye bajeti, nilitegemea mpango utuoneshe namna wanavyokwenda kutunga sheria kwa ajili ya Sera ya Wazee ya Mwaka 2003. Sera hii imepitwa na wakati. Nilitegemea kwamba mngetueleza kwamba sasa tunakwenda kutengeneza sheria ili wazee wapate backup katika mambo ambayo tunataka kuwafanyia. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapomwambia Mzee atibiwe bure akaenda kwenye dirisha akakuta hakuna dawa anakwenda kwa nani, atalalamika wapi, kwa sheria ipi, Mheshimiwa Jenista unanisikiliza hapo, hakuna sheria na tangu mwaka 2003 hii sera mmeilalia kwa sababu gani, Wazee katika nchi yetu wametupwa katika jamii sawa kwamba watunzwe na Watoto, wapo wazee ambao watoto wao hawana uwezo wa kuwatunza. Wazee wa Kitanzania wanaishi miserably kabisa katika nchi yao.(Makofi)
MWENYEKITI: Katibu hebu weka saa yako vizuri muongezee dakika mbili kwa sababu ni kweli kabisa ili Mheshimiwa Jenista amsikie vizuri, maana hapa ni kweli kabisa yaani wazee wao wameambiwa wataimarishwa na watapata msaada wa kisaikolojia katika mpango mzima huu.
Mheshimiwa Conchesta endelea. (Makofi/Kicheko)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana hawa Mawaziri ni Vijana, wanafikiri sisi hatusomi hivi vitabu, umeshatuelekeza tusome na kweli tunajipinda mimi nasoma kusema ukweli, nasoma kwanza naenda kutafuta kile kipengele cha wazee wakina Conchesta sisi wanatusemea nini?
Katika ukurasa huo huo nenda kwenye kipengele cha saba wamesema kuimarisha Huduma za Ustawi wa Jamii kwa Wazee, Watoto na Watu wenye Mahitaji Maalum, how, mnakwenda kutuimarisha vipi, kwa sababu kama hakuna kitu chochote kwenye elimu huku wamesema tutafanya hiki tutafanya hiki kwetu wanasema ni kisaikolojia na kisaikolojia mnatufanyiaje sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani nimeshangaa sana kwa sababu nchi hii imetekeleza kabisa Wazee tukubali, tunakubaliana kabisa kwamba tunapaswa jamii kutunza Wazee, lakini pale ambapo Wazee Watoto wao wamekosa kuwatunza Serikali inapaswa kuweka mkono wake. Nchi nyingine zinajenga hata majumba kwa ajili ya Wazee, Wazee wanapata matibabu, wazee hawa wanaonufaika ni wale ambao wapo katika mfumo rasmi. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru umetupa semina UTT, jana Benki Kuu tumeweza kujua lakini ni ile kada ambayo sisi tuna uwezo wa kwenda kuwekeza vipande, lakini wale waliopo huku wakulima wanateseka nchi haina mpango wowote haioneshi lolote kuonesha ni namna gani wazee wanaweza kulindwa, wanaweza kutunzwa, wanaweza kuhakikisha kwamba wanapata matibabu yao, wanaweza kuishi kwa neema katika nchi yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msitulinde kisaikolojia tu tunataka mtuambie, neno hili limenichanganya sana kwa sababu nikajiuliza sasa hivi wanataka kutufanyia psychology ya nini? Kwa hiyo kuna mipango mingine kwa kweli msiseme by the way ndiyo maana mnaona watu wanalalamikia kilimo, kilimo kinapaswa kuwepo ili watu waweze kupata chakula na Wazee na wenyewe waweze kustawi. Lakini wapo Wazee ambao bado wana uwezo wa kufanyakazi ukienda kwenye Halmashauri Vijana na Wanawake wamepewa mikopo na sheria ipo Wazee wapi na wapi?
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri wa Nchi nashukuru umesimama ufafanuzi saikolojia hii. (Kicheko)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimpe taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli anasoma kwenye mpango kipo kipengele cha Ustawi wa Wazee kwa kuwaimarisha kisaikolojia hatuwezi kukikwepa, hatuwezi kukikwepa wapo baadhi ya Watanzania ambao wanaangukia kwenye kipengele hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ningemuomba asome na vipengele vingine vya mpango ambavyo pia vimezungumzia ni kwa kiasi gani Serikali itakwenda kuangalia Ustawi wa Wazee.
Kwa hiyo, ninamuomba tu Mheshimiwa Mbunge nimpe taarifa kwamba hiyo ni sehemu moja, lakini zipo sehemu nyingine na hapo amesema yapo na mengine pia ambayo, tunaweza tukamsomea hapa na hayo mengine ambayo pia ni package ya wazee ikiwa ni pamoja na hiyo ya saikolojia kwa wale Wazee ambao wanahitaji kusaidiwa katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba tu nimpe taarifa Dada yangu. (Makofi)
MWENYEKITI: Taarifa hiyo Mheshimiwa Conchesta unaipokea?
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, siwezi kupokea, Mheshimiwa Jenista anakumbuka kwamba tulishapendekeza kwamba hata wazee wanaweza kupata hata pension ya shilingi 20,000 tu katika nchi hii sasa baadaye naona alikwepa wakati ndiye yeye alikuwa anasimama imara kutetea hiyo sera mpaka hapo kimya hakuna chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndiyo maana Wazee Watanzania wanazidi kuzarauliwa.
MWENYEKITI: Alipokuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ilikuwa ndiyo hoja, Mheshimiwa Jenista. (Kicheko)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Sasa baada ya kutoka huko kwenye Uenyekiti akaenda huko kwingine akaona Wazee awaweke pembeni hapana! Tuhakikishe Bunge hili likitetea wanawake, likitetea vijana.. (Kicheko)
MWENYEKITI: Sasa anasimamia kuwapatia huduma ya kisaikolojia! (Kicheko)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, eee!
MWENYEKITI: Amekuja kivingine sasa (Kicheko)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi naomba…
MWENYEKITI: Kuna taarifa uko wapi, endelea Mheshimiwa Waziri, samahani.
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wake Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza ameuliza kama tuko kwenye uchumi wa kati na pia akaeleza kwamba uchumi wa nchi umeshuka. Sasa naomba nimpe taarifa tu, Mheshimiwa Conchesta kwamba la kwanza kwenye mpango wa ukuaji wa uchumi huwa tunaangalia tofauti ya uchumi kati ya mwaka mmoja na mwingine kwa ukuaji siyo kwa uzalishaji ni kwa ukuaji. Kilichotokea 2019 ambacho ulisema tumekua kwa asilima 7.1 ni kwamba hiyo 7.1 unachukua uzalishaji wote wa mwaka 2019 unatoa uzalishaji wote wa mwaka 2018 halafu unagawanya kwa uzalishaji wote wa 2018 unazidisha mara 100 kwenye market prices ndiyo unapata ukuaji wa asilimia Saba. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa 2020 ni kwamba uzalishaji wa mwaka 2020 bado ulikuwa ni mkubwa kuliko 2019 isipokuwa tofauti ya mwaka 2020 ukitoa ile 2019 ukagawanya 2019 ukazidisha mara 100 unapata asilimia 4.2. Kwa hiyo, ukuaji upo pale pale, uchumi haujashuka na kwamba tuko kwenye uchumi wa kati kwa sababu Tanzania tarehe Mosi Julai, 2020 tulitangazwa na Benki ya Dunia kwamba tumevuka kiwango cha chini cha kipato cha mtu mmoja mmoja kwa kuchukua uzalishaji wote gawanya kwa idadi ya watu kufikia dola 1,080 kuvuka 1,038 ambayo imewekwa kidunia. Ahsante.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri tunakushuru taarifa yako ni ya hakika ila anachoniambia namsikia huko akisema unazidi kumchanganya kisaikolojia. (Kicheko)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee.
MHE. ESTER A. BULAYA: Eeh! kwa kweli Mama endelea.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua kama kuna kitu ambacho kimeharibu nchi hii ni ma-book hawa vijana wetu wanatuandikia ma- book, ma-book unaweka kwenye kabati ndiyo maana mpaka sasa hivi tunalia kilimo miaka yote hii. Kwa sababu ya mipango ya ma-book. Unaandika Misahafu hiyo ma-book minus, plus sasa hiyo ndiyo mmeileta, sisi tunachotaka kuambiwa ni kwamba uchumi umetoka asilimia saba umekuja asilimia Nne na kwa sababu asilimia saba ndiyo imetufanya tuwe kwenye … sasa nimekosea nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima ueleze Watanzania kwamba hapana na hayo uyaseme katika lugha nyepesi, usituletee one hundred minus x uwaambie watu wakuelewe kwa sababu watu huku nimeuliza kitu ambacho wanauliza kwamba sasa tunarudi huku na je, utaweza kukopa kwa masharti nafuu hayo ndiyo utueleze kusudi tuweze kuelewa. (Kicheko)
MWENYEKITI: Kengele ya pili Mheshimiwa. (Kicheko)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi/Kicheko)