Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Issa Jumanne Mtemvu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kibamba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Mapendekezo ya Mpango wa mwaka 2022/2023. Nitajielekeza katika maeneo mawili tu muda ukinifaa sana; eneo la mapato katika sehemu ya mawasiliano na eneo lingine ni mwenendo wa riba hapa nchini na hasa eneo ambalo halijazungumzwa na wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayoifanya; sehemu kubwa wamesema wengine, lakini kwa jinsi anavyotuheshimisha kwenye majimbo yetu.

Pia nitumie nafasi hii kumshukuru sana kwa usikivu kama ambavyo nimeendelea kusema, Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii, kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kazi nzuri ya usikivu anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nakushukuru sana Mheshimiwa Spik ana Naibu Spika. Kwa kweli sisi tunaendelea kujifunza sana kila siku na kila wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi inayofanywa na Kamati ya bajeti mimi nikiwa ni Mjumbe wa Kamati inayoongozwa na kaka yetu Mheshimiwa Daniel Sillo na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Omari Kigua, tunaamini Waheshimiwa Wabunge wameiona na wameipongeza, nasi tumefarijika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na mchango wangu, katika eneo hili la makampuni ya simu, kuna changamoto sana. Tunakubali sana kwamba eneo hili la mobile sectors limechangia sehemu kubwa sana kwenye nchi yetu. Kwa uchache sana, katika kipindi cha miaka miwili wamechangia takribani Dola za Kimarekani milioni 441, takribani shilingi trilioni moja za Kitanzania. Vilevile wana mchango kwenye GDP takribani asilimia 5.2 na ziada ya mchango wao kwenye ajira kwenye sekta hii ni takribani watu 1,500,000. Hii ni karibu asilimia 2.6 ya idadi ya watu wetu wote wa takribani watu milioni 60 hadi 64.

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko jambo hapa ambalo nataka kusema na kubwa ni eneo linaloonekana kuna upotevu mkubwa sana wa mapato katika eneo la mawasiliano. Liko jambo ambalo ukiliangalia kwenye takwimu za miaka karibu nane, tisa; mwaka 2013 hao wenzetu kwenye sekta hii waliwahi ku-declare.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa average revenue per user; kiwango cha mtu moja moja katika kipato anachokipata kwa haya makampuni; kwa mtu mmoja kwenye idadi ya watu wote, ilikuwa ni takribani dola 5.5, kama 12,000 hivi. Katika kipindi hiki cha miaka miwili iliyopita, wame- declare tena punguzo takribani dola 2.3, yaani kama shilingi 5,000 au shilingi 6,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali linakuja hapa. Huo wakati ambao wanasema hayo kwa mtu average revenue per user ni 12,000, tulikuwa hatuna data wala tulikuwa hatuna mambo ya kuhamisha miamala ya kifedha. Leo tunajua wote idadi ya watu ni zaidi ya asilimia takribani milioni 60, 64. Nao wanasema takribani watu asilimia 42 ya population nzima wameji-engage kwenye mobile service. Sasa unaiona siyo chini ya milioni 30, lakini punguzo hili linatoka wapi kama leo tume-engage kwenye data, kwenye mobile transfer (miamala ya fedha)? Iko shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nimejitembeza kwenye nchi kadhaa kwenye jambo hili, nikakuta takribani nchi saba ziligutuka juu ya wizi mkubwa au upotefu wa mapato makubwa katika eneo hili, wakafanya Forensic Audit. Nchi kadhaa, mimi nitataja chache sana; baada ya kufanya Forensic Audit wamekuta upotevu mkubwa sana wa mabilioni ya namba. Hizi ni nchi kama Ghana, Kenya, Uganda, Rwanda, Malawi na nyingine nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwepesi, nchi nyingi zimeanza kufanya ukaguzi huu kuanzia mwaka 2003. Ndugu zetu Kenya na Uganda walifanya mwaka 2003. Uganda walifanya mwaka 2009. Hawa walikuta upotevu wa zaidi ya asilimia 300, increase; na waliweza kurudishiwa fedha zilizopotea kwa Kenya tu ni zaidi ya shilingi bilioni 600; kwa Uganda ni zaidi ya shilingi bilioni 600 na yenyewe.

Mheshimiwa Spika, nataka niseme kwa haraka, Ghana ambao juzi, mwezi wa Nane mwaka 202,1 wamefanya Forensic Audit kwenye data na mobile money transfer na wamemaliza juzi tu, wamekuta upotevu wa zaidi ya asilimia 300; Dola za Kimarekani milioni 418, hizi ni takribani shilingi trilioni moja za Kitanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba, sisi huwa tunachelewa sana. Leo Serikali ikaone inayo sababu ya kwenda kufanya Forensic Audit kwenye miamala hii kwenye haya makampuni yetu ya simu. Ni ukweli, wanafanya kati ya miezi mitatu hadi sita, wala siyo muda mrefu, watakuja kutuambia kwenye Bunge lako hapa ni kiasi gani tumeokoa kwenye declaration zao za revenue kila mwaka? Ni kiasi kikubwa sana tunapoteza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dakika chache kama nitaweza, niseme kidogo juu ya eneo hili la mwenendo wa riba. Maeneo mengi wamesema BoT imefanya kazi nzuri, Serikali imeingiza shilingi trilioni moja ili kupunguza zile riba na mambo mengine. Nataka kusema kuna wizi mkubwa hapa, nitumie tu hiyo lugha. Katika eneo hili wananchi wanaumizwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu viwili vinaitwa: moja, credit life insurance na nyingine ni takeover loans penalties. Niseme kwa haraka hili la kwanza, tutagundua Waheshimiwa Wabunge wote, tukichukua mkopo tunakatwa credit life insurance at once. Mkopo utachukua wa miaka mitano, lakini tunakatwa bima ya miaka mitano mara moja. Huu ni wizi mkubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikilisema hili, linaenda sambamba na suala la takeover loans penalties. Hawa Waheshimiwa Wabunge hapa wamechukua mikopo inawezekana kwa asilimia 13 au 14, lakini kuna benki nyingine zinatoa mikopo kwa asilimia 12. Katikati ya mwaka, katika mkopo wangu wa miaka mitano unapoamua kuuhamisha, unau-takeover, unau-liquidate pale, unauhamisha kwenye benki nyingine, kwa sababu ya faida ya difference of interest rate. Wanaku-charge asilimia tatu hadi tano bila wewe kujua. Hii ni kitu kibaya sana. Maana yake customer wanaumizwa na haki yao ya msingi ya kuhamisha mkopo wao kwa faida ya interest rate walizoziona kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda, namwomba sana Mheshimiwa Waziri kwenye eneo hili, sana ni mambo mawili; moja, atoe clear directive kwamba hakuna penalty ambayo inastahili kulipwa wakati mteja anahamisha mkopo wake. Hili muhimu sana, itawasaidia Watumishi wa Umma, itawasaidi Waheshimiwa Wabunge na wengine na wengine wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, hizi insurance, kama nimechukua mkopo unanikata miaka mitano kwa mara moja, leo nauhamisha mwaka wa pili, napeleka kwenye benki nyingine, naenda kukatwa insurance tena, wakati wewe umechukua yote ya miaka mitano. Kwa nini isifanywe kwa pro-rata; miaka yako miwili chukua, nikihama miaka mitatu kwenda benki nyingine, kule nikakatwe makato yale yale ambayo nilikuwa nimeshayapeleka kwenye benki ya awali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Huo ulikuwa mchango wangu wa leo. Ahsante sana. (Makofi)