Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ndanda
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia wakati huu wa Mpango. Nimesoma taarifa ya Mheshimiwa Waziri, pia nimesoma na taarifa ya Kamati ya Bajeti, nami niungane nao na niunge mkono taarifa hii iliyopo mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, naomba kukazia baadhi ya maeneo ambayo nilitamani sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up atueleze wanafikiria kufanya nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma taarifa ya Kamati ya Bajeti, wamesema wazi kwamba pesa ya Mfuko wa Jimbo kwa zaidi ya miaka sita, saba sasa hivi haijaongezwa. Kwa hiyo, fedha tuliyokuwa tunaipata mwaka 2015/2016 ndiyo hiyo hiyo inayopatikana sasa hivi wakati inflation imekuwa inaongezeka kila mwaka. Kwa hiyo, tunaomba ifanyiwe adjustment ili fedha hii iweze kuwa na manufaa yaliyokusudiwa pale mwanzoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetolea tu mfano wa Jimbo la Ndanda, tunapokea shilingi milioni 42, ambayo ni wastani wa shilingi milioni 2.6 kwa kila Kijiji. Sasa katika vijiji 77 unataka upeleke shilingi milioni 42 ili wale watu uweze kuwagusa wote kwa ajili ya miradi, unaweza ukachagua miradi michache, lakini wengine wanaweza wasielewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tumeona, na ninaishukuru sana Serikali, imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kwenda kujenga madarasa. Naishauri tena Serikali kwamba madarasa haya yanayokwenda kujengwa takribani 15,000 yaende sambamba na ajira zitakazotolewa. Kwa sababu kama unajenga madarasa 15,000, tafsiri yake unakwenda kuongeza wanafunzi kwenye shule zetu, unakwenda kuongeza na madarasa, lakini kama idadi ya walimu na watumishi itabaki pale pale, basi itakuwa ni tatizo. Hilo ni sawa sawa na jambo ambalo lipo kwenye vituo vya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ningependa kuishauri pia Serikali ni kuhusiana na mitambo pamoja na magari yaliyozagaa nchi nzima, kwenye Halmashauri zetu, kwenye hospitali zetu pamoja na kwenye Serikali Kuu. Magari haya yanazidi kuoza na mitambo hii inazidi kuoza. Kama Serikali wana nia njema, ni bora wakauza mapema kwa sababu tayari walishafanya tathmini ya vitu hivi, kwa hiyo, TR atoe kibali mapema yauzwe japo ipatikane fedha kidogo, lakini pia itapunguza kwenye asset badala ya kuonesha Serikali ina magari mengi, ina mitambo mingi ambayo ipo kwenye vitabu vyake, haitumiki, yanabaki kama makuukuu na mengine yanakuwa sasa kama vijumba vya majambazi huko kwenye maeneo yetu. Kwa hiyo, niwaombe sana waiangalie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, mimi naomba, nawe ni Mwenyekiti wetu, niliona siku moja picha yako umeanza kilimo cha korosho. Sasa utusaidie sana wakulima wa korosho tumekuwa kwenye adha kwa muda mrefu sana kwenye suala la Export Levy. Imefikia mwaka huu hapa ninapoongea nawe mkulima anakatwa takribani shilingi 979/=? Katika hii shilingi 979/= mgawanyo wake uko hivi: Export Levy peke yake inakatwa shilingi 499/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sasa sheria hii iletwe ndani ya Bunge na Mheshimiwa Waziri wa Fedha akae na Wizari ya Kilimo wajaribu kuipitia hii sheria na walete mapendekezo ili sheria hii ibadilishwe, kwa sababu imekuwa inakandamiza sana wakulima. Kwa mfano, hiyo Export Levy ni shilingi 499 kwa bei ya mnada huu uliopita. Kwa hiyo, mkulima jumla anakatwa almost shilingi 979. Kati ya hizi, direct deduction ni shilingi 260 au shilingi 270; na kiasi chote kinachobaki huwa kinakatwa indirect kwa kupitia hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia Sheria hii ya SDF ambayo ilitungwa hapo nyuma kwa ajili ya kutaka kusaidia wakulima, imekuwa kama ni marudio kwa sababu ukiangalia kuna direct deduction ambayo ni pesa ya ushirika shilingi 100, pesa ya CBT shilingi 25, pesa ya TARI shilingi 25, pesa ya Halmashauri shilingi 56, lakini pia kuna pesa ya mchango wa elimu shilingi 30, pesa ya Halmashauri ndiyo sawa na mchango wa elimu, almost, lakini pia ukilinganisha na usafirishaji ni shilingi 50. So in total, unapata karibia shilingi 979.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana tuwashauri hawa ndugu zetu, Wizara ya Kilimo pamoja na Wizara ya Fedha wajaribu kuipitia hii sheria na wailete hapa ndani Bungeni tuibadilishe. Korosho siyo zao la mkoa mmoja au mikoa miwili, mitatu; korosho limekuwa zao la Kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala la madeni. Kuna madeni mengi sana ya ndani, mengine yanayotokana na mazao ya kilimo, lakini mengine yametokana na maamuzi ya Serikali. Kwa mfano, ukienda kwenye korosho, madeni ya Bodi pamoja na Vyama vya Ushirika ni takribani shilingi bilioni 40. Tunaomba sana madeni haya yahamishiwe Hazina kwa sababu Bodi haiwezi kuyalipa na vyama vile vya msingi kule kwetu hawawezi kuyalipa, yamekuwa mzigo kwao, yanachafua vitabu vyao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye Bodi ya Pamba, wanadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 60. Pia ni sawa sawa ukienda kwenye tumbaku. Kwa hiyo, tunaomba sasa Mheshimiwa Waziri aridhie madeni haya yachukuliwe na Hazina yaweze kulipwa kwa sababu ni mitaji ya watu waliokuwa wanafanya biashara na Serikali na maeneo mengine kutokana na maelekezo ya Serikali. Kwa hiyo, Wakandarasi wa ndani wanao-supply vitu mbalimbali kwenye huduma za kilimo, kwenye huduma za mashule kwa mfano, Shule ya Sekondari Ndanda, Shule ya Sekondari Chidya watu walipeleka pale chakula, sukari, unga kwa ajili ya wale Watoto na Halmashauri zetu zinaelemewa, hawawezi kulipa tena. Tunaomba Hazina wachukue haya madeni na wayafanyie kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema hapo mwanzoni, kuna miradi mikubwa sana ya kimkakati iliyoelekezwa kwa upande wa kusini. Kwa mfano reli ya Kusini hatujui mpaka sasa wamefikia hatua gani na nini kinakwenda kufanyika? Tuna barabara zetu za kiuchumi ambayo ni barabara inayoanzia Mtwara kufika Newala - Masasi - Nachingwea kwenda Liwale kuja kutokea Lupilo kuja kutokea mpaka Morogoro kwa maana ya kutaka kufungua ukanda huu wa kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutamshukuru sana Mheshimiwa Rais, endapo wazi kabisa ataamua sasa kufanya kazi na hii barabara, kwa sababu pia ndiyo barabara inayotokea Songea kupitia Namtumbo kwa sababu tunatamani sisi wakati fulani siyo lazima tufike Dar es Salaam tunapoamua kuja huku, lakini pia ni sehemu ya kufungua ukanda huu wa kusini, tusiwe na barabara moja tu ya kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia utakumbuka kulikuwa na suala hapa la Mtwara Corridor ambayo ilikuwa ni makusudi mazima ya kwenda kuboresha Bandari ya Mtwara. Katika mikakati ya sasa inayotajwa, naona kama habari za Mtwara Corridor zimesahaulika kabisa. Sijasikia ikiwa inatajwa karibuni ndani ya Bunge kwa sababu sisi Wabunge tunaongea kidogo, lakini hata Wizara nayo haijawahi kutuambia habari hii na sijaiona huko.
Kwa hiyo niwaombe sana, kama inawezekana turudishe tena huu utaratibu wa Mtwara Corridor ili kuweza kusaidia Mikoa ya Kusini kwa maana ya Mtwara, Lindi pamoja na Ruvuma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la mwisho kabisa niliseme na kwa kusisitiza, tuendelee kuangalia sasa, tumeona hapa Mheshimiwa Rais wameridhia sasa na wameondoa ile withholding tax kwenye mazao mbalimbali. niipongeze sana Serikali kwa hatua hii. Pia tunaomba, sisi hasa tunaotoka kwenye maeneo yanayolima korosho waangalie na uwezekano wa kuja kufanyia maboresho kwenye Sheria ya Export Levy kwa sababu imekuwa yenye maumivu makubwa kwa wakulima na haina tija tena kama ambavyo ilikusudiwa mwanzoni, kwa hiyo sasa hivi ije ikiwa na utaratibu mpya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana na naomba Serikali wazingatie hayo machache kama sehemu ya mchango wangu. (Makofi)