Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kudumu Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu shughuli za Kamati hizo kwa Mwaka 2021

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuwa mchangiaji wa hoja ambayo imewasilishwa mezani. Nitajielekeza kwenye hoja ya Kamati ya Ulinzi, Mambo ya Nje na Usalama.

Mheshimiwa Spika, kwa kuanza napenda kutumia nafasi hii kwa niaba ya wananchi wa Mafinga Mjini, kukupongeza kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge letu. Mwenyezi Mungu akusimamie na kukuongoza; hizi ni salamu ambazo nimetumwa na Wanamafinga nizifikishe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya salamu hizo, kama mara zote ambavyo huwa nasema kwamba, Mheshimiwa Rais ndio mwanadiplomasia namba moja. Pale anapokuwa amefanya kazi ametimiza majukumu yake kama mwanadiplomasia namba moja, tunao wajibu wa kumpongeza na kumtia moyo. Mimi sitaishia tu kumpongeza na kumtia moyo, lakini nitafanya na takwimu kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na kazi nzuri ya diplomasia, kama mwanadiplomasia namba moja ambayo Mheshimiwa Rais anaifanya, nchi yetu imeendelea kupata fursa mbalimbali za kibiashara, hasa katika eneo letu la afrika Mashariki, lakini na maeneo mengine.

Mheshimiwa Spika, hapa unipe ruhusa nitoe takwimu kidogo tu; kutokana na kazi nzuri anayoifanya Mheshimiwa Rais, biashara kwa maana ya trade balance kati yetu sisi na kenya, kwa mara ya kwanza tumefanya vizuri sana katika kipindi cha Januari mpaka Septemba, 2021. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kwa takwimu kibiashara, mauzo yetu katika nchi Jirani ya Kenya, kama wenzetu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na hii naitoa kulingana na takwimu za ile Kenya National Bureau of Statistics kwamba, mauzo yetu yameongezeka kutoka dola za kimarekani milioni 347 sawasawa na bilioni za Kitanzania 802 mpaka dola za kimarekani milioni 396, sawasawa na fedha za Kitanzania bilioni 915.

Mheshimiwa Spika, hili ni ongezeko kubwa na ni ongezeko ambalo mara nyingi, trade balance kati yetu sisi na wenzetu, wenzetu wamekuwa wakituzidi, lakini kutokana na kazi nzuri ambayo Mheshimiwa Rais, kama mwanadiplomasia namba moja ameifanya, tunaona sasa kama Taifa letu na sisi trade balance kati yetu sisi na majirani zetu sasa inaendelea kukua. Kwa hiyo, napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu, kama Kamati tulikuwa na kilio cha muda mrefu na kuishauri Serikali kupeleka maafisa katika balozi zetu, ili waendelee kutafuta fursa za kiuwekezaji, fursa za biashara na fursa mbalimbali za kiuchumi kwa ajili ya Taifa letu. Ninapozungumza hapa Wizara imefanikiwa kupeleka maafisa 137 katika balozi zetu 44 ambao ni sawa na wastani wa asilimia 63% kati ya maafisa 215 wanaohitajika. Hii ni hatua kubwa ambayo itaenda kuongeza ufanisi katika balozi zetu, itaenda kuongeza utendaji na zaidi ya yote kung’amua zaidi fursa za kiuwekezaji na hivyo kuliongezea Taifa letu mapato zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kama ambavyo tumesema katika Kamati yetu, bado kuna shida kubwa ya uchakavu wa majengo na uhaba wa majengo katika balozi zetu. Kama taarifa yetu ilivyojionesha ni Balozi nne tu za Cairo, Lusaka, Maputo na Harare ndizo ambazo maafisa wetu au Serikali yetu ina majengo kwa maana ya ofisi na ina majengo kwa maana ya makazi ya maafisa wetu wa ubalozi.

Mheshimiwa Spika, jambo hili linaifanya Serikali kubeba mzigo mkubwa sana wa kugharamia pango kwa ajili ya ofisi na pango kwa ajili ya makazi ya maafisa wetu na hivyo kuwa ni mzigo mzito sana kwa Serikali. Ndio maana Kamati yetu imekuwa ikishauri na inaendelea kushauri kwamba, Serikali kwa maana ya Hazina, waweze kutoa fedha ili ule mpango mkakati ambao Wizara ya Mambo ya Nje imejijengea au imejiwekea wa miaka 15 wa kuondokana na kupangisha na kukodi majengo ya ofisi na makazi ambayo hata kiusalama sio nzuri sana, basi uweze kutimia, lakini utatimia ikiwa tu wenzetu hawa watapatiwa fedha kama ambavyo Kamati imeelekeza.

Mheshimiwa Spika, hapa nitatoa mfano mdogo. Kwa mfano, katika Ubalozi wetu wa Marekani, pale Washington DC, tuna jengo ambalo ikiwa Serikali itatoa fedha kiasi cha bilioni 3.8 likakarabatiwa, maana yake ni kwamba, lile jengo ambalo tunalitumia sasa hivi tutahama na hivyo, lile jengo tunalolitumia sasa hivi tutalipangisha na kwa mwaka tutapata wastani wa bilioni 2.4. Kwa hiyo nitoe wito na ushauri kama Kamati ambavyo imesema tukitoa fedha hizi kwa Wizara tukakarabati majengo maana yake kwanza tutaokoa fedha ambazo tunapanga sasa, lakini pili, tutazalisha mapato zaidi kwa ajili ya kuendeshea shughuli zingine za Serikali.

Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano mdogo. Kwa mfano, katika Ubalozi wetu wa Marekani, pale Washington DC, tuna jengo ambalo, ikiwa Serikali itatoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 3.8 likakarabatiwa, maana yake ni kwamba, lile jengo ambalo tunalitumia sasa hivi tutahama na kulipangisha na kwa mwaka tutapata wastani wa shilingi bilioni 2.4.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo natoa wito na ushauri ushauri kama Kamati ambavyo imesema, tukitoa fedha hizi kwa Wizara, tukakarabati majengo, maana yake kwanza tutaokoa fedha ambazo tunapanga sasa, lakini pili, tutazalisha mapato zaidi kwa ajili ya kuendeshea shughuli nyingine za Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili katika Kamati yetu ambalo tumeliona, tulikuwa tumeshauri kwamba Magereza wajitosheleze kwa chakula. Tunapozungumza hivi sasa, Magereza kutokana na kazi nzuri wanayofanya, wameokoa takribani shilingi bilioni 11 ambazo zilitokana na kuwalipa wazabuni kwa ajili ya chakula kwa wafungwa na mahabusu.

Mheshimiwa Spika, ushauri wetu kama Kamati na mimi kama Mjumbe wa Kamati, ninashauri ili Magereza iweze kujilisha na kuzalisha ziada, basi kile ambacho kinakuwa kimepangwa na Serikali katika bajeti, fedha zile ziende. Sambamba na kuwapa fedha ambazo zitawasaidia kuwa na uwezo katika kujenga miundombinu ya umwagiliaji, pia Jeshi la Magereza tunapozungumza hivi sasa ukiacha yule Mkuu wa Magereza (Commissioner General of Prison) ambaye kimuundo anatakiwa kuwa na wasaidizi wanne, hana hata msaidizi mmoja. Pia kimuundo kuna ma- Deputy ambao wanatakiwa kuwa kama 17, lakini yuko mmoja tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni wakati wa Serikali sasa kuliwezesha Jeshi la Magereza kifedha na nyenzo ili liweze kuzalisha kwa ajili ya kujilisha kama ambavyo wameokoa hizo shilingi bilioni 11, lakini pia waweze kuzalisha kwa ajili ya ziada. Haya yatawezekana ikiwa tu tutawapa fedha, na ile ikama yao kwa maana ya muundo wao yule Mkuu wa Magereza, apatiwe wasaidizi wake.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kutokana na muda, naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)